* Ni sawa na alivyoondoka Mrema
Moi Dodo
SPIKA mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa amesema Waziri Mkuu wa
zamani, Edward Lowasa hakukosea kuondoka CCM na kujiunga na upinzani, lakini
asijidanganye kuwa bado ana nguvu kisiasa.
Msekwa alisema hayo hivi karibuni alipozungumza katika
mahojiano maalumu na gazeti hili nyumbani kwake Oysterbay, jijini Dar es
Salaam.
“Kwenye Biblia kuna mtu anaitwa Samson alikuwa na nguvu
nyingi, aliweza kuvunja hata mageti ya chuma. Maadau zake walipoona
wamemshindwa wakaamua kumtumia mwanamke sijui anaitwa nani yule…”
Aliendelea “yule mwanamke alimdanganya na akafanikiwa
kumwambia kuwa nguvu zake ni nywele zake na walipomnyoa kweli bwana nguvu zake
zikaisha.”
“Sasa Lowassa asijidanganye kuwa bado ana nguvu kisiasa, ni
kama Samson. Yeye alipotoka CCM akaacha nguvu zake huko. Nywele za Lowassa na
hata Mrema wakati huo ni CCM. CCM ina nguvu ya asili ambayo mtu ukitoka
unaiacha.”
Majibu wa Lowassa
Alipotakiwa kuzungumzia kauli hiyo ya Msekwa, Lowassa
alisema “Hayo ni maoni yake, hivyo hawezi kuyajadili.”
Alisema “Msekwa alisema lini hayo? Lakini siwezi kuzungumzia
hilo kwa kuwa hayo ni maoni yake na nguvu zangu Msekwa hawezi kuzijua.”
Kwa nini hakukosea
kuhama?
“Wale wanaodai kuwa alifanya kosa, wanaudanganya umma.
Hakukosea kabisa. Ukisoma Katiba ya CCM, kifungu cha 13, kinaeleza kuwa mtu
anaruhusiwa kujitoa ndani ya chama kwa kujiuzulu au kuhamia chama kingine,
endapo ataona kuwa utendaji wa chama haumridhishi.
“Kwa hiyo, Lowassa aliona kuwa haridhishwi na mambo yanavyoendelea
ndani ya CCM ndiyo maana akaamua kuondoka na kuhamia Chadema ambako aliona kunamfaa
zaidi,” alisema Msekwa na kuongeza;
“Katiba ya chama iko wazi na wala haimfungi mwanachama
kuhama au kujiuzulu. Ukiona kuwa mambo yanayotendeka ndani ya chama
hayakuridhishi, basi uko huru kuondoka na wala hakuna atakayekuuliza.”
Mtikisiko wa Lowassa
Akizungumzia mtikisiko uliosababishwa na kuondoka kwa
mwanasiasa huyo nguli, Msekwa alisema CCM haikupata wakati mgumu, kwani ina
nguvu kubwa ambayo inaifanya ipambane nyakati zote.
“CCM haikitikiswa kwa namna yoyote na kuondoka kwa Lowassa,
kwani ilishajiandaa na ikumbukwe kuwa chama kina nguvu ya ndani ambayo
inakifanya kihimili vishindo vya kila namna. Hivyo watu waache kuamini kuwa
kuondoka kwa Lowassa kuliifanya CCM ipitie wakati mgumu kuliko wakati mwingine wowote,”
alisema Msekwa.
Msekwa alisema kuondoka kwa Lowassa ndani ya CCM kunafanana
kwa kiasi kikubwa na safari ya Augustine Mrema mwaka 1995, baada ya
kutoridhishwa na mambo yalivyokuwa ndani ya chama wakati huo.
“Kuondoka kwa Lowassa ni sawa kabisa na Mrema, alipoamua
kujiondoa CCM mwaka 1995. Aliondoka na watu walidai kuwa huo ndiyo ulikuwa
mwisho wa chama lakini wapi? Kilishinda tena kwa kishindo na kimeendelea
kushinda uchaguzi wote,” alisema Msekwa.
Aidha, Msekwa alisema kuwa umaarufu na nguvu walizokuwa nazo
kina Lowassa na Mrema, zilitokana na uwepo wao ndani ya CCM na hivyo kuondoka
kwao kumewafanya wasahaulike kwa haraka kwenye medani za siasa.
“Nguvu alizokuwa nazo Lowassa zilitokana na umaarufu mkubwa
wa CCM. Si mnamkumbuka Samson wa kwenye Biblia? Yule bwana alikuwa na uwezo wa
ajabu wa kupambana na kushinda watu zaidi ya 1,000. Hakukuwa na mtu aliyefahamu
siri ya nguvu zake.
“Lakini baada ya maadui zake kumpeleleza kwa muda mrefu na
kwa kutumia mwanamke aitwaye Delila, walifanikiwa kufahamu kuwa nguvu zake
zilikuwa katika nywele hivyo wakamnyoa.
“Lowassa naye nguvu zake zilikuwa ndani ya CCM, hivyo muda
si mrefu yatamkuta yaliyowakuta Mrema na Samson. Hatodumu katika umaarufu na
nguvu alizokuwa nazo kama kipindi alipokuwa CCM,” alisema Msekwa.
Awali, Msekwa aliwataka Watanzania wawe na kumbukumbu ya
enzi za Mrema alipoondoka CCM na watu wengi kumfuata kiasi cha baadhi yao
kusukuma gari lake kwa ushabiki.
“Unajua watu hawataki kukumbuka matukio yaliyowahi kutokea,
japokuwa si ya miaka mingi. Nakumbuka mwaka 1995, wakati Mrema akijitoa ndani
ya CCM, maelfu ya watu walimshangilia na kumfuata alikokuwa akienda. Aliondoka
na wanasiasa mashuhuri kama Wassira (Stephen), Marando (Mabere), Lamwai
(Masumbuko) na Ndobho (Paul).”
“Lakini, cha kushangaza ni kwamba baada ya kuondoka nao na
kudumu na umaarufu wake kwa muda usiozidi miaka miwili, yuko wapi leo? Si ajabu
na hao mambo yaliyompata Mrema yakampata na Lowassa,” alisema Msekwa.
0 comments:
Post a Comment