Hayati Aboud Jumbe Mwinyi |
Na Suleiman Msuya
ALIYEKUWA Rais wa Pili wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na
Makamu wa Kwanza wa Rais, Aboud Jumbe Mwinyi (pichani) amefariki dunia jana
nyumbani kwake Mjimwema, jijini Dar es Salaam.
Taarifa za kifo cha Jumbe zilianza kuzagaa jana mchna kwenye
mitandao ya kijamii kabla ya kutangazwa kwenye vyombo vya habari kisha Ikulu
kutoa taarifa ikimnukuu Rais John Magufuli kutoa salamu za rambirambi kwa Rais
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein kufuatia
kifo cha Rais huyo mstaafu.
Kwa mujibu wa mtoto wa marehemu, Mustafa, Jumbe alifariki dunia saa
7 mchana jana na anatarajiwa kuzikwa leo visiwani Zanzibar.
Marehemu Jumbe alikuwa Rais wa Zanzibar, Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania kuanzia Mwaka 1972 akichukua
nafasi ya hayati Sheikh Abeid Amani Karume aliyeuawa, hadi 1984 alilazimishwa
kujiuzulu madaraka kufuatia kutokea kwa kilichoelezwa ni machafuko ya hali ya
hewa Zanzibar.
Katika salamu zake za rambirambi, Rais Magufuli alisema:
"Nimeshtushwa sana na kifo cha Mzee wetu Aboud Jumbe, kwa hakika Tanzania
imepoteza mtu muhimu ambaye katika kipindi cha uongozi wake alitoa mchango
mkubwa wa kupigania na kuijenga Tanzania tunayoiona leo."
Aliongeza: "Napenda kuwapa pole familia ya marehemu, ndugu,
jamaa na marafiki wote, wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa jumla kwa
kufikwa na msiba huo mkubwa" Rais Magufuli alisema Taifa limempoteza mtu
muhimu aliyejitoa kupigania uhuru, umoja, haki na maendeleo ya wananchi wa
Zanzibar na Tanzania kwa jumla katika kipindi kigumu ambacho Taifa lilipitia.
Aboud Jumbe Mwinyi, alizaliwa Juni 14 mwaka 1920 na amefariki
Agosti 14 mwaka huu akiwa na miaka 96. Enzi za uhai wake, mbali na urais wa
Zanzibar na uenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Jumbe aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti
wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia kiongozi wa Chama cha Afro Shiraz (ASP) kabla
ya kuungana na Tanu na kuzaliwa CCM.
Aidha Jumbe anatajwa kutoa mchango mkubwa wakati vyama vya Tanu na
ASP vilipoungana mwaka 1977 kwa kuridhia muungano huo. Mwaka 1979, Jumbe
alikuwa mwanzilishi wa mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar kwa mara ya kwanza
ambayo ilisababisha kutenganishwa Baraza la Mapinduzi na Baraza la Wawakilishi.
Mapema mwaka 1984 Jumbe alienguliwa kwenye nyadhifa zote hizo kwa
kile kilichodaiwa kuchafua hali ya kisiasa Zanzibar.
Jumbe pia ndiye aliyeanzisha mfumo wa uwakilishi baada ya kufutwa,
kufuatia Mapinduzi ya mwaka 1964 yaliyouondoa utawala wa Sultani.
Taarifa zinaonesha kuwaJanuari 1984, Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM,
iliyoketi mjini Dodoma kwa dharura, ilimvua Jumbe nafasi zote za uongozi,
ikidaiwa alihoji muundo wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mazrui
Akimzungumzia marehemu Jumbe
Naibu Katibu Mkuu wa
Chama cha Wananchi (CUF), Nassor Mazrui alisema Wazanzibar wamepata pigo kubwa ambalo hawawezi kulisahau. Mazrui alisema Jumbe alikuwa msomi wa kwanza kabla ya Mapinduzi ya Zanzibar hali iliyochangia awe na mitazamo chanya kwa nchi yake.
"Kwa kizazi cha sasa hamuwezi kuwa na kumbukumbu ila huyo
Jumbe ni msomi wa kwanza katika kipindi cha Mapinduzi lakini alikutana na
changamoto nyingi hali ambayo watu wamebakia kumsoma katika vyombo vya habari
pekee," alisema.
Mbowe
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema
kiongozi huyo ni moja ya vielelezo visivyo na mfano katika nchi kwa kile
alichodai kuwa alitengwa na Serikali na CCM kwa misimamo na ukweli ambao
aliamini.
"Mimi namkumbuka kama kiongozi ambaye alisimamia misimamo yake
bila woga hivyo kwa viongozi ambao hawakupenda ukweli, waliamua kumtenga na
jamii," alisema. Mbowe alisema kiongozi huyo kwa mchango wake alioutoa
katika Taifa hasa Zanzibar alipaswa kuenziwa ili vizazi vya sasa viweze
kumtambua na kumuenzi.
Ligora
Katibu wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Kapteni mstaafu
Mohamed Ligora alisema kifo cha Jumbe ni msiba mzito kwa jamii ya Tanzania na
kuwa Jumbe alikuwa mtumishi mwadilifu na mwenye kujiamini. Alisema marehemu alikuwa
mvumilivu na mwenye kunyamazia mambo hata kama yalikuwa linamkwaza jambo ambalo
kwa sasa viongozi wengi hawana.
Ngayoga
Mtangazaji wa zamani wa Radio Tanzania(RTD), sasa TBC Taifa,
Mohamed Ngayonga alisema anamkumbuka Mzee Jumbe kwa mengi huku akibainisha
jambo kubwa alikuwa ni mtu mwenye msimamo, asiyeyumbishwa na kukubalika kwa
Wazanzibar.
0 comments:
Post a Comment