Yusufu Makamba |
*Amtaka
asisubiri nyumba kukamilika
*Yeye
asema safari imeiva, anahamia
Na Mashaka
Mgeta
KATIBU Mkuu mstaafu wa CCM, Yusufu Makamba amesema Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa, hana sababu ya kubaki Dar es Salaam badala ya kuhamia Dodoma
wakati huu.
Makamba aliyeshika nafasi hiyo kati ya mwaka
2007 na 2011, alisema hayo kwenye mahojiano maalumu na JAMBO LEO nyumbani
kwake, Tegeta, Dar es Salaam juzi.
Akizungumzia masuala ya siasa na utawala
wa Serikali ya Awamu ya Tano, alisema uamuzi wa Rais John Magufuli kuhamishia Serikali
Dodoma, ni sahihi na unapaswa kutekelezwa
kwa kasi anayoihitaji.
Alisema wapo viongozi na watumishi wa
umma wanaotumia kigezo cha ukosefu wa makazi na ofisi kutohamia Dodoma kwa
wakati huu.
“Nilimsikia hata Waziri Mkuu akisema
anasubiri nyumba ya kule juu imalizike ndipo ahamie Dodoma, pale (Dodoma) kuna
makazi anayofikia hata sasa, kwa nini asiende kukaa humo mpaka hiyo nyumba
itakapokamilika,” alisema Makamba.
Alisema Waziri Mkuu kama ilivyo kwa
mawaziri wengine, wana makazi na ofisi ndogo za kufanyia shughuli zao hasa
wanapokuwa mjini humo wakati wa mikutano na vikao vya Bunge.
Alihoji: “Kwani wanapokuwa Dodoma
wanaishi wapi, wanafanyia wapi kazi zao, si wana ofisi ndogo …ninavyojua ni
kwamba kila Waziri ana nyumba kule, mimi ninaijua ya mwanangu Januari,”
alisema.
Januari Makamba ni Waziri wa Nchi Ofisi
ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano ambaye ni Mbunge wa Bumbuli kupitia
CCM.
Makamba alitoa mfano, kwamba
alipoteuliwa mara ya kwanza kuwa Katibu Tarafa, miaka ya mwanzoni mwa 1970,
alikwenda kwa Waziri Mkuu wakati huo, Rashid Kawawa (marehemu) kudai kwamba
hapana nyumba kwa ajili yao.
“Kawawa aliniambia, Makamba walimu wako
huko wanaishi wapi, kuna watumishi wengi sasa ukiulizia suala la nyumba ya
kuishi hata hiyo kazi utaikosa,” alisema na kuongeza:
“Sasa hawa viongozi na watumishi wajue
kwamba Dodoma wapo waandishi wa habari, walimu, wanajeshi, polisi wakifanya
kazi, kuhamia Dodoma kunatekelezwa kwa dhamira licha ya kuwapo changamoto hasa
za miundombinu,” alisema.
Julai 23 Rais Magufuli alitangaza Serikali
kuhamia Dodoma ili ifikapo mwaka 2020, mji huo ulio katikati ya nchi uwe Makao
Makuu halisi ya nchi.
Majaliwa
Hata hivyo, akizungumza jana na
watumishi wa ofisi yake walio Dar es Salaam Waziri Mkuu aliwataka kujiandaa
kisaikolojia kwani safari ya Dodoma imeiva.
Hivi karibuni Waziri Mkuu alinukuliwa na
vyombo vya habari akieleza kuwa ifikapo Septemba atakuwa amehamia Dodoma.
“Mtambue kuwa uamuzi wa Serikali kuhamia
Dodoma ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambao chimbuko
lake ni agizo la Oktoba mosi, 1973 kwenye Mkutano Mkuu wa 16 wa TANU,” alisema
Majaliwa na kuongeza:
“Tangu wakati huo kuna juhudi
zilizofanyika ili kuandaa miundombinu na hata awamu ya nne ilisimamia kwa
kiwango kikubwa uwekaji wa miundombinu hiyo."
Waziri Mkuu pia alitumia nafasi hiyo
kuwatoa hofu watumishi hao na kuwahakikishia kuwa mambo yanakwenda vizuri na
kuwataka wajiandae kuhama kwa awamu.
"Napenda kuwatoa hofu, mambo
yanakwenda vizuri ila mtambue kuwa safari imeiva, kikubwa ni kwamba tutakwenda
kwa awamu kama ilivyopangwa,” alisema Waziri Mkuu.
Majaliwa aliwataka watumishi hao
kuzingatia uamuzi wa Serikali akisema: "Pia tukumbuke kauli ya Rais kwenye
hotuba yake ya Julai 23, alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa CCM, akairudia Julai
25, kwenye maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mashujaa na mimi siku hiyo hiyo
nikaweka msisitizo."
Kupitia taarifa hiyo, pia aliwataka
watumishi hao wazidishe mshikamano miongoni mwao huku wakitambua kuwa wana dhamana
ya kutumikia Watanzania kwa uadilifu na uaminifu.
"Watumishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu
tunapaswa tutambue dhamana tuliyonayo.
0 comments:
Post a Comment