* Asema JPM asiachwe aingie
vitani na wapinzani, Lowassa msingi wa maandamo
Suleiman Msuya na Mashaka
Mgeta
KADA mwandamizi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Steven Wasira amesema wasaidizi wa Rais John Magufuli,
hawapaswi kumuacha kiongozi huyo aingie vitani dhidi ya wapinzani waliotangaza
kufanya maandamano na mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi mwaka huu.
Wasira ambaye pia aliwahi
kuwa mwanachama wa Chama cha NCCR-Mageuzi pamoja na kushika nafasi mbalimbali
za uwaziri tangu Serikali ya awamu wa kwanza na ubunge wa Bunda kwa vipindi
tofauti, alisema ipo haja ya kuwapo mazungumzo kati ya pande mbili zinazohusika
ili kufikia muafaka na kwamba nafasi hiyo ipo.
“Kinachohitajika ni
wasaidizi wa Rais kumshauri ili kuhakikisha kuwa tofauti zilizopo baina yake na
vyama vya upinzani haziendelei ili kuepusha madhara yanayoweza kuzuilika,
itafutwe suluhu,” alisema Wasira.
Aliongeza: “Wazungumze,
wasimuingize Rais kupigana na watu wake kwa maana wote tutapoteza. Kwa nini
uweke askari polisi wote hao, msimweke Rais kwenye vita.”
Maandamano hayo
yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kupewa jina la
Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania (Ukuta), yameibua taharuki kwa umma na
malumbano kati ya Chadema na watawala.
Viongozi wa serikali akiwamo
Rais Magufuli na makamanda wa jeshi la polisi, wamekaririwa mara kadhaa
wakionya kuwashughulikia washiriki wa maandano na mikutano hiyo, huku Chadema
ikijinadi kuwa maandalizi yao yanakwenda vizuri.
Kauli hiyo ya Wasira
imekuja wakati juzi na jana mitandao ya kijamii na vyombo kadhaa vya habari,
vilichapisha picha za askari wenye sare, wengine wakiwa na silaha wakifanya
doria barabarani kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mazoezi ya kukabiliana na
uhalifu na wahalifu.
Alisema ni wakati mwafaka
kwa Bunge kupitia Spika Job Ndugai, kuwakutanisha wapinzani, serikali na kutoa
ushauri unaofaa kwa rais Magufuli ili kuepusha hali hiyo kwani hakuna sababu ya
nchi kuingia katika malumbano yasiyokuwa na tija.
Kwa mujibu wa Wasira,
Bunge ni chombo kinachovikutanisha vyama vyenye wabunge hivyo kuwa sehemu
muafaka kwa mazungumzo yenye lengo la kuleta muafaka huku yakisimamiwa na
Ndugai aliyeonesha kutoridhishwa na hali ilivyo sasa.
“Nadhani wangelitumia
Bunge kutoa kero zao ili kuhakikisha Serikali inazifanyia kazi, hivyo kuepuka
kasumba ya kutoka bungeni,” alisema.
Alisema kitendo cha
upinzani kujiandaa kufanya mikutano na maandamano inaweza kuibua mambo ambayo hayakutarajiwa hivyo
Serikali inapaswa kuangalia kabla ya kuruhusu.
TATIZO NI LOWASSA
Wasira alisema msingi wa
kuzuiwa mikutano na maandano ya wapinzani inawezekana ikawa ni kumzuia
aliyekuwa mgombea urais mwaka 2015 kupitia Chadema, Edward Lowassa, asifanye
ziara ya nchi kuwashukuru waliompigia kura.
"Wakati wa uchaguzi
nchi inachemka kwa harakati ambazo zinafanyika hivyo ukiruhusu mikutano kwa
muda mchache baada ya uchaguzi unaweza kurejesha hali ambayo inaweza kuongeza
migongano," alisema.
Alisema azma hiyo ya
upinzani ingeweza kurejesha hisia za umma kwenye uchaguzi uliopita hivyo kuathiri
mipango ya Rais Magufuli katika kuwatumikia wananchi kupitia kauli mbiu ya
‘Hapa kazi tu’.
Alisema baada ya uchaguzi
kumalizika, Lowassa, alitangaza kushinda kwa asilimia 62, hivyo akiachwa kutoa
shukrani nchi nzima, anaweza kusababisha migongano, hivyo si vema kuruhusu
mikutano kwa sasa.
“Hebu fikiria kama
wananchi watatangaziwa kuwa Lowassa atakuwa katika maeneo yao, kuna uwezekano
wa shughuli kusimama kwani ni mtu ambaye alifanikiwa kupata kura nyingi katika
historia ya uchaguzi hapa nchini,” alisema.
Aliongeza, “ukiwaruhusu
kufanya mikutano na ukawaambia kuwa atakayekuja kutoa shukurani ni Lowassa,
ambaye amekuwa akipinga kushindwa ni sawa na kurejesha hali ya uchaguzi kipindi
hiki.”
Wasira aliwataka viongozi wa serikali
wasiishie kutoa matamko ya kupiga marufuku maandamano na mikutano ya Chadema,
bali waelezee sababu ili kutoa elimu pana kwa jamii.
“Kama mimi hapa nimetaja
sababu kwamba inaweza kuwa ni Lowassa, sasa na wao (serikali) wasiseme tu
tunapiga marufuku mikutano na maandamo, wataje na kuzifafanua sababu za kufanya
hivyo ili kuepusha upotoshaji,” alisema.
AWASAA CHADEMA
Hata hivyo Wasira alisema
demokrasia na uhuru ni mambo mazuri lakini yana mipaka hata kama yatatokana na
Katiba ya nchi.
Kwa hali hiyo, aliiasa
Chadema kuondokana na siasa za maandamano na mikutano baada ya Uchaguzi Mkuu,
kama ilivyo kwa mataifa makubwa kama Marekani, Uingereza na Ujerumani.
“Hakuna demokrasia na
uhuru isiyo na mipaka, nataka nikuambie ukweli katika dunia yote uhuru wa
mikutano na maandamano umeandikwa katika Katiba zao ila lazima kufuata
taratibu," alisema.
Wasira alisema kumbukumbu
zake ni kwamba Chadema imekuwa ikifanya mikutano kila baada ya uchaguzi jambo
ambalo linaonekana kuwa ni mkakati wa kukwamisha Serikali isifanye kazi zake
ipasavyo.
Wasira alisema mitizamo na
utashi wa kuongoza nchi vinatofautiana kati ya viongozi, hivyo akawataka
Chadema wasitarajie mfumo wa uongozi wa Rais Magufuli uwe sawa na Rais msraafu
Jakaya Kikwete.
0 comments:
Post a Comment