Mbunge Lema agoma kula mahabusu



Seif Mangwangi, Arusha

HALI ya afya ya mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema (Chadema), inaelezwa kuwa mbaya baada ya  kugoma kula kwa siku nne sasa tangu alipokamatwa na polisi jijini hapa akituhumiwa kwa uchochezi.

Akizungumza na JAMBO LEO jijini hapa jana Meya wa Jiji la Arusha, Calist Lazaro alisema licha ya kushawishiwa na viongozi wa chama hicho, viongozi wa dini  hata mke wake mbunge huyo hakubadili uamuzi wake wa kugoma kula.

Lazaro alisema Lema amegoma kula kutokana na hasira alizonazo nazo kufuatia kukamatwa akiwa ndani kwake akijiandaa kuelekea polisi baada ya kupewa agizo la kufika kituoni hapo na Mkuu wa Upelelezi Mkoa.

"Sisi kama chama tumejaribu kuzungumza na Lema kumsihi ale lakini amegoma, amekuja mke wake bado amegoma, hata viongozi wa dini wamekuja bado amekataa kula," alisema.
Alibainisha kwamba anachosisitiza Lema ni kuendelea na mgomo huo huku akifanya ibada kwa madai ya kudhalilishwa mbele ya familia yake kama mwizi.

Meya Kalist alisema kwa nafasi yake alijaribu kuwasihi polisi kumwachia mbunge huyo ajumuike na familia yake ili aweze kula na kuokoa afya yake na kuripoti kituoni hapo kulingana na maagizo atakayopewa. lakini polisi wamemkatalia.

Alisema Lema alikamatwa Alhamisi ilitiopita na kuwekwa mahabusu ya polisi huku akinyimwa haki yake kimsingi ya dhamana kwani hata kosa analotuhumiwa nalo linadhaminika kisheria.

"Kama Chadema tumewataka polisi kumfikisha mahakamani Lema kesho na kama watakaidi, asubuhi wanasheria wetu wanaoongozwa na Tundu Lissu na John Mrema wataenda mahakamani kuomba kibali cha mahakama kushinikiza polisi wamfikishe mahakamani mbunge wetu,"alisema Meya Lazaro.

Alipoulizwa kama amezungumza na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Meya Lazaro alisema kesi hiyo iko chini ya Mkuu wa upelelezi Mkoa wa Arusha hivyo Kamanda wa Mkoa hahusiki na dhamana ya Lema

Alipotafutwa kuzungumzia tukio hilo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Charles Mkumbo  alikiri mbunge huyo kugoma kula lakini akasema: “Hatuna namna ya kumshiniza ale kwani amekataa. Lakini tumemweleza anachofanya pia ni kosa kisheria, Kugoma kula ni kosa.”

Alipoulizwa kama mbunge huyo atafikishwa lini mahakamani Kamanda Mkumbo alisema: Hatuna hakika ni lini, hivyo hatuwezi kuseme kama ni kesho.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo