Mwandishi Wetu
KASI ya Rais John Magufuli kuhakikisha Tanzania
inajitegemea kwa kila mtu kulipa kodi, imeanza kulipa baada ya takwimu kuonesha,
kwamba watalii wameongezeka na hivyo kuongeza mapato serikalini.
Ukweli huo ulitolewa jana Dar es Salaam na Waziri
wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alipokuwa akizungumzia
mikakati iliyotekelezwa na Wizara yake.
“Pamoja na kelele za sekta ya utalii baada ya
Serikali kuanza kutoza Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) nakuhakikishia hivi
sasa watalii wameongezeka na mapato yamekua kwa asilimia 22 zaidi,” alisema
Waziri Maghembe.
Alitanabahisha kuwa tofauti na mtazamo wa wadau wa
sekta ya utalii, ongezeko la kodi hiyo halijaathiri watalii wengi hasa
ikizingatiwa kuwa Tanzania inabaki kuwa na vivutio vya kipekee duniani.
“Nchi yetu ina vivutio vingi ambavyo havipo nchi
nyingine. Hii ikijumlishwa na amani na utulivu nchini, hakuna mtalii
atakayeshindwa kugharimia ongezeko la dola nane,” alisema Waziri.
Alitumia muda huo kueleza kuwa utafiti wake katika
nchi za nje unaonesha balozi za Tanzania zinaongoza kwa kutoa viza kwa watalii
ikilinganishwa na nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hasa katika miji mikubwa
kama ya Berlin, Ujerumani.
Akizungumzia vita dhidi ya ujangili, Waziri
Maghembe alisema juhudi za Serikali kuwekeza kwenye mafunzo na vifaa vya kisasa
zimezaa matunda pia baada ya ujangili kupungua nchini kwa kiasi kikubwa.
Alisema tayari watuhumiwa wakubwa wa mtandao wa
ujangili wamekamatwa na baadhi wamehukumiwa vifungo jela.
Alimtaja mmoja wa watuhumiwa wakubwa wa mtandao huo
kuwa ni raia wa kigeni ajulikanaye kwa jina la ‘Malkia wa Pembe za Ndovu’ ambaye
naye yuko mahabusu kwa sasa.
“Katika vita hii tumeamua kuuchukulia ujangili kama
ugaidi au uhujumu uchumi. Tumekamata majangili wakubwa na wafadhili wao na bado
vigogo zaidi tunaendelea kuwafuatilia na muda wowote tutawakamata,” alisema.
Aliongeza kuwa Serikali pia imepiga marufuku
uvunaji wa mazao ya misitu hasa magogo bila leseni na atakayefanya hivyo
atakamatwa, mali na gari husika vitataifishwa na wahusika kufikishwa
mahakamani.
Takwimu za kuongezeka watalii nchini zinaipa nguvu
Serikali ya Rais Magufuli kwa sababu tangu alipoingia amekuwa akisisitiza
umuhimu wa kukusanya kodi ili nchi ijitegemee.
Tofauti na mtazamo huo, baadhi ya watu wamekuwa
hawaamini kama hilo linawezekana.
0 comments:
Post a Comment