Na Peter Kimath, Morogoro
ZAIDI ya sh. bilioni 1
zimetolewa na Manispaa ya Morogoro kwa ajili ya kunusuru kaya maskini 4,039.
Hayo yalisemwa na Meya wa Manispaa ya Morogoro, Paschal Kihanga na
kubainisha kuwa fedha hizo zilitolewa katika kipindi cha Julai 2015 hadi Juni
mwaka huu.
Akizungumza katika wa kikao cha kawaida cha baraza la madiwani wa
manispaa hiyo, alisema kiasi hicho kilitolewa katika kaya hizo baada ya kukidhi
vigezo.
Kihanga alisema katika kutekeleza maagizo ya Serikali ya fedha
zinazotolewa kwa ajili ya kusaidia kaya maskini zisilipwe kwa kaya ambazo si
maskini hivyo kaya 157 zilihakikiwa na kuondolewa katika mpango huo.
Hata hivyo, alisema bado kuna kaya ambazo zina vigezo vya kaya
maskini ambazo zimetambuliwa na kuandikishwa na manispaa imepeleka maombi ya
kufanya mchakato wa utambuzi wa nyongeza ili waweze kuingizwa katika mpango
huo.
Meya alisema Manispaa ya Morogoro ni miongoni mwa halmashauri 161
zinazotekeleza Mpango wa TASAF awamu ya tatu kupitia mpango wa kunusuru kaya
maskini wenye malengo ya kuziwezesha kuongeza kipato.
Kwa upande mwingine, meya huyo alisema manispaa hiyo ilitoa mikopo
kwa vikundi vya wanawake na vijana yenye jumla ya sh. milioni 100.
Alisema kwa vikundi vya wanawake 50 vilipatiwa mkopo wa sh.
milioni 50 na vikundi 28 vya vijana vilipatiwa sh. milioni 50.
0 comments:
Post a Comment