Lema apandishwa kizimbani akiwa dhaifu

Seif Mangwangi, Arusha

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi ya Mkoa wa Arusha  imesimama kwa muda baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza huku amedhoofu.

Lema alifikishwa mahakamani hapo jana baada ya kushikiliwa kwenye mahabusu ya Polisi kwa takribani siku nne.

Hata hivyo, tafrani nyingine iliibuka baada ya askari waliopandisha kizimbani kutaka kumpeleka Magereza baada ya kutokidhi masharti ya dhamana aliyopewa na   baada ya nyaraka za wadhamini wake kutokuwa sahihi.

Mbunge huyo machachari alisomewa mashitaka mawili yaliyokuwa yakimkabili mbele ya

Hakimu Mkazi, Desdery Kamugisha huku upande wa Serikali ukiwakilishwa na Mwanasheria Innocent Njau.

Akimsomea mashitaka yake mahakamani hapo, Mwendesha Mashitaka wa Serikali, Njau alidai kuwa Agosti 20, Mbunge huyo alimtumia ujumbe mfupi wa maneno Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo akitumia namba 0764150747 kwenda namba 0766 757575 ya Mkuu huyo.

Ujumbe huo kwa mujibu wa mashitaka ulikuwa ukisomeka: “Karibu tutakudhibiti kama mashoga wanavyodhibitiwa Uarabuni".

Katika mashitaka ya pili, Njau alidai kuwa Lema alitumia mtandao wa WhatsApp kushawishi wananchi wa Arusha kuandamana  Septemba mosi.

Baada ya kusomewa mashitaka hayo, Lema alikana   ndipo mwendesha mashitaka wa Serikali akaiomba Mahakama imnyime dhamana kwa sababu kuna taarifa za kiintelijensia kuwa akipewa usalama wake utakuwa shakani.

Hata hivyo hoja hiyo ilipingwa na wakili wa utetezi, John Mallya ambaye alimwomba Hakimu Kamugisha kumpa dhamana Lema, kwa sababu kosa lake linaruhusu dhamana na pia ni mbunge hivyo taarifa za kiitelijensia hazina uzito na kama zipo zinapaswa kutajwa mahakamani ili imnyime dhamana.

"Tunaomba pingamizi hili la dhamana litupiliwe mbali maana hakuna ushahidi wa maandishi wala kutamkwa mahakamani hapa, kama Lema akipewa dhamana anaweza kuhatarisha usalama wake, tunaomba apewe dhamana,” Wakili Mallya aliomba.

Baada ya mabishano hayo, Hakimu Kamugisha alitupilia mbali pingamizi la mwanasheria wa Serikali, na badala yake alitoa masharti ya dhamana kwa mbunge huyo, ambaye alipaswa kuwa na wadhamini wawili watakaosaini hati ya Sh milioni 10, kila mmoja kwa kiasi hicho hicho na pia mbunge huyo asiruhusiwe kutoka nje ya nchi bila ruhusa ya Mahakama na kutakiwa kusalimisha hati yake ya kusafiria mahakamani hapo.

Baada ya masharti kutolewa wadhamini wawili walijitokeza ambao ni madiwani jijini hapa, lakini karatasi zao zilionekana kuwa na kasoro baada ya mwanasheria wa Serikali kuzikagua hasa majina.

“Hati za wadhamini zina kasoro katika majina kwenye vitambulisho vilivyowasilishwa mahakamani hapa vinaonesha majina matatu lakini barua zinaonesha majina mawili, la mwanzo na la mwisho hivyo naiomba Mahakama isipokee barua hizi,” aliomba.

Kutokana na sintofahamu hiyo, Hakimu Kamugisha alikubaliana na hoja ya Wakili Njau na kumtaka Lema atafute wadhamini wengine na kuahirisha kesi hiyo hadi  Septemba 19.

Katika mashitaka ya pili ya kuhamasiaha maandamano Agosti mosi hadi 26 alikana pia na Mallya kuomba   dhamana ambapo  wakili wa Serikali  hakuwa na pingamizi huku akiondoa hoja yake ya awali aliyoitumia kupinga dhamana ya Lema.

Kwa mara nyingine Hakimu Kamugisha alitoa masharti   kwa mbunge huyo kuwa na wadhamini wawili   watakaosaini bondi ya Sh milioni 15 kila mmoja  na kuahirisha kesi hiyo hadi Septemba 13  huku akitoa amri kwa wadhamini kushughulikia kasoro ya awali kabla ya muda wa Mahakama kumalizika. 

Baada ya kesi hizo kuahirishwa Lema alipelekwa   mahabusu kwa muda ili kusubiri wadhamini wake kurekebisha kasoro zilizojitokeza.

Saa 8:20 mchana, polisi walimtoa mahabusu na kutaka kumpandisha kwenye karandinga kwa ajili ya kumpeleka mahabusu ya Kisongo.

Hata hivyo, yaliibuka mabishano kati ya Lema na askari hao na mawakili Mallya na James Lyatuu ambao kwa pamoja walihoji, mbunge huyo anakopelekwa wakati akisubiri kurekebishwa kwa hati ya dhamana na muda wa Mahakama ulikuwa bado haujamalizika.

“Muda wa mahakama haujafika mnanipeleka wapi nasema, nitafia hapa mahakamani saa hizi ni saa 8 muda wa Mahakama haujaisha mnanipeleka wapi siendi mniue, siendi popote mniue hapa hapa,  mnanipeleka wapi na kwa nini mnanifanyia hivi nasema siendi kokote bora kufa sikubali," alisikika Lema akipaza sauti.

Lema ambaye alionekana kudhoofu kutokana na kugoma kula kwa siku nne, aliweza kuwakimbia askari hao na   kuingia ndani ya vyumba vya Mahakama  hali iliyofanya polisi kupambana naye hata akaanguka chini kwa muda huku polisi wakimzingira na ndugu, jamaa na marafiki   wakishuhudia tukio hilo.

Baada ya muda huku tafrani hiyo ikiendelea, wadhamini wake Isaya Doita, Paulo Matsei, Sabina Francis na  Naibu Meya wa Jiji la Arusha, Viola Lekindikoki walijitokeza na kufanikiwa kumdhamini   na kuondolewa mahakamani hapo akiwa amebebwa kwa kukosa nguvu huku akipanda gari aina ya Toyota Harrier na kukimbizwa hospitali ya Aga Khan kwa  matibabu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo