Spika wa Bunge, Job Ndugai |
Na Suleiman Msuya
SPIKA wa Bunge, Job Ndugai amesema ingawa msuguano baina ya
Serikali na wapinzani kuhusu mikutano ya hadhara na maandamano hauna tija, kuna
haja ya kufanya mazungumzo ili kupata mwafaka kuhusu jambo hilo.
Ndugai alisema hayo jana katika Kipindi cha Funguka kilichorushwa
na televisheni ya Azam Two kikiongozwa na mmoja wa waandishi wakongwe nchini,
Tido Mhando.
“Mimi nashauri mazungumzo yaendelee kama yapo, waone namna gani
tunavyoweza kujenga demokrasia yetu ya Kitanzania, lakini kwa kweli kuendelea
na kampeni zisizoisha za maandamano na mikutano ya hadhara ni kuwadanganya
wananch kwa kueleza mambo ambayo hayapo, kwa sababu kumbuka hii mikutano ni
information (taarifa) za upande mmoja tu, upande wa pili hauna fursa ya
kubalansi,” alisema Ndugai.
Mbali na msuguano huo, Ndugai pia alizungumzia mambo kadhaa,
ikiwamo sakata la Lugumi, mgogoro wa wabunge wa upinzani na uongozi wa Bunge na
Serikali kuhamia Dodoma kama inavyonukuliwa hapo chini:
Swali: Unazungumziaje taarifa za vyama vya
siasa kutaka kuandamana kwa kile wanachodai kuwa kuna uminyaji wa demokrasia?
Jibu: Hili jambo lina tatizo la utamaduni tu.
Tatizo kwa siasa za Tanzania watu wakimaliza uchaguzi wanataka kufanya mikutano
ambapo asilimia kubwa ya mikutano hiyo inatawaliwa na maneno ya kashfa na
matusi, hivyo hatuwezi kukubaliana na hali hiyo.
Kinachotakiwa ni sisi tufuate utaratibu wa Jumuia ya Madola ili
kuruhusu Serikali ifanye kazi kwani asilimia kubwa ya wanaotaka kufanya siasa
wanajukwaa la Bunge, hivyo watumie nafasi hiyo kufikisha ujumbe.
Wapo baadhi ya wabunge wanaotumia lugha chafu ndani ya Bunge kwa
kuwatukana mawaziri, hivyo watu hao wakipata uwanja wa kusema nje ya Bunge ndio
kasi inaongezeka.
Mikutano hiyo asilimia kubwa kinachosemwa hakina ukweli wowote hali
ambayo hata ndani ya Bunge inatokea ila zipo adhabu za kikanuni tofauti na huko
nje ambako hakuna kanuni.
Aidha, changamoto iliyopo ni kuwa yanayosemwa huko nje hakuna mtu
wa kujibu, hivyo jamii inaaminishwa jambo ambalo linawezekana kuwa na majibu.
Naamini mazungumzo bado yanahitajika ili kuhakikisha kuwa muafaka unafikiwa
kwani hakuna sababu ya kuendeleza malumbano ambayo hayana tija.
Swali: Ipo hoja ya Lugumi ambayo imeonekana
kuzimwa katika mazingira ya kutatanisha hasa baada ya wabunge wa upinzani
kutoka nje ya Bunge. Wewe unazungumziaje uamuzi huo?
Jibu: Ninavyojua sakata la Lugumi halijapita
bado baada ya kamati ndogo kufanya kazi kwa kupita nchi nzima na kuona kuwa vifaa
vilipelekwa na havijafanya kazi hivyo Naibu Spika aliagiza baadhi ya mapungufu
kutatuliwa. Wabunge wa upinzani ambao walitoka wametolewa kwa makosa ambayo
walifanya ila hawa wengine walikuwa wanatoka katika mgomo wao.
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), itapata nafasi ya
kutoa taarifa yake, lakini taarifa rasmi kuhusu Lugumi itawasilishwa bunge
lijalo na wapinzani wakiwapo na watapata fursa ya kuchangia kinagaubaga.
Swali: Je, unafikiria utachukua mkondo gani
ili kumaliza hali hii ya kutoelewana baina ya wapinzani na uongozi wa Bunge.
Jibu: Kusema kweli katika mambo ambayo
yananinyima usingizi ni hali hii ya kutofautiana baina yetu na wabunge, hivyo nafikiria
kuwepo na watu wazoefu na wastaafu kama spika mstaafu Anne Makinda na wenzake
waweze kutusaidia kutatua changamoto zilizopo.
Aidha, kuna dhana kuwa Naibu Spika Dk Tulia Ackson ujio wake
umekuwa na maswali mengi na hofu kwa baadhi ya wabunge kuamini kuwa atakuwa
anatetea maslahi ya upande ambao umemteua. Ni kweli kuwa hali hiyo haijawahi kutokea
hata mabunge ya Jumuia ya Madola yamekuwa yakitumia mfumo wa kuhakikisha kuwa
Naibu Spika anakuwa ni mbunge wa kuchaguliwa na si kwa mfumo wa Dk Tulia.
Sisi hatupokei maagizo kutoka popote pawe Ikulu au kwa Rais moja
kwa moja ila tunafanya kazi kwa kufuata kanuni za Bunge ambazo zinatumika kila
siku. Napenda wabunge watumie nafasi zao kuibana Serikali kupitia Bunge na
wakisema tunafanya kwa msukumo wa Serikali tunapaswa kuuliza ni mbunge yupi ameuliza
swali tukakataa kuwapa nafasi ya majibu.
Swali: Kitendo cha Bunge kutooneshwa moja kwa
moja unakizungumziaje?
Jibu: Kwa sasa ndio uamuzi ambao umefikiwa,
hivyo tunaendelea na utaratibu huo kwani tumeona faida yake tofauti na zamani
ilivyokuwa ambapo wabunge walikuwa wanatumia vibaya nafasi hiyo. Wabunge
wakijua wanaoneshwa moja kwa moja wanatumia nafasi hiyo kuleta usanii na kuwa
ni tatizo kubwa lakini tukiwa kama kamati utulivu unakuwepo.
Swali: Baada ya Serikali kutangaza kuhamia
Dodoma, Bunge nalo limeanza kupeleka vikao vyao huku kwa nini imekuwa hivyo?
Jibu: Sisi Bunge tumekuwaDodoma kwa muda
mrefu ila changamoto ilikuwa ni kufanya vikao vya kamati Dodoma kwani kamati
zilikuwa za watu wachache hivyo kuhamishia watendaji Dodoma wakati wa kamati
ilikuwa ngumu. Kwa sasa tumeamua kuanzia sasa kila kitu ni Dodoma na asilimia
99 ya watumishi wa Bunge watakuwa Dodoma kiofisi na makazi. Naamini watabakia
asilimia moja tu ambayo itakuwa inashughulikia mambo machache kama wabunge
wakitaka kusafiri, wakiumwa na baadhi ya mambo ambayo yatahitaji kutatuliwa Dar
es Salaam. Kwa mimi ambaye ninatoka Dodoma naunga mkono uamuzi wa Rais John
Magufuli, kuhamishia shughuli za Serikali Dodoma kwani ni jambo jema.
Swali: Bunge lako limekuwa na utoro wa hali ya
juu wewe umejipangaje kutatua au kuondoa hali hiyo?
Jibu: Hili la utoro ni kweli lipo ila si kwa
Tanzania pekee, nchi nyingi hali hiyo ipo mfano nilikuwepo Kenya wakati fulani
na kushuhudia uwapo wa wabunge 14 tu bungeni.
Wapo wabunge ambao wanaingia na kusaini halafu wanaingia katika
mgahawa na baabaye wanaondoka. Pia lipo tatizo la wabunge wafanyabiashara, hawa
nao hawatulii bungeni. Muda mwingi wanashughulika na biashara zao na jambo hilo
linakatisha tamaa kwani hawataekeleze majukumu yao ipasavyo.
Swali: Wabunge wamekuwa wakisema kuwa posho zinazotolewa
ni nyingi na wengine wamediriki kusema hawatachukua hili unalizungumziaje?
0 comments:
Post a Comment