Suleiman Msuya
JUKWAA la Wahariri
Tanzania (TEF) limepinga uamuzi wa Serikali kuvifunga vituo Radio 5 ya Arusha
na Magic FM cha Dar es Salaam likieleza kuwa uamuzi huo haukuzingatia misingi
ya utawala bora na kutoa mwito kwa Waziri husika kutafakari upya suala hilo.
Taarifa iliyotolewa jana na
TEF kupitia Katibu Mkuu wake, Neville Meena, ilisema kwa miezi takriban 10 tangu alipoteuliwa kuwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amejitokeza mara nne kutangaza
kufuta na kufunga baadhi ya vyombo kwa muda usiojulikana.
Alisema TEF imeshitushwa
na kusononeshwa na hatua ya Serikali kupitia kwa Waziri huyo kuvifunga kwa muda
usiojulikana vituo hivyo, huku sababu iliyotolewa ikiwa ni siri yake.
TEF ilisema kwa sababu
hiyo, si rahisi kwa waandishi wengine wa habari kujifunza kwa makosa ya wenzao
kwa kuwa mchakato uliotumika kushughulikia suala hilo umebaki kuwa siri ya Waziri.
“Alianza kulifuta Gazeti
la Mawio, baadaye alitangaza kufuta mamia ya magazeti na majarida ambayo
hayajachapishwa kwa muda mrefu, ikafuata adhabu ya kulifungia kwa miaka mitatu
Gazeti la Mseto na sasa vituo viwili vya redio,” alisema.
Alisema katika tukio la
kufutwa kwa Mawio, walihoji ukubwa wa kosa la gazeti hilo na sababu za kufutwa.
“Leo hii tunahoji tena ukubwa wa makosa na pengine historia ya redio husika
siku zilizopita. Ndiyo maana tunasema hili la sasa ni mwendelezo wa
ukandamizaji wa uhuru wa habari,” taarifa hiyo ilisema.
TEF ilisema inachukulia
hatua hiyo kama mwendelezo wa ukandamizaji wa uhuru wa vyombo vya habari nchini
na wanashindwa kuelewa dhamira ya Serikali kwa sekta ya habari nchini.
Ilisema kinachoonekana ni
kutumia kila aina ya sheria kukandamiza
uhuru wa vyombo vya habari na kuwa hawaoni nia ya malezi katika uamuzi wa
Waziri.
Msimamo wa TEF
Utaratibu uliotumiwa na Waziri
hata kufikia uamuzi huo, umekuwa wa makosa ya siku zote. Pamoja na kwamba
vyombo vya habari hufanya makosa, lakini hata makosa yanapotokea taratibu za
kuyashughulikia lazima zizingatie misingi ya utawala bora, haki na demokrasia.
Mfumo wa kushughulikia
matatizo au kasoro za kitaaluma katika vyombo vya habari ni kandamizi kwani
unamfanya Waziri kuwa na mamlaka ya kutoa adhabu, kwa kuzingatia mtazamo wake,
hata kama unakinzana na misingi ya taaluma.
Kimsingi uamuzi wa Nape
unaonekana kukosa nia njema ndani yake, kwani Kifungu cha 28 cha Sheria ya
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) alichotumia kutoa adhabu hiyo,
hakimlazimishi kufungia vituo vya redio kama alivyofanya.
Kosa la vituo hivyo kwa
mujibu wa Waziri ni uchochezi, lakini hakuweka bayana maudhui ya vipindi au
habari ambazo zilivifanya vituo hivyo ‘kutiwa hatiani’ na baadaye kufungwa
kwake kwa muda usiojulikana.
0 comments:
Post a Comment