NA EMERCIANA ATHANA
HOJA ya kutaka aliyekuwa
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi(CUF) Profesa Ibrahim Lipumba aliyejiuzulu
arudi kwenye nafasi yake, jana ilisababisha mpasuko kwa Mkutano Mkuu Maalum wa
chama hicho ambapo ulivunjika bila kupata uongozi mpya.
Chama hicho kilikutana
jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kujadili na kupitisha majina ya wagombea
uenyekiti na makamu mwenyekiti wake kufuatia kujiuzulu kwa Lipimba wakati wa
kampeni za uchaguzi mkuu mwaka jana na makamu wake Juma Haji Duni aliyekwenda
kuwa mgombea mwenza wa Edward Lowassa wa Chadema katika nafasi ya urais.
Awali, chama hicho
kilitangaza majina ya waliopitishwa kugombea uenyekiti na umakamu huku Duni
akitangaza kujitoa kwa kilichoelezwa kukosa sifa kuwania nafasi hiyo kikatiba.
Mkurugenzi wa Uchaguzi na
Mipango wa CUF, Shaweji Mketo, alisema Duni alijiondoa kutokana na baadhi ya
maadui wa Ukawa kutaka kukihujumu chama hicho.
"Katiba ya chama
inasema kama kiongozi alijiuzulu na kuhamia chama kingine, basi itamlazimu
kukaa ndani ya miaka miwili kisha kuwania tena nafasi hiyo,” alisema.
Alitaja majina ya wagombea
hao akisema uteuzi wao ulifanyika juzi katika mkutano mkuu wa dharura wa chama
hicho uliofanyika jijini Dar es Salaam.
Mketo, aliwataja wanachama
watakaowania nafasi ya Mwenyekiti kuwa ni Riziki Mngwali, Twaha Taslima na Juma
Nkumbi.
Kwa upande wa Makamu
Mwenyekiti, waliopitishwa kuwania ni Mussa Hajji Kombo na Salim Abdalla Bimani.
Majina yao yalifikishwa kwenye Kamati Kuu ya CUF kwa ajili ya kupigiwa kura.
Mketo alisema majina 34 ya
wanachama waliojitokeza kuwania nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la Taifa
yalipitishwa yote kwenda Kamati Kuu kwa ajili ya kupigiwa kura ili kupata
wajumbe watakaoziba nafasi zilizoachwa wazi.
Pia, Mketo alisema mkutano
huo wenye wajumbe 832 ulipokea rasmi taarifa ya kujiuzulu kwa Profesa Lipumba.
Hata hivyo, taarifa kutoka
ndani ya mkutano huo zinaeleza kuwa baada ya kujadili hoja ya Lipumba kuliibuka
mvutano kati ya wajumbe 832 waliohudhuria mkutano huo na kusababisha mkutano kusimama
kwa muda.
Habari zinasema baada ya
kurejea, walishindwa kupata mwafaka hali iliyosababisha waamue kupiga kura.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa
viongozi waliopo walitumia ubabe kulazimisha kupigwa kura ya wazi, jambo ambalo
linaloelezwa ni kinyume cha Katiba ya CUF na misingi ya demokrasia.
“Haki haikutendeka, ni
ubabe wala mkutano haukuzingatia kutimia kwa akidi. Tulilazimishwa kupiga kura
kwa kunyoosha mikono wakati kwa mazingira yaliyopo na usahihi kura ni siri,”
alisema mmoja wa wakjumbe wa mkutano huo aliyeomba kuhifadhiwa jina kwa sababu
si msemaji wa chama.
Taarifa zaidi zinaeleza
kuwa katika kura hizo Lipumba alipata kura 14 zilizotaka arejee kwenye nafasi
yake, huku wajumbe 476 wakimkataa kati ya wajumbe 832, jambo lilizozua tafrani
na mkutano kuvunjika.
Awali, nje ya ukumbi
wafuasi wa chama hicho walitanda huku wengine wakiwa wamevalia fulana zenye
picha ya Lipumba ambaye baada ya kuwasili walimshangilia na kuisikika wakisema;
‘Lipumba kwanza mengine baadaye.’
Wafuasi hao kwa nyakati
tofauti walisikika pia wakisema hawawezi kukubali kumwacha Lipumba kuondoka na
kukiacha chama hicho kife.
Habari za ndani ya kikao
hicho zinaeleza kuwa muda mfupi baada ya kuanza kujadili barua ya Lipumba,
baadhi ya wafuasi walitaka mkutano usitishwe na kumsubiri hadi atakapofika huku
wanachama wengine wakipinga ujio wa Lipumba.
Kwa mujibu wa taarifa hizo
baada ya Lipumba kuwasili alikwenda mbele kwa ajili ya kusalimiana na viongozi
waliokuwa Meza Kuu, wakiongozwa na
Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad ambao walikataa salamu
yake kwa kutompa mkono, badala yake aliamriwa kukaa kwa ajili ya kuendelea
kuijadili barua yake ya kujiuzulu.
0 comments:
Post a Comment