WASOMI na wanasiasa wameeleza siri ya Rais John Magufuli kukutana na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, huku baadhi wakibainisha kuwa kitendo hicho kinaweza kufungua njia ya mwafaka kati ya Serikali na chama hicho cha upinzani kilichotangaza kufanya maandamano yaliyopewa jina la Ukuta.
Lowassa alikutana na Rais
Magufuli juzi katika hafla ya Jubilei ya
ya miaka 50 ya ndoa ya Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa na
mkewe Anna, iliyofanyika katika Kanisa la Mtakatifu Peter jijini Dar es Salaam.
Wawili hao walipeana
mikono kwa mara ya kwanza tangu kampeni na kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu mwaka
jana, jambo ambalo Magufuli alilitafsiri kama muujiza akieleza hawakuwahi
kukutana wa kampeni ambazo alikiri zilikuwa na ushindani mkali.
Magufuli alipewa nafasi ya
kuzungumza katika hafla hiyo ambapo alisema: "Nimepata muujiza wa tofauti
leo kwasababu nimeshikana mkono na Mheshimiwa Lowassa,tumezunguka kampeni zote
sikuwahi kukutana naye,miujiza ya ndoa yenu imekuwa ni miujiza pia kwetu
wanasiasa ambao nikiri kweli tulikuwa na ushindani mkali."
Aliongeza kuwa Mkapa na
Mkewe ni madhebu tofauti, Katoliki na
Lutheran, lakini wameishi miaka 50 na kwamba ana uhakika wataishi miaka
yote iliyobaki .
Tukio la hilo la Dk
Magufuli na Lowassa limezua hisia tofauti miongoni mwa wachambuzi wa kisiasa na
wasomi huku likitafsiriwa kama njia ya kupata suluhu kwa mvutano kuhusu
kufanyika au kutofanyika kwa maandamano ya Umoja wa Kupinga Udikteta (Ukuta)
operesheni iliyoasisiwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo.
Chadema imepanga kufanya
maandamano na mikutano na maandamano yasiyo na kikomo Septemba mosi, huku
Serikali ikisisitiza kutofanyika kwa maandamano na mikutano ya hadhara nchi
nzima.
Hata hivyo, wachambuzi wa
masuala ya kisiasa na wasomi waliozungumza na JAMBO LEO walitaka tukio hilo
lisaidie kuwakutanisha Chadema na Rais Magufuli katika meza ya mazungumzo
kumaliza mvutano uliopo.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam, Profesa Kitila Mkumbo alisema ingawa anatofautisha tukio la
Ukuta na kukutana kwa Dk. Magufuli na Lowassa, lakini linaweza kutumika kama
njia kuzikutanisha pande hizo katika meza ya mazungumzo kwani viongozi hao
wameonyesha ukomavu.
"Rais Magufuli na
Lowassa wameonyesha ukomavu wa kisiasa na utanzania wao bila kujali itikadi za
vyama, wameonyesgha kuwa pamoja na tofauti zao wanaweza
kukaa, kula, kusalimiana
pamoja," alisema Profesa Mkumbo.
Alisema kukutana kwao ni
mwanya wa mazungumzo, ingawa Lowassa si kiongozi wa juu wa Chadema bali ni mtu
anayekubalika na watu wengi katika jamii ndani na nje ya chama chake hivyo
anaweza kusaidia kupata muafaka wa Ukuta katika meza ya mazungumzo.
"Waliochokifanya
Magufuli na Lowassa ndio utanzania ambao sisi tunao, Lowassa ni mtu
anayekubalika watu wengi wanalitambua hilo hivyo kukutana kwake na Magufuli
jana (juzi) kutafungua njia ya mazungumzo ambayo inaweza kuridhiwa na wafuasi
wa Chadema na hatimaye Ukuta usifanyike,"alisema Profesa Mkumbo.
Alisema alichokifanya
Lowassa ‘kimemvua nguo’ Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (Cuf), Maalim Seif
Sharif Hamad, ambaye hivi karibuni alikataa kumpa mkono hasimu wake kisiasa
Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein walipokutana kwenye msiba wa Rais
Mstaafu wa Awamu wa Pili Zanzibar, Aboud Jumbe Mwinyi.
Kwa upande wake Mhandiri
wa Chuo cha Mzumbe, Profesa George Shumbusho alisema alikuwa miongoni mwa watu
waliokuwa wanahofia siku hiyo ya Ukuta kwa jinsi hali ilivyokuwa,alitamani
Magufuli awaite Chadema wazungumze ili suala hilo lisitokee.
"Sijawahi kutishwa na
masuala ya kisiasa, lakini hili la Ukuta nilihofia. Nilikuwa namwomba Mungu
Rais Magufili aone haja ya kuzungumza na Chadema ili suala hili lipate suluhu,
ndicho kilichotokea kukutana kwao jana (juzi), kumenipa moyo kwamba mambo haya
yatakwisha," alisema Shumbusho
Alisema kutokana na
kukutana kwa wawili hao, haoni kama maandamano ya Ukuta yatatokea, bali
viongozi watakaa meza moja na kuzungumza.
"Kukutana na wawili
hawa na hotuba ya Rais Magufuli kumetoa mwanga tayari kwamba Ukuta hautakuwepo,
haijalishi kama watakutana kwa siri au kwa uwazi, tunachoshukuru ni kwamba kile tulichokuwa
tunakiona ni kama kimetulia ghafla, jambo ambalo ni la kushukuru," alisema
Profesa Shumbusho.
Naye Dk Benson Bana wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alisema viongozi hao wameonyesha ukomavu wa
kisiasa na wamewatoa hofu wananchi kuhusu hali ilivyokuwa ikiendelea nchini na
wameona viongozi wao wanaweza kukaa pamoja na kuzungumza hata kama wana itikadi
tofauti.
"Nasaha inaonyesha
kuwa Ukuta mwisho wake ilikuwa jana (juzi) siasa sio uadui, nafasi waliyopata
wanaweza kuitumia kuzungumza na kuachana na Ukuta ili kazi ziendelee kutokana
na kuwa Magufuli anakubalika maeneo mengi ya nchi kwa kazi alizofanya, nipo
mikoani wananchi wanamuunga mkono kuliko hiyo operesheni,'' alisema.
Alieleza kuwa kitendo
alichokifanya Lowassa kinamfunza Maalim Seif na kumkumbusha kwamba hakufanya
sahihi alipokataa kusalimiana na Dk Shein kwani siasa sio uadui,kuna mambo
mengine watu wanaweza kufanya pamoja hata kama ni vyama tofauti.
Kwa upande
wa Profesa Joseph Semboja alieleza kufurahishwa na viongozi hao
akisema kimeuonyesha ulimwengu kwamba Watanzania ni watu wenye amani
na upendo.
“Hatua hiyo imeonyesha
Watanzania wanaweza kuwa na tofauti zao kiitikadi, lakini wakaendelea kuishi
pamoja na kushirikiana kwa maendeleo yao katika mambo mbalimbali ya kijamii,”
alisema Profesa Semboja.
Kwa mujibu wa msomi huyo,
Lowassa na Rais Magufuli wameonyesha ni
lazima wakae pamoja kwa ajili kushughulikia mambo muhimu ya maendeleo ya
wananchi, badala kuendeleza tofauti zisizo na manufaa kwa Watanzania.
“Ipo haja ya kwenda zaidi
ya hapo, waweke utaratibu kwa mustakabali wa taifa wakae pamoja na kujadiliana
kuondoa migogoro kwa afya ya Taifa,” alisema.
Profesa alisema sio sahihi
kutumia mfumo wa jino kwa jino kwani utaratibu huo ndio unaoweza kusababisha
kukua zaidi kwa migogoro na wakati mwingine unasababisha umaskini kwa wananchi
na Taifa kwa ujumla kwani muda mwingi wananchi hawana muda wa kushiriki katika
shughuli za maendeleo kwa sababu ya migogoro.
Kwa upande wake, Profesa
Samwel Wangwe alisema hatua ya viongozi hao kukutana na kupeana mikono ni
ishara kwamba Watanzania wajifunze kuwa mazungumzo yana nafasi kubwa katika
kuleta muafaka mgogoro wowote kuliko kutunishiana misuli.
Alisema kuwa mazungumzo
yana nguvu kubwa katika kultea upatanishi katika migogoro mbalimbali inatokea
katika jamii kuliko kutumia njia nyingine ambazo zinaweza kusababisha vurugu na
uharibifu wa mali za watu na upotevu wa maisha ya watu.
Msemaji wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka, alisema ni jambo jema kwa viongozi
kukaa pamoja kwa sababu giyo mambo mengine yanaweza kwenda mbele.
“Wote wanajenga nyumba
moja, Rais Magufuli na Lowassa wameonyesha ukomavu wa kisiasa na mambo mengine
yanaweza kwenda mbele,” alisema Sendeka.
Alisema anaamini sasa
Lowassa ameshaelewa kwamba anapogombania nafasi moja ni lazima mmoja apate na
mwingine akose hivyo kukutana kwao na kupeana mkono ni ishara nzuri na busara
zinazopaswa kuigwa.
0 comments:
Post a Comment