Leonce Zimbandu
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Nape Nnauye amevifunga kwa muda vituo vya Radio 5 cha Arusha na Magic
FM cha Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Waziri Nape, hatua hiyo
imefikiwa baada ya kujiridhisha kuwa
kipindi cha Matukio kilichorushwa Agosti 25,
saa 2 usiku na Radio 5 na cha Kupaka Rangi kilichorushwa Agosti 17, na
Magic FM vilikuwa na maudhui ya uchochezi.
Alisema hayo alipozungumza na waandishi
wa habari Dar es Salaam jana kwa kusisitiza
vipindi hivyo kuwa na maudhui ya uchochezi ambao ungeweza kusababisha uvunjifu
wa amani.
Alisema vitendo vilivyofanywa na vituo
hivyo vinakiuka kanuni ya 5 (a),(b),(c) na d, pia kanuni ya 6(2), (b),(c) na
18 (1), b(i),(ii) na (iii) ya huduma za utangazaji
na maudhui ya mwaka 2005.
“Kwa mamlaka niliyopewa chini ya kifungu
cha 28 (1) cha sheria ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ya mwaka 2003
ninavifunga vituo hivyo hadi Kamati ya Maudhui itakapoviita vyombo hivyo
kuvisikiliza,” alisema.
Alisema baada ya Kamati kusikiliza
vyombo hivyo, itatoa mapendekezo ya kumshauri Waziri hatua zinazopaswa kuchukuliwa,
lakini kwa sasa hatua iliyochukuliwa itakuwa ya muda.
Aidha, Waziri Nape alipongeza vyombo vingine
vya habari vilivyojikita kutekeleza wajibu wao wa sheria, kanuni na kufuata
weledi wa tasnia ya habari katika kuleta amani, umoja, mshikamano na maendeleo
ya nchi.
Alisema Serikali inaendelea kuvihadharisha
vyombo vya habari kutoshawishika kuvunja sheria na kanuni zinazoongoza tasnia
ya habari ili kulinda heshima ya tasnia na amani ya nchi.
Vyombo hivi vimefungwa huku gazeti la
Mawio nalo likiwa kifungoni kwa tuhuma za uchochezi.
0 comments:
Post a Comment