Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Biashara
imemwamuru Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Dk Reginald Mengi, kujieleza kwa nini
asifungwe jela kwa kushindwa kutekeleza hukumu ya kulipa dola 598,750 za Marekani
sawa na Sh bilioni 1.2.
Kiwango hicho ni malipo ya
wafanyabiashara watatu; Muganyizi Lutagwaba, Eric Mshauri na Charles Mgweo,
kutokana na mgogoro unaohusu malipo ya uuzaji hisa kwenye kampuni ya Douglas
Lake Minerals Ltd, ambayo kwa sasa inaitwa Handeni Gold Inc.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na
wafanyabiashara hao ilisikilizwa na Jaji Agathon Nchimbi huku Dk Mengi na
kampuni ya K.M. Prospecting Limited wakiwa ndio walalamikiwa.
Kwa mujibu wa hati ya mwito, Dk Mengi
anatakiwa kufika mahakamani hapo Agosti 24 kujieleza kwa nini asifungwe
gerezani kama sehemu ya kukazia hukumu hiyo.
Hatua hiyo ya Mahakama inatokana na
wafanyabiashara hao kuwasilisha maombi ya kuiomba Mahakama ikazie hukumu hiyo
ya Januari 28.
Hati ya kiapo cha pamoja cha
wafanyabiashara hao, ilieleza kuwa walifungua shauri kwenye Mahakama hiyo
wakidai malipo yaliyobaki ambayo ni dola 428,750, dola 100,000 na dola 70,000,
kila mmoja.
Walieleza kuwa baada ya ushahidi
kutolewa, Mahakama ilitoa hukumu dhidi ya walalamikiwa na hadi jana hawakuwa
wamekata rufaa dhidi ya hukumu hiyo.
Walisema ingawa Dk Mengi ni
mfanyabiashara maarufu anayejulikana kuwa na fedha, akaunti za benki, mali
zinazohamishika na zisizohamishika, lakini juhudi za wao kupata mali hizo
zikiwa na jina lake au ushahidi wowote wa umiliki wake, ziligonga mwamba.
Walalamikiwa wameeleza kuwa juhudi kama
hizo zimefanyika pia na Kampuni ya K.M. Prospecting Limited ambayo pia
inadaiwa, lakini zimeshidikana kuwa mali na akunti zake za benki hazijulikani
zilipo.
Kufuatia hali hiyo, walalamkaji
wanaeleza kuwa juhudi za kukamata mali za walalamikiwa ili kutimiza matakwa ya
hukumu iliyotolewa yameshindikana.
Hivyo walidai kuwa namna pekee ya
kutekeleza hukumu hiyo ni kumtaka mlalamikiwa afike mahakamani na kujieleza kwa
nini asipelekwe gerezani na kwamba ni jukumu lake kueleza mali zake ziliko ili
zitumike kutekeleza matakwa ya hukumu.
Taarifa zaidi zilionesha kuwa tayari Dk
Mengi alishapelekewa hati ya mwito huo wa Mahakama.
0 comments:
Post a Comment