Waandishi Wetu
SPIKA mstaafu wa Bunge,
Pius Msekwa amesema kazi ya Jeshi la Polisi ni kutekeleza maagizo ya Rais na si
kubeba chama tawala.
Aidha, Msekwa alitaja adui
wa Chama Cha Mapinduzi, akisema adui huyo yupo karibu lakini anaweza kuwa mbali
na atatokea na kukidhuru iwapo kitafanya makosa.
Msekwa alitoa kauli hiyo
hivi karibuni kwenye mahojiano maalumu aliyofanya na gazeti hili nyumbani kwake
Dar es Salaam.
Alikuwa akijibu swali
lililomtaka aeleze mtazamo wa baadhi ya watu kwamba kwa kubaki madarakani muda
mrefu, CCM imefanya taasisi zote za Serikali ikiwamo Polisi na wanachama wake.
Kwa nyakati tofauti
wapinzani wamekuwa wakilalamika kuwa Polisi haiwatendei haki. Imekuwa ikizuia
mikutano yao na kuwadhibiti wanapotaka kufanya maandamano lakini CCM iko huru
kufanya siasa.
Majibu
“Polisi hawatakiwi
kupendelea chama cha siasa, wanachotakiwa ni kutekeleza maagizo ya Rais na
kutenda haki kwa vyama vyote. Kama Rais amezuia mikutano ya hadhara, agizo hilo
libane pia CCM,” alisema Msekwa na kuongeza:
“Labda nichukue fursa hii
kueleza kuwa kama polisi wanadhani wanatakiwa kupendelea CCM wamekosea na kama
kuna watu wanaamini kuwa polisi ni tawi la CCM ni fikra potofu, kwani hata
Lowassa (Edward) angeshinda Uchaguzi Mkuu mwaka jana, polisi haohao
wangetekeleza maagizo yake.”
Adui wa CCM
Kuhusu adui wa chama hicho
tawala, Msekwa alimtaja kuwa ni CCM yenyewe iwapo itafanya makosa katika kuteua
wagombea uongozi.
Alikuwa akijibu swali
lililotaka kujua kwa mtazamo wake kwa sasa ni nani adui wa CCM.
Kauli hiyo ya Msekwa
inafananishwa na iliyopata kutolewa na Mwenyekiti wa kwanza wa CCM, Baba wa
Taifa, marehemu Mwalimu Julius Nyerere kwamba: “Mpinzani wa kweli wa CCM,
atatoka CCM.”
Nyerere alitoa kauli hiyo
kukihadharisha chama hicho, kwamba iwapo kitafanya makosa na baadhi ya watu
wenye nguvu wakatoka na kugeuka wapinzani, wataipa wakati mgumu CCM.
Naye Msekwa alisema: “Adui
wa CCM ni CCM yenyewe kama itafanya makosa ya kuleta mgombea asiyetakiwa. Kama
ingefanya makosa ya kumpitisha… tungefanya makosa ya kumleta …tusingepita.
“Walikuwa wanatwambia,
‘mkimpitisha (anamtaja), mtakwenda na maji’.
Watu wanachukia mtu. Adui mkubwa wa CCM ni madhara ya kujitakia wenyewe.
Unaleta mgombea ambaye hatakiwi, lazima utaanguka tu.”
Alitaja mifano mingi ya
watu kutokubalika akisema katika mambo ya siasa kikubwa si chama au chombo
anachoongoza, bali kiongozi anavyokubalika.
“Kuna mifano mingi, baadhi
ya majimbo katika uchaguzi watu walisema akigombea huyu, hata akiwekwa na jiwe
tutachagua jiwe,” alisema.
Alipotakiwa kueleza kama
adui huyo wa CCM yupo karibu au mbali, Msekwa ambaye ni mjumbe wa Baraza la Wazee
ndani ya chama hicho alisema: “Hiyo ni ramli sasa, hatuwezi kujua inategemea
mazingira.”
Baraza la Wazee ndani ya
CCM linatajwa kuhusika kuchuja na kukata majina ya wana CCM waliotaka kuteuliwa
kuwania urais, akiwamo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowasa na Benard Membe
aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, walioonekana
kuzua mvutano ndani ya chama hicho, kwa kuwa na wafuasi wengi zaidi.
Katika mchujo wa Baraza
hilo, jina la Lowasa lilikatwa bila kufika mchujo wa tano bora, huku Membe
akikatwa baada ya kufika hatua ya tano bora, ndipo Dk John Magufuli akapenya na
kuongoza hata kupata nafasi ya kupeperusha bendera ya CCM kuwania urais na kushinda.
Akifafanua kuhusu alipo
adui wa CCM, Msekwa alisema: “Anaweza kuwa yupo karibu kwa maana ya miaka
mitano ijayo utakapofanyika uchaguzi, lakini kwa kuwa tunaye Rais Magufuli,
hatutafanya makosa kutomweka Magufuli, tunajua atamaliza miaka 10 hadi 2025,
hivyo adui yuko mbali kwa maana hiyo.”
Msekwa alisisitiza kuwa
adui mkubwa wa CCM ni CCM yenyewe, hasa pale itakapokuwa ikienda kinyume na
matakwa ya Katiba yake kwa ajili ya maslahi ya watu wachache wenye utashi na
dhamira ya kujilimbikizia madaraka.
Alisema CCM ina misingi
yake ambayo imewekwa na Katiba ya chama hicho, hivyo haina budi kufuatwa hata
kama inahatarisha maslahi ya chama, kwani kwenda kinyume na Katiba ni dhambi ya
kukiua chama.
“Usisubiri adui wa CCM
atoke nje ya chama au kiwe chama kingine, haiwezekani na kamwe haitawezekana.
Adui wa CCM ni CCM yenyewe, kwa maana kuwa pale viongozi wanapoanza au kuamua
kupitisha jambo au mambo fulani ili kulinda maslahi yao.
“Mara watakapoanza kufanya
hivyo na kwenda kinyume na Katiba, basi chama kitakuwa na muda mfupi wa kuishi.
Fanya makosa mengine yote lakini si ya kwenda kinyume na Katiba, kwani lazima
chama kisambaratike na kupoteza mwelekeo moja kwa moja,” alisema Msekwa.
Bunge
Katika hatua nyingine,
Msekwa alijibu maswali kadhaa kuhusu uendeshaji wa Bunge, akisema anavyoona
hakuna jipya kwa kuwa hata vurugu za Upinzani zilipata kutokea enzi zake akiwa
Katibu wa Bunge.
“Kama ni vurugu hata enzi
zile zilikuwapo, lakini tulifanikiwa kuzidhibiti na hali ilikuwa shwari,”
alisema Msekwa akitaja wanasiasa machachari wa wakati huo kuwa ni pamoja na Dk
Masumbuko Lamwai, Steven Wasira, Mabere Marando na Paul Ndobho.
Hata hivyo, Msekwa
alieleza tofauti za wanasiasa hao na wabunge wa sasa wa upinzani kuwa ni
uvumilivu akisema:
“Hawa (Marando, Lamwai,
Wasira na Ndobho) walikuwa machachari kuliko wabunge wengi wa sasa, lakini
mambo yetu tuliyamaliza bungeni. Siku hizi nashangaa kuona mwakilishi wa
wananchi anasusa Bunge!
“Bunge unamsusia nani?
Wewe umetumwa kuwakilisha wananchi halafu unatoka bungeni, unasusa! Hiyo ndiyo
tofauti kubwa ninayoiona, ni ajabu kweli.”
Msekwa alipuuza madai kuwa
wabunge wa sasa wanasusa Bunge wanapoona mambo hayaendi sawa, kwa sababu ni
damu changa zinazohitaji mabadiliko ya haraka, akisema: “Kila wakati kuna
vijana wake, hata mimi niliwahi kuwa kijana. Bunge nililoongoza nalo lilikuwa
na vijana kwa wakati ule, lakini hawakufanya haya.”
Msekwa hakuweka wazi kuwa
tatizo la wabunge wa sasa ni elimu. Lakini akasema “Elimu hutafutwa, na Biblia
inasema usimwache elimu akaenda zake. Kwa nini wasitafute elimu?”
Alisema ni wajibu wao
kutafuta elimu ili iwasaidie katika kuwakilisha wapiga kura wao bungeni badala
ya kudhani wanajua kumbe wanaboronga.
0 comments:
Post a Comment