Edith Msuya na Edith Msuya
WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imesema
tukio lilitokea maeneo ya Mbagala Mbande, Wilaya Temeke la polisi kuvamiwa na
majambazi ambapo askari wanne waliuawa na raia wawili kujeruhiwa ni shambulizi dhidi
ya askari polisi, wakidai kuna viongozi wa kisiasa wanaohusika na tukio hilo.
Mbali na kauli hiyo, jeshi hilo limepiga
marufuku mikutano yote ya ndani ya vyama vya siasa ya kiutawala, kiutendaji hata ya harusi likieleza mikutano hiyo ina
viashria vya moja kwa moja kuhamasisha vurugu, hatimaye kuvunja sheria za nchi.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Kamishna
Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Mssanzya alisema: “Ni dhahiri
wahalifu hao walikuwa na kusudio moja tu la kuwashambulia askari polisi. Wapo
viongiozi wa kisiasa ambao wamesikika katika majukwaa ya kisiasa wakihamasisha
wafuasi wao wawashambulie askari wa Jeshi la Polisi.”
Licha ya kuwahusisha baadhi ya viongozi
wa kisiasa na tukio hilo Mssanzya alisema tukio hilo ni la uhalifu katika
mazingira ya ulipizaji kisasi
Aliwataja askari waliouawa katika tukio
hilo kuwa ni E.5761 CPL Yahaya, F.4660
CPL Hatibu, G.9524 PC Tito na G.9996 PC Gastone huku waliojeruhiwa wakiwa ni
Ally Chiponda na Aziz Yahaya wote wakazi wa Mbade.
Alisema katika tukio hilo majambazi hayo
yalifanikiwa kupora silaha mbili aina ya SMG na risasi 60 na hakuna fedha au
mali ya benki iliyoibwa au kuharibiwa.
“Kutokana na majambazi hayo kutochukua
kitu chochote, ni dhahiri kuwa wahalifu hao walikuwa na kusudio moja tu la
kuwashambulia askari polisi,”alisema Kamishna Mssanzya.
Kwa mujibu wa Kamishna Mssanzya, baada
ya tukio hilo baadhi ya watu waliandika mitandaoni kubeza na kukejeli mazoezi
ya kawaida yanayofanywa na Jeshi la Polisi huku wengine wakiandika ujumbe wa
kushabikia tukio hilo la kuuawa kwa askari polisi.
“Wengine walidiriki kuandika ujumbe
unaosema kwamba endapo watapigwa na polisi Septemba Mosi, basi viongozi wa
Jeshi la Polisi wawaondoe askari wanaoishi uraiani na kuwarudisha kambini la
sivyo watawashambulia:
Natoa onyo kali kwamba watu hao waache
tabia hiyo…; tutawafuatilia kwa karibu kila andiko na tamko lenye mlengo wa
kushabikia au kuhamasisha uhalifu aina yeyote kupitia mtandao ya kijamii. Wote
walioandika au kusema kwa leno la kushabikia uhalifu huo tutawakamata ili
sheria ichukue mkondo wake,”alisema Mssanzya.
MIKUTANO
Akitangaza kupiga marufuku mikutano ya
ndani na kiutawala kwa vyama vya siasa, Mssanzya alisema polisi imebaini
mikutano mingi inayoitishwa ina nia ya kuhamasisha vurugu jambo ambalo ni
kinyume cha sheria.
“Jeshi la Polisi halijazuia mikutano ya
ndani, lakini katika kufuatilia suala hilo mikutano hiyo imekuwa ikitumika na
watu kugawana vifaa vya kazi na kuchochea wananchi kufanya mapambano, hivyo
tunapiga marufuku mikutano yoyote ya ndani, hata kama ni ya harusi,” alisema.
SEPTEMBA MOSI/ MAZOEZI
Akijibu swali kuhusu askari kufanya
mazoezi ya kijeshi hadharani kamishna Mssanzya alisema: “Ndiyo, mazoezi hayo
yanafanywa kwa ajili kulinda usalama wa nchi na moja ya mambo hayo ni Septemba
Mosi, nguvu zitatumika na zitaongezeka kwa mujibu wa sheria.”
SHUHUDA
Mmoja wa mashuhuda wa aliyekuwa eneo
hilo wakati tukio hilo lilipofanyika, Rashid Katimba aliliambia gazeti hili
kwamba mauaji hayo yalitokea wakati wakati yeye akinunu matunda.
“Ndipo walipotokea hao majambazi wakiwa
na silaha na kuanza kuwashambulia polisi. Kwa hali ilivyokuwa, nilijikuta
nimejitumbukiza kwenye mtaro pamoja na mantunda yangu ili kujificha,” alisema
Katimba.
Aliongeza: “Kwa kweli wale polisi
wameuawa kinyama na inavyoonyesha majambazi husika walikuwepo maeneo hayo ya
Mbande Mwisho kwa muda mre wakitafuta nafasi ya kuvamia.”
Alisimulia kwamba aliona majambazi
watano, wote walikuwa na pikipiki aina ya boxer na walipomaliza kutekeleza
mauaji hayo walitokomea kuelekea maeneo ya Mvunde kupitia Kisimba kuelekea njia
ya Chanika.
“Mbande Mwisho hali si nzuri kabisa hali
niliyoshuhudia si ya kawaida, kwa jumla hali inatisha,” alisema.
MCHAMBUZI
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya
kijeshi wanalihusisha tukio hilo na watu waliopitia mafunzo ya kijeshi
wakieleza kuwa katika hali ya kawaida, mtu anayeweza kulenga risasi usoni au
kichwani kama majambazi wa Mbande.
“Lile si tukio la kawaida, hata
waliotekeleza lazima watakuwa wamepata mafunzo ya kijeshi tofauti nay ale ya
polisi. Hilo naliamini kwani kuna watu wengi waliopata mafunzo ya kijeshi hata
nje ya nchi ambao waliacha kazi hiyo na sasa haijulikani wanafanya kazi gani au
walipo,” alisema mmoja wa wataalamu wa kijeshi aliyeomba kuhifadhiwa jina lake.
Alisema ipo hatari kwa watu hao kutumia
vibaya mafunzo waliyopata wakiwa uraiani kama hakuna ufuatiliaji wa vyombo vya
usalama, akiongeza kuwa matukio kama hayo yanaweza kutekelezwa pia na askari
walio kazini iwapo hawatapata uangalizi wa kutosha ikiwapo stahiki zao kwa
wakati kwani hawafanyi biashara.
0 comments:
Post a Comment