Suleiman
Msuya na Celina Mathew
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeelezea utayari wake kushirikiana
na vyama vyote, ikiwamo chama cha Tanzania Labour Party (TLP) kujenga nchi,
lakini hakifikirii kuanzisha makundi yasiyo rasmi na vyama vingine nchini.
Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka, alisema hayo
jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu kauli ya Mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema kuwa chama chake na
vingine vya upinzani viko tayari kuanzisha umoja na CCM.
Mrema akihojiwa kwenye kituo cha radio cha TBC Fm kwenye
kipindi cha Busati, alisema vyama vinavyopenda maendeleo na amani nchini, viko
tayari kuanzisha ‘Ukawa’ yao na CCM
Akizungumzia kauli hiyo, Sendeka alisema CCM ni chama
kilichosajiliwa na kilicho tayari kufanya kazi na chama kingine cha siasa
chenye usajili wa kudumu na usio wa kudumu.
Aliongeza kuwa kiko tayari kutoa mafunzo ya kuimarisha
uzalendo wa kujenga nchi na kwamba kama vyama vingine vitahitaji ushauri
vinakaribishwa, maana lengo ni kushirikiana na vyama vyote.
Hata hivyo, wanachama
wa TLP walimpinga Mrema kwa kauli yake ya kuungana na CCM.
Aidha,
walimtaka achague TLP au Parole kwa kinachodaiwa kuwa ameanza kulewa madaraka.
Wakizungumza
na JAMBO LEO baadhi ya wanachama hao walisema kiongozi huyo anafanya mambo
kinyume na Katiba na taratibu za chama hivyo hawako tayari kushirikiana na CCM.
Mwanachama
James Haule aliweka bayana kuwa anachofanya Mrema sasa ni kinyume na chama
hicho, kwani hajawashirikisha katika mapendekezo yake ya kujiunga na CCM.
Haule
alisema Mrema amelewa madaraka ya Parole hata achanganyikiwe, hivyo anashindwa
kuongoza chama na kufanya kazi za Parole na kujikuta akitoa matamko yasiyo shirikishi.
Aidha,
alisema Mrema anapaswa kutoa tafsiri sahihi ya yeye kutaka kuungana na CCM, kwani
anaonekana kuacha maswali mengi juu ya muungano anaotaka.
Mwanachama
huyo alisema umuhimu wa Mrema ndani ya TLP ni mkubwa hivyo kutokana na kupewa
madaraka mengine, ameonekana kuanza kukiacha chama hivyo sasa ni wakati mwafaka
kupisha watu wengine waongoze.
"Napenda
kumwambia Mwenyekiti aamue jambo moja, kufanya siasa akiwa TLP au Parole, kwani
naona ameanza kulewa madaraka ndiyo maana leo unamwona yuko kwa watumia dawa za
kulevya, kesho waendesha pikipiki," alisema.
Dickson
Rutabanzibwa wa Bukoba, Kagera, alisema hawako tayari kuungana na CCM kwa
alichodai ni lengo la chama cha Upinzani kukiondoa chama tawala madarakani.
“Atupishe,
kwanza anavunja Katiba ya chama, sisi hatuko tayari kuungana na CCM, lengo letu
ni kukamata Dola, kama yeye amechoka siasa ahamie huko atuachie chama chetu,”
alisema.
Akizungumzia
malalamiko hayo, Mrema alisema hawezi kuacha nafasi ya uenyekiti kwa sababu ya
kuwa kwenye Bodi ya Parole, kwa kuwa hakuna anachokosea na wanaosema hayo ni
wabaya wake kisiasa.
Mrema
alisema ataondoka kwenye uenyekiti wa TLP kwa kufuata taratibu zinazopaswa
kufuatwa kichama na si kwa kauli za wanaojiita wanachama.
Kuhusu
kuungana alisema hakumaanisha kuungana na kuwa chama kimoja ila ni kutekeleza
majukumu, kwani anaona CCM ya sasa inafanya mambo ambayo yeye na chama chake
wanafanya.
"CCM
ya sasa inapingana na ufisadi, rushwa na kuhitaji uwajibikaji kazini hayo ndiyo
malengo yetu ya kila siku, ndiyo maana nikasema tuungane kufanya kazi na si
kuunganisha vyama.
“Ila
mbona Rais John Magufuli ni Mwenyekiti na Rais, kipi kimeharibika nadhani
tunapaswa kuheshimu nafasi hii tuliyopewa," alisema.
0 comments:
Post a Comment