Suleiman Msuya
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chadema,
Edward Lowassa ametoa waraka akieleza alichokiita masikitiko yake kwa jinsi Serikali
inavyoelekea kulitumbukiza Taifa kwenye mkwamo.
Katika waraka huo
alioutuma jana kwa vyombo vya habari kupitia Msemaji wake, Abubakar Liongo,
Lowassa alisisitiza kwamba maandamano ya Ukuta yatakayofanyika kesho yatakuwa
ya amani.
“Tumelazimika kutangaza Operesheni
Ukuta kupinga ukandamizaji huo. Binafsi nafurahishwa na kutiwa moyo na jinsi Watanzania
walivyoipokea Operesheni hii licha ya vitisho vya Dola,” alisema Lowassa.
Kwa mujibu wake, kukutana kwake
na Rais John Magufuli na kusalimiana katika Jubilei ya Miaka 50 ya Ndoa ya Rais
mstaafu Benjamin Mkapa, kulikuwa ni mwanzo wa juhudi za kuondoa sintofahamu
iliyokuwapo.
Lakini akasema kitendo cha
juzi yeye na viongozi wenzake wa Chadema kukamatwa na Polisi, kimerudisha nyuma
juhudi hizo.
“Cha kushangaza wenzetu
hawako tayari kuupokea mkono huo. Jana (juzi) tukiwa kwenye kikao cha
kujadiliana jinsi ya kuunyosha zaidi mkono huo, Jeshi la Polisi likaja na
kuukata kwa kutukamata,” ilieleza sehemu ya waraka huo.
Lowassa alisema anasikitishwa
na utaratibu wa Polisi kunyanyasa na kusumbua viongozi na wanachama wa Upinzani hasa Chadema.
Waziri Mkuu huyo wa zamani
alisema amepokea simu nyingi kutoka kwa viongozi wastaafu na watu wengine
mashuhuri na wa heshima kubwa nchini kuwataka wazungumze na Serikali ili
kuepusha Taifa kutumbukia kwenye machafuko.
Alisema kitendo hicho
kwake binafsi kimezidi kumwimarisha na kumpa nguvu zaidi ya kudai demokrasia na
kuheshimu Katiba, ambayo viongozi waliapa kuifuata na kuitetea.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu
alisema amelazimika kushika kalamu na kuandika
masikitiko yake, kwa jinsi Serikali ya CCM inavyoelekea kulitumbukiza Taifa kwenye mkwamo na machafuko ya kisiasa.
“Sote tunafahamu hali ya kisiasa ilivyo tete kwa sasa nchini. Serikali
inaukandimiza Upinzani na demokrasia kwa jumla. Tumelazimika kutangaza Operesheni
Ukuta kupinga ukandamizaji huo,” alisema.
Alisema
siku zote Chadema na Ukawa wanalitakia amani
na utulivu Taifa la Tanzania, lakini vitendo vya Polisi
vimewapa wasiwasi Watanzania.
Kwa takriban
mwezi mmoja sasa kuna hali ya sintofahamu kati ya Polisi, Serikali na vyama vya
siasa baada ya Jeshi hilo na Rais Magufuli kutangaza kuzuia mikutano ya hadhara
hadi mwaka 2020 na kutaka ifanywe na
wabunge katika majimbo yao tu.
Kauli
hiyo ilisababisha mijadala kupitia mitandao ya kijamii na vyama vya siasa, hata
kuzaliwa Ukuta ambao unarajia kufanya mikutano na maandamano kuanzia kesho
nchini kote kwa kinachodaiwa ni kupinga ukandamizaji wa demokrasia na udikteta.
Tangu
Ukuta utangazwe, habari katika kila kona ya nchi imekuwa ni Ukuta hali ambayo
imesababisha kuwapo kwa taharuki huku kila upande ukitunisha misuli na
kukosekana kwa majadiliano ya kutatua.
Mvutano
huo ulipelekea Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Msajili wa
Vyama Siasa, viongozi wa dini wanasiasa maarufu na makundi kujitokeza
mbele ya vyombo vya habari na kukemea na kuomba mazungumzo yafanyike, ili
kutoingiza nchi kwenye machafuko.
0 comments:
Post a Comment