Sharifa Marira
MAANDAMANO ya Kupinga
Udikteta Tanzania (Ukuta) yaliyokuwa yamepongwa kufanyika leo yalizua hofu na
taharuki miongoni mwa wananchi huku wengi wakieleza yangetokea wasingefanya
shughuli zao.
Maandamano hayo yaliyoasisiwa
na Chadema, hata hivyo yalitangazwa kusitishwa kwa muda wa mwezi mmoja hadi
Oktoba mosi, ambapo mwenyekiti wake Freeman Mbowe alisema wamefanya hivyo ili
kuwapa nafasi viongozi wa dini kutafuta suluhu na serikali ya Rais John
Magufuli.
JAMBO LEO lilifanya
mahojiano na baadhi ya wananchi kutokana na mategemeo yao juu ya siku hiyo
ambapo walikuwa na maoni tofauti huku wengine wakidai kwamba wangejifungia
ndani.
Semambe Mshana, mkazi wa
Mbuyuni jijini Dar es Salam alisema endapo (Ukuta) ungetokea asingetoka katika
shughuli zake za kila siku kwani alishuhudia Askari wakifanya mazoezi ya wazi
maeneo mengi hivyo alijua kutatokea vurugu.
“Kesho (leo) nisingetoka
kwenye pilika pilika zangu, sababu nilitegemea itakuwa siku ya fujo, na ghasia
tuu, hivyo basi ningebaki nyumbani tuu ila nilikuwa naomba muwafaka upatikane
kati ya serikali na vyama vya upinzani ili kuwe na utulivu na watu tuendelee na
kupambana na maisha”alisema Mshana
Alieleza kuwa alijawa na
hofu kutokana na kuona nguvu za viongozi wa dini na wanasiasa wakijitahidi
kutafuta suluhu lakini Chadema wakiendelea na msimamo wao wa kudai maandamano
yapo pale pale hivyo alikuwa anamuomba mungu pekee kuepusha.
Zainab Issa ambaye ni
Mwalimu Mkazi wa Makongo Juu alisema hakuwa anategemea kufanya chochote zaidi
ya kukaa nyumbani kusikiliza yatakayojiri.
“Nilijua kabisa polisi
watakuwepo barabarani na leo (jana)
niliona ndege za wanajeshi zikipita mapema asubuhi nikaambiwa ni za
kivita hivyo niliona ni vyema kutulia nyumbani kuliko kwenda barabarai kuumizwa
wakati siwezi kufaidika na chochote kutokana na maandamano hayo”alisema
Judith Mvella wa Mwanza
alisema alitegemea kutembelea familia za watu walioumia kwani alishajua polisi
wamekasirika kwa kuwa walishakemea maandamano hivyo ambaye angefanya hivyo
angekuwa ametafuta kupigwa.
“Naishi na dada angu hapa
Mwanza lakini tulishaamua kama familia hakuna watoto kwenda shule,biashara yetu
ya duka la nguo tusingefungua kwasababu hatukujua maandamano yangeanzia
wapi,tulikuwa tunaogopa kupata hasara ya kujitakia”alisema Mvella
Zuhura Masoud wa Tabata
Dar es Salaam alisema alitegemea kuendelea na shughuli zake na endapo atakutana
na maandamano njiani angeweza kuunga mkono jitihada hizo za kutetea demokrasia.
“Nilijua Ukuta utafanyika
ili wanademokrasia wenzangu wafikishe ujumbe kwa serikali kama tunataka nchi
iwe yenye uhuru na demokrasia na mfumo wa vyama vingi uheshimiwe”alisema Masous
na kuongeza kuwa
“Chadema wamefanya jambo
jema kuwasikiliza viongozi wa dini lakini wasiishie hapo wanapaswa kupaza sauti
zao bila kuchoka kutokana na kuwa wanachokipigania wananchi
tunakihitaji,natamani itokee tena siku ya Ukuta’’
David Kahumbi ,kutoka
Shinyanga alisema alijua kama maandamano hayo hayawezi kufanyika kutokana na
watanzania wengi kuwa waoga wa kudai demokrasia lakini pia vitisho vya polisi
vilichangia kuwarudisha watu nyuma.
“Huku migodini
tungeendelea na shughuli zetu kama kawaida,nawajua watanzania walivyo vitisho
vya polisi ilikuwa ni njia moja wapo ya kuwafanya warudi nyumba,ila Chadema
waendelee kudai demokrasia kwa njia nyingine”alisema Kahumbi
Jackline Yeuda mkazi wa
Mbezi Tangi Mbovu alisema anaishi na wadogo zake wawili ambao alishawaagia
katika shule wanazosoma kwamba kwa siku ya Ukuta wasingeweza kwenda shule
kutokana na kwamba wakati wa kupigwa mabomu hayachagui aliyeandamana na ambaye
hajafanya hivyo.
Alisema kwa kuwa ni kijana
anayependa demokrasia alihamasisha vijana maeneo mbalimbali kuandamana bila
kujali ni kiasi gani wameumizwa na polisi lakini ujumbe ungefika.
Rashidi Mahanyu wa Mlalo
Tanga alisema wananchi wa maeneo hayo hawakuwa wanafuatlia jambo lolote kuhusu
Ukuta hivyo hata ungefanyika kusingekuwa na madhara yoyote.
Boniface Mteketa,wa Gongo
la Mboto alisema Ukuta ungemfanya ashindwe kula kwani anamiliki kibanda cha
kuuza vifaa vya simu ambacho kipo barabarani hivyo endapo kurupushani
zingetokea alijua atakuwa muathirika wa kwanza hivyo aliamua kutokufanya kazi.
Salma
Mahamdu,alisema”Katika vitu ambavyo nilikuwa sivipendi ni huo Ukuta,sikuwa
najua maana yake na haikuwa unatusaidia chochote,nimeshukuru kusikia
hayafanyiki kwa kuwa yangeumiza watu wasiokuwa na hatia,wamuache rais afanye
kazi ya kutuletea maendeleo”
Abdallah Hamisi, wa Mabibo
Dar es Salaam alisema Kusitisha maandamano ni jambo zuri kwani serikali ilikuwa
inatumia nguvu kubwa na haikuwa na
dhamira ya nzuri kwa wananchi hivyo yanghetokwea machafuko makubwa ambayo ni
bora Chadema walivyoyaepusha.
“Kwa namna nyingine naona
jinsi serikali inavyotumia majeshi yake kukandamiza demokrasia hivyo naona kama
ni kifo cha demokrasia kwani watakuwa
hawako huru” alisema Hamisi.
0 comments:
Post a Comment