Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe |
WAKATI Chadema ikitangaza
msimamo wa kuzindua Operesheni ya Umoja wa Kupambana na Udikteta Tanzania
(Ukuta) Septemba mosi, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu amesema
hajapata taarifa kuhusu suala hilo na hivyo hawezi kulizungumzia.
Akizungumza na Jambo Leo
jana, Mangu alisema kama angekuwa amepelekewa barua kuhusu mchakato huo
angezungumza, lakini kutokana na kuwa suala hilo bado halijafanyika hawezi kuzungumza.
"Siwezi kuzungumza
chochote kuhusu hilo, kwa maana hawajaleta barua yoyote ya kujulisha kuwa siku
hiyo watafanya maandamano na mikutano nchi nzima," alisema Mkuu wa Polisi.
Alitaka aachwe hadi chama
hicho kitakapopeleka barua ndipo atoe majibu kuwa ni hatua gani zitachukuliwa.
"Subirini niletewe barua kueleza kuwa wanataka kufanya nini na baada ya
hapo nitatoa majibu, maana kwa sasa nitakuwa nazungumza wakati barua
sijaiona," alisema.
Chadema
Chadema ilisema msimamo wake kuhusu kuandamana na kufanya mikutano kuanzia Septemba mosi uko palepale kwani lengo lao ni kulinda Katiba na sheria za nchi.
Aidha, ilisema maandamano
yao yatakuwa ya amani, hawatavunja sheria za nchi na kuwa lengo la kufanya
hivyo ni kupigania haki za Watanzania wengi ambao wanakosa haki zao.
Naibu Katibu Mkuu wa
Chadema Zanzibar, Salim Mwalimu wakati akizungumza na gazeti hili jana,
alisisitiza kuwa wako tayari kwa mazungumzo iwapo watahitajika kabla ya tukio
hilo. Mwalimu alisema tafsiri ya Ukuta, si kufanya fujo bali kupinga mfumo wa
uongozi wanaodai kuwa umekuwa wa mtu mmoja.
Alisema Chadema kupitia
kamati ndogo ambazo ziliundwa, inaendelea na maandalizi ya mikutano na maandamano
nchi nzima Septemba mosi na kutaka wanachama na Watanzania kuhakikisha
wanatekeleza azimio hilo kwa amani na utulivu.
"Chadema hatuna
ugomvi na Jeshi la Polisi na hatutarajii kupambana nao tunachotaka ni kuonesha
kuwa hatukubaliani na uamuzi ambao Serikali kupitia Rais John Magufuli aliutoa
wa kuzuia mikutano hadi mwaka 2020," alisema.
Mwalimu alisema
haiwezekani wakakubaliana na hali hiyo, kwani siasa ndiyo kazi iliyomfanya awe
Chadema na kuacha ajira zingine ambazo zilikuwa zinamtaka akae ofisini.
Alisema jambo la
kusikitisha ni kuona Rais anafanya mikutano na kutumia nafasi hiyo kuwakebehi,
jambo ambalo si la kiungwana na eneo sahihi la kujibu hoja zake ni kupitia
mikutano kama anavyofanya yeye.
"Tunafuatilia kila
anachofanya kwenye mikutano yake, hazungumzii Serikali yake ila muda mwingi
anatusema sisi na kupandisha jukwaani watu wake, ili kutusema hii haikubaliki,
hivyo tutapigania haki hii ya kufanya mikutano bila kurudi nyuma,"
alisema.
Aidha, Mwalimu alivitaka
vyama vya siasa viliovyo tayari kushirikiana nao katika harakati hizo
vinakaribishwa, kwani harakati hizo si za Chadema ila ni kwa faida ya Taifa.
Kwa upande mwingine, Mwalimu amelalamikia Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi kuingia
katika vikao vya ndani vya Chadema na kuchukua viongozi wao bila sababu za
msingi.
0 comments:
Post a Comment