* Kasi na viwango vya Sitta vilipitiliza, ikavuruga
* Makinda ajitolea kufunda wabunge vijana
Neema
Mgonja
ALIYEKUWA
Katibu Msaidizi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, John Joel amesema hakuna
uhusiano wa karibu kati ya taaluma ya Sheria na Uspika wa Bunge, akitolea mfano
wa uongozi wa Samuel Sitta ambaye ni mwanasheria na Anne Makinda.
Alisema kazi
ya uspika inaongozwa zaidi na kanuni za Bunge na busara za Kiti cha Spika
kuliko sheria, ndiyo maana Bunge la Sitta lilipitiliza na kufanya mambo yaliyoingilia
kazi za Serikali ikilinganishwa na la Makinda.
Joel
alitoa kauli hiyo alipozungumza kwenye mahojiano maalumu na gazeti hili
nyumbani kwake Dodoma hivio karibuni.
“Hakuna
ulazima wa kuwa na Spika mwanasheria, uspika unaongozwa na kanuni, Katiba ya
Jamhuri ya Muungano inatoa nafasi kwa raia yeyote mwenye sifa za kugombea
ubunge kugombea uspika, na kanuni zinatoa mwongozo wa uendeshaji wa Bunge.
“Busara
ikitumika zaidi inakuwa ndiyo msingi wa kuongoza Bunge, wabunge ni watu ambao kila
mmoja ana tabia zake, ukisema utumie sheria kwenye kila kitu, lipo tatizo la kuongoza
wabunge kwa kuwa ni wanasiasa wanatakiwa kuwa huru. Ukiwabana sana wakati
mwingine unaweza kupata Bunge ambalo si hai, ndiyo maana upo utaratibu wa
kufuata kanuni.”
Hata
hivyo, Joel ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema: “Faida kubwa ya kuwa na Spika
mwanasheria – pengine ni wakati wa utungaji sheria. Labda hapo kwa wanasheria
wanapata nafuu ya kuwa wanajua mambo mengi, lakini hata hivyo, bado Kiti cha Spika
kina wataalamu wengi wakiwamo wa sheria ambao muda wote wanafanya kazi
kumsaidia Spika.”
Utendaji
wa Sitta
Akizungumzia
utendaji wa Sitta aliyeongoza Bunge la tisa kwa miaka mitano, Joel alisema
Sitta alijikita katika kuongoza Bunge kwa dhana aliyoijenga ya kasi na viwango.
Alisema
kutokana na mtazamo huo, alijikuta Bunge aliloongoza likifanya kazi ambayo
haikustahili kufanywa kwa kuwa lilikwenda mbele zaidi.
Joel alifafanua
kuwa Sitta alikuwa na mtazamo wa Kasi na Viwango na si mtazamo wa sheria, ila alitazama kufanya
kazi kwa haraka na viwango.
“Bunge
lake lilipitiliza, matokeo yake Serikali ikawa inabaki nyuma kulingana na mambo
yaliyokuwa yakifanywa na Bunge, ikasababisha wabunge kufanya kazi isiyo yao,
walianza kuingilia kazi za Serikali,” alisema.
Joel alieleza
kuwa hayo yalisababishwa na Sitta kwa kuwa alitaka mambo yaende haraka na hata kusababisha
Serikali kujikuta imeachwa nyuma.
“Unakuta
wabunge wako kwenye vikao badala ya Serikali kuwa mtekelezaji, wabunge
wanakwenda kuhimiza utekelezaji, walifanya kazi zisizo zao kabisa.
“Lakini
hiyo ilitokana na mtazamo wa Sitta kutaka mambo ya kasi na viwango, kwa hiyo
kwenye kuvutana huko kwenda na kasi lazima kuna aliyebaki nyuma, ndiyo
yalifanya Serikali kuachwa nyuma,” alisema Joel.
Makinda
Naibu
Katibu huyo mstaafu akizungumzia utendaji kazi wa Spika wa Bunge la 10, Makinda
alisema alijikita zaidi kulea wabunge
kwa maadili, huku akieleza kuwa alirudisha hadhi ya Bunge kwa kuliwezesha
kujitegemea na kuachana na kasumba iliyokuwa imejengeka ya wabunge kupokea takrima
na bahasha zisizo rasmi.
Kuhusu Spika
huyo aliyehudumu katika Bunge kwa miaka 24 kabla ya kustaafu, alisema ingawa alikumbana
na changamoto mbalimbali lakini alitumia muda mwingi kujenga Bunge, kwa kuelekeza
wabunge kwenye maadili.
Huku akimwita
‘mama wa Bunge’, Joel alisema Bunge chini ya Makinda lilikuwa na changamoto
nyingi hasa kwa kuwa ndicho kipindi ambacho kilikuwa na mabadiliko makubwa
likishuhudia ujio wa wabunge wengi vijana.
Alisema ingawa
vijana waliingia kwa kiasi kikubwa, alitumia ulezi kuwarudisha kwenye mstari
unaotakiwa na kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.
“Katika
uongozi wake, yeye alitaka kuwarudisha wabunge wajue wajibu wao kama wabunge,
na mipaka yao ya namna ya kufanya kazi…Makinda alikuwa na mtazamo wa ulezi
zaidi, tukumbuke kwamba tangu tulipoanza mfumo wa vyama vingi yalijitokeza
mambo mengi.
“Zamani
Bunge lilikuwa kwa watu waliostaafu na watu wasio na kazi, lakini baada ya
mfumo wa vyama vingi na siasa kukua, ukaonekana umuhimu wa kuwapo kada
mbalimbali, kwa hiyo Makinda akakutana na changamoto ya wabunge vijana,”
alisema.
“Mtazamo
wa Makinda hasa baada ya kuona yuko kwenye Bunge la vijana wakiwamo ambao
hawakupata kufanya kazi kwingine na hiyo kuwa kazi yao ya kwanza, ilimfanya
ajikute ameingia kwenye enzi za ulezi zaidi, akifundisha vijana maadili,”alisema
Joel.
Takrima
Katika
hatua nyingine, Joel alisema Makinda
tofauti na maspika waliomtangulia, alipenda Bunge liwe lijitegemee, ikiwa ni
pamoja na kurudisha heshima na hadhi yake kama Bunge.
Alifafanua,
kwamba kabla ya uongozi wa Makinda, Bunge lilikuwa na taratibu ya kuruhusu kupokea
fedha kutoka nje, zikiwa ni gharama zilizokuwa zikilipwa kama takrima kwa
wabunge, jambo ambalo Spika Makinda hakupendezwa nalo.
Aliongeza
kuwa Makinda aliona utolewaji wa fedha za ziada kwa wabunge ambao pia walikuwa
wakigharimiwa na mhimili huo, ni jambo ambalo halipendezi na linarudisha nyuma
utendaji wake kiuadilifu.
“Awali
wabunge walipokea bahasha sana, kwa mfano wakienda kutembelea sekta fulani walilipwa,
siwezi kuita rushwa, lakini ni kama takrima hivi, jambo ambalo yeye akiwa Spika
hakulikubali akaondoa huo mfumo wa kufadhiliwa,” alisema.
“Unajua
mtu akikufadhili utataka kumfanyia mazuri, sasa unakuta wabunge wanakwenda
kutembelea sehemu Fulani, wanapewa fedha na Bunge, na tena hiyo taasisi iwape
fedha, ufanisi unakuwa si mzuri, kwa hivyo yeye Spika ambaye alikuwa na mtazamo
tofauti alikuja na mbinu nyingine ya kukataa mifumo hiyo ya takrima kwa wabunge,”
alisema Joel.
Mchango
wa Sitta
Katika
uongozi wake wa Bunge, Sitta aliyejulikana kwa jina la ‘Spika wa Kasi na
Viwango’, Bunge lilibadili kanuni ambazo kwa mara ya kwanza kamati muhimu za
fedha, ikiwamo ya Mashirika ya Umma, ya Fedha za Serikali Kuu na ya Serikali za
Mitaa, zilisimamiwa na wenyeviti wa vyama vya Upinzani.
Baada ya
kuundwa kwa kanuni hiyo, Bunge lilishuhudia vyama vya Upinzani kupitia kwa
aliyekuwa Mbunge wa Karatu, Dk Wilibrod
Slaa (CHADEMA) na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye sasa ni Mbunge
wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT), wakitumia kamati hizo kuimarisha upinzani
ndani na nje ya Bunge kwa kuisulubu Serikali.
Mafanikio
mengine yanayohusishwa na Sitta, ni pamoja na kuanzishwa kwa kipindi cha
maswali ya papo kwa hapo kwa Waziri Mkuu, ambacho kilirithiwa na mabunge
yaliyofuata baada ya uongozi wake.
Uongozi
wa Spika huyo wa zamani, pia anatajwa kuwa ndio uliolipa Bunge uhuru mkubwa
kiasi cha kufanikiwa kuiangushwa Serikali wakati aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward
Lowassa, alipolazimika kujiuzulu wadhifa wake sambamba na Baraza lote la
Mawaziri.
Ni kutokana
na uongozi huo wa Sitta, ndani ya CCM kuliibuka makundi yaliyohasimiana ambayo
yalifikia hatua ya Sitta kunusurika kuvuliwa uanachama kwa kuonekana kuwa kiini
cha msuguano wa makundi hayo, yaliyokuwa yakihatarisha umoja na mustakabali wa
chama tawala.
Msuguano
huo uliendelea hata Sitta alipotoswa kwenye kinyang’anyiro cha uspika hata
wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita, ambapo Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Jakaya
Kikwete alipokiri kuwa kama CCM ilipita salama katika uchaguzi huo, basi
itaendelea kudumu.
0 comments:
Post a Comment