Aidha, wamesema wako kwenye mchakato wa
kuandaa kikao cha dharura baina ya viongozi wa pande hizo mbili, ili kutafuta
mwafaka wa kudumu kuhusu mvutano huo unaoweza kuhatarisha amani.
Katibu Mkuu wa Taasisi ya Maridhiano
Tanzania, inayounda umoja wa madhehebu ya dini za kikristo na kiislamu,
Mchungaji Osward Mlay alitoa tamko hilo Dar es Salaam jana kwenye mkutano na
wanahabari.
Alisema wanakusudia kusuluhisha pande
hizo ili kuondoa hali iliyopo bila nchi kuingia kwenye mvutano na msuguano
usiokuwa na maslahi kwa Taifa.
“Tunaomba viongozi wa kisiasa na Serikali
watambue sisi viongozi wa dini na taasisi ya maridhiano Tanzania tunatambua
kwamba nchi yetu ni ya uongozi wa kidemokrasia na utawala wa kisheria,” alisema
Mlay na kuongeza:
“Hivyo, tunaomba ninyi viongozi wetu wa
kisiasa na Serikali muheshimu Katiba na sheria tulizojiwekea kama Taifa kuhusu
muundo wa uongozi tunaotaka uongoze nchi yetu,” alisema.
Alihadharisha kwamba iwapo Chadema
itafanya maandamano waliyopanga yanaweza kusababisha madhara kama yaliyotokea
siku za karibuni Ethiopia ambako wapinzani waliingia mitaani kudai haki ya
demokrasia kwa maandamano na kupambana na Dola, ambapo watu wengi waliuawa na
wengine kujeruhiwa hivyo kubaki na msiba wa kitaifa.
Alionya kuwa iwapo Serikali itafanya
ukandamizaji na kuminya demokrasia kama ilivyotokea Burundi kwa kutumia ubabe
na mabavu ya Dola, inaweza kusababisha nchi kuingia katika machafuko na
umwagaji damu za watu wasio na hatia.
Mchungaji Mlay alisema inapotokea
mivutano ya namna hiyo kwenye Taifa, waathirika huwa si viongozi bali wananchi
wa kawaida hasa wanawake, watoto na wazee ambao hukosa walezi ambao hupoteza
maisha kwenye maandamano hayo.
“Inapotokea mivutano ya namna hii
husababisha vifo, ulemavu, wajane, yatima na wazee kukosa walezi,” alitanabaisha.
Alisema viongozi wanapaswa kutambua
dhamana kubwa waliyonayo kwa wananchi wanaoongoza na kutaka wawe makini
wanapotoa matamko na misimamo inayosababisha kutoelewana baina yao na wananchi
wa kawaida.
“Mwito wa viongozi wa dini kwa
wananchi, tuilinde amani yetu tuliyoipata tangu uhuru, wananchi wa Tanzania
hatuhitaji Kamati ya Umoja wa Mataifa ije kusimamia Amani tuliyonayo, sisi
wenyewe tuna wajibu wa kuilinda,” alisema.
Mchungaji Mlay alibainisha kwamba
jukumu walilonalo Watanzania sasa ni kusonga mbele kwa kuhakikisha wanafanya
kazi za kuchochea elimu bora, kazi za kijamii, kisiasa, kiuchumi na afya,
pamoja na kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji, mauaji ya albino na
vikongwe, kuzuia vijana kujiingiza katika vitendo vya ukahaba na uasherati.
Pamoja na Mchungaji Mlay, mwakilishi wa
Kanisa la Assemblies of God (TAG), wengine waliokuwa kwenye mkutano huo ni
Shekhe Salim Juma, Shekhe Bakari Mkomeni, Askofu Msaidizi wa Kanisa la
Evangelical Assemblies of God Tanzania (EAGT) na Naibu Katibu wa Taasisi ya Maridhiano
na Padri Meshack Chidundwa wa Kanisa la Anglikana.
Katika siku za karibuni, kumekuwapo na
mvutano kati ya Serikali kupitia Jeshi la Polisi na Chadema kuhusu kuwepo au
kutokuwepo kwa mikutano ya hadhara ya kisiasa na maandamano.
Wakati Serikali ikizuia mikutano na
maandamano, Chadema inadai ni haki yao kikatiba na kwa mujibu wa Sheria ya
Vyama vya Siasa kufanya mikutano na maandamano nchi nzima Septemba mosi,
kupinga wanachodai ni kuminywa kwa demokrasia kunakofanywa na Serikali.
0 comments:
Post a Comment