Suleiman Msuya
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim
Lipumba, amesimamishwa uanachama wa chama hicho huku Naibu Katibu Mkuu wa chama
hicho(Bara), Magdalena Sakaya akivuliwa nyadhifa zake zote na kusimamishwa
uanachama.
CUF pia imemsimamisha uanachama Mbunge wa Mtwara Mjini, Maftah Nachuma
hatua ambayo inaweka rehani ubunge wake na Sakaya ambaye pia ni mbunge wa
Kaliua mkoani Tabora.
Aidha, CUF imemfukuza uanachama Katibu wake wa Baraza la Wazee, Shashi
Lugeye huku pia ikiwasimamisha uanachama, Thomas Malima na Naibu Mkurugenzi wa
Habari na Mawasiliano, Abduli Kambaya.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili wakati linakwenda mitamboni kutoka
ndani ya kikao cha Baraza Kuu la CUF mjini Zanzibar, zinaeleza kwamba uamuzi wa
kumfukuza Shashi umefuatia kupewa nafasi ya kujieleza, huku Lipumba, Sakaya na
wengine wakishindwa kuhudhuria mkutano huo.
Taarifa zinasema Baraza Kuu limewaadhibu wanachama 15, ambapo nafasi ya
Sakaya sasa itakaimiwa na Joram Nachingwa, huku ile ya Kambaya ikikaimiwa na
Mbarak Maharagande.
Kwa mujibu wa Katiba ya CUF, wanachama hao waliosimamishwa na kufukuzwa
hawana nafasi nyingine ya kukata rufaa.
Wiki iliyopita baada ya Mkutano Mkuu Maalum wa CUF uliovunjika jijini
Dar es Salaam, Jambo Leo lilimnukuu Sakaya ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la
Kaliua, akisema yupo tayari kwa uamuzi wowote utakaochukuliwa kuhusu yeye kwani
anaamini kwamba anasimamia Katiba na si
maslahi binafsi.
Aliyasema hayo alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa taarifa kuwa Baraza Kuu la
CUF, linatarajia kukutana wakati wowote ili kumjadili Profesa Ibrahim Lipumba
na baadhi ya wanachama akiwemo yeye.
0 comments:
Post a Comment