Na SharifaMarira
MWANASIASA
Mkongwe Nchini, Kingunge Ngombale Mwiru amewaomba viongozi wakuu wastaafu wa kitaifa
kuzungumza na Rais John Magufuli kuhusu mgogoro uliopo kati ya Chama cha Demokrasia na
Maendelo (Chadema) na Serikali ili kuepusha uvunjifu wa amani.
Kingunge
alisema hayo jana akieleza hali iliyopo sasa ya mvutano kati ya Serikali na
Chadema kupitia Operesheni ya Kutetea Demokrasia (Ukuta) iliyopangwa kufanyika
Septemba Mosi, busara za wazee hao zinahitajika kwa kukutana na Rais Magufuli
kumshauri isipokuwa, lakini bila kuwemo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya
Kikwete.
Ametoa
kauli hiyo zikiwa zimesalia siku saba kabla ya kufanyika kwa Opereseni Ukuta,
wakati alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya kisiasa nchini na
kauli ya Rais Magufuli kupiga marufuku mikutano yote ya kisiasa ambayo alidai
ndiyo iliyoleta mgawanyiko na ni
uvunjifu wa katiba na kuvinyima haki vyama vya siasa.
“Nawaombeni
wazee wa nchi hii, Kikwete hastahili katika hili, zungumzeni na mzee mwenzenu
Magufuli kwa haraka zaidi kwani zimebaki siku saba pekee ifanyike Opresheni
Ukuta, ambayo itaumiza vijana wa kitanzania na amani itatoweka. Haki
isipotendeka hakuna amani daima,” alisema Kingunge.
Alifafanua
kwamba Kikwete hastahili kuwepo katika kundi hilo akimtaja ndiye aliyelifikisha
Taifa lilipo sasa katika ombwe la uongozi kwa kuacha waliokuwa na uwezo bila kuwapa
nafasi kuongoza.
Aliongeza:
“Wazee wenzangu ambao wote mliapa kwa kauli ya kuilinda,kuihifadhi na kuitetea
katiba ya nchi,msikae kimya hivi sio sawa,lazima tujitokeze tuhesabiwe,hatuwezi
kubaki nyuma tukubaliane kuingilia kati jambo hili tusisubiri yatokee matatizo
ndiyo tuzungumze.”
Kingunge
alisema jambo kubwa ambalo wazee wanapaswa kuomba kuonana na Magufuli ni
kumuomba aitishe kikao cha mazungumzo na Chadema na kwamba baada ya kufanya
hivyo watakigeukia chama hicho kuwataka wasitishe Ukuta ili kuepusha shari na
uwezekano wa kuvuja damu.
“Hakuna
sababu ya kumwaga damu wakati wazee wenye busara tupo,ingekuwa Chadema
wanavunja katiba na sheria serikali ingekuwa inafanya vyema kuwashikisha adabu
lakini sasa serikali inashindana na watu wanaotetea haki na katiba ambao ndio
kundi kubwa”alisema Kingunge
Alisema
kauli ya Magufuli ndiyo iliyosababisha mgawanyiko wa maoni katika jamii wapo
waliomuunga mkono lakini kundi kubwa halijakubaliana na amri yake hivyo
yanayotokea sasa yanatokana na kauli yake ni vyema wazee kutoyafumbia macho ili
nchi ibaki salama.
Alisema
endapo wastaafu hao hawatafanya jitihada hizo jambo lolote linaweza kutokea na
ni wazi kwamba Amani itaponyoka kutokana na hali ya kisiasa kuwa tete ,ina
utata na ni ngumu.
Alisema
ni vyema wazee wakakumbuka kuwa wajibu walio nao kwa watanzania ni kutumia
busara zao kama walivyokula viapo na kwamba jambo hilo sio la Chadema ni la
watanzania wote.
“Kama
tunavyoona kuna pande mbili zinazovutana upande mmoja unanoa mapanga,visu na
silaha za moto na kufanya mazoezi wazi wazi ili kuwakomesha wengine lakini
ukiangalia raia wa kawaida wanalilia Amani bila kujua kwamba haiwezi kupatikana
bila haki”alisema
Hata
hivyo Kingunge alisema nchi kwa sasa ina ombwe la uongozi lakini wapo viongozi
wengine waliopo nje ya serikali ambao wana uwezo wa kuongoza na hawajapewa
nafasi na kwamba kuna umuhimu kwa watu wanaopewa madaraka kuzijua na
kuziheshimu haki za kisiasa.
Alisema
tatizo kubwa lililopo sasa binadamu wanaishi kwa chuki na uhasama ndiyo maana
Amani inaweza kutoweka na kwamba mungu anawasaidia watu wanaojisaidia hivyo
wanaoomba wananchi kuombea Amani ya nchi ni vyema wakawa wa kwanza
kusimamia,kulinda na kutetea haki.
Mwisho.
0 comments:
Post a Comment