SERIKALI
imeanza kuchunguza akaunti za watumishi wake kubaini miamala isiyo ya kawaida
kwenye akaunti hizo kwa lengo la kudhibiti fedha haramu zinazoweza kuingia au
kupita.
Uchunguzi wa Jambo Leo kwa takriban
wiki mbili, umebaini Serikali ‘kudukua’
akaunti hizo kwa watumishi wake wote kwenye wizara, taasisi na halmashauri zote
nchini ili kubaini miamala hiyo.
“Sikia, sisi watumishi hali inazidi
kuwa ngumu, Serikali sasa imeanza hata kuchunguza akaunti za watumishi wake,”
alisema mtoa habari wetu kutoka moja ya wizara nyeti serikalini. Alipoulizwa
lengo la kufanya hivyo, alisema: “Serikali inataka kudhibiti mapato yasiyo
halali kwa watumishi wa umma.”
Uchunguzi umebaini kuwa Serikali
inalenga kugundua watumishi ambao akaunti zao zina fedha nyingi kuliko kipato
chao cha kawaida au zinapitisha fedha kutoka au kwenda akaunti zinazotiliwa
shaka, hasa kuhusu ufisadi, pia mishahara hewa.
Hata hivyo, taarifa zinaonesha kuwa
sheria za kibenki haziruhusu mtu asiye mwenye akaunti husika kuchunguza akaunti
ya mtu bila idhini kwani ni kosa kisheria.
Kwa mujibu wa Mwanasheria, Aloyce
Komba, taarifa za akaunti ya mtu ni siri kati yake na benki husika.
"Haki hiyo itageuzwa kwa amri ya
Mahakama, au akaunti itachunguzwa kwa amri ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) ambayo sasa imepewa mamlaka ya kufanya hivyo," alisema.
Aliongeza: "Pia hilo linaweza
kufanyika kwa ruhusa ya Meneja wa Benki husika, lazima uchunguzi huo uendane na
sharia au mamlaka, kama nilivyosema. Kamishna wa Maadili anaweza kuagiza hilo
iwapo atabaini viongozi waliowasilisha hati za kiapo cha maadili na mali
zinatia shaka, vinginevyo itakuwa ni kosa."
Alisema uchunguzi wa akaunti binafsi ya
mtumishi hufanyika kwa kutumia pia Sheria ya Udhibiti wa Fedha Haramu. Hata
hivyo, chanzo cha habari kilieleza kuwa mbali na hatua hiyo, Serikali pia
imepiga marufuku watumishi wake kupokea zawadi au fedha kama shukrani kutoka
kwa watu wanaohudumia.
Kwa mujibu wa uchunguzi huo, mfanyakazi
atakayebainika kupokea fedha au zawadi kutoka kwa mtu au taasisi aliyoihudumia na
kubainika, atachukuliwa hatua za kinidhamu.
Habari zinapasha kuwa kwa hatua hiyo,
watumishi wa Serikali wanatakiwa kuweka wazi kwa kutoa taarifa kwa wakuu wao wa
idara iwapo watapewa fedha au zawadi kutokana na kazi wanazofanya.
"Tumeambiwa ni marufuku kupokea
zawadi yoyote hata fedha, tukitaka kufanya hivyo tutoe taarifa kwa wakubwa na
kueleza tumepewa nini au kiasi gani," alisema mmoja wa watumishi katika
Wizara ya Ardhi.
Mtumishi mwingine alisema: "Si
kuzuiwa kupokea zawadi tu na fedha tu, Serikali ya Awamu ya Tano imetusainisha
wote hati za kiapo cha maadili, kina mambo mengi pamoja na hayo."
Mwandishi wa gazeti hili alimtafuta
Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dk Servacius Likwelile kuzungumzia
suala hilo Jumapili iliyopita, lakini akasema hayupo tayari kuzungumza kwa
sababu yuko nyumbani amepumzika na kumtaka mwandishi amtafute ofisini siku
inayofuata.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Fedha na Mipango, Dk. Servacius Likwelile alikanusha kuwepo kwa uhakiki huo
akisema: “Serikali haina mpango wa kufanya uhakiki wa miamala ya fedha kwenye
akaunti za watumishi wa umma na idara zake nchini."
Akizungumza na Jambo Leo jijini Dar es
Salaam jana, Dk Likwelile alisisitiza: ìHakuna uhakiki unaofanywa na Serikali
kimya kimya, kama utakuwapo vyombo vya habari vitajulishwa ili Watanzania
wafahamu."
Hata hivyo, habari za uhakika kutoka
ndani ya Serikali zinaeleza kwamba miamala ya fedha kwenye akaunti za watumishi
wa umma na idara zake inahakikiwa. "Unafanyika kupitia manispaa na
halmashauri zote nchini.
Lengo la uhakiki huo ni zuri. Ni
kuhakikisha mishahara inamfikia mlengwa na kuepuka kulipa watumishi hewa kama
ilivyokuwa awali ambapo mtu mmoja alimiliki akaunti zaidi ya moja,"
alisema mmoja wa watendaji wa Wizara ya Utumishi aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa
kuwa si msemaji.
Hata hivyo, alisema kinachosubiriwa ni
mrejesho kamili kutoka kwa wakurugenzi wa Halmashauri na Manispaa na kwamba
taarifa husika zitatumwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya hatua zaidi za
kiserikali.
"Kazi inafanyika, lakini bado
mrejesho wa utekelezaji kutoka kwa wakurugenzi wa manispaa na halmashauri
haujawasilishwa Serikali Kuu kwa maana ya Wizara ya Fedha na Mipango, naamini
hilo linasubiriwa na wahusika." alieleza mtendaji huyo.
0 comments:
Post a Comment