*Watuhumiwa kufanya mkutano wa ndani
*Wamo pia Mashinji, Mnyika na Said Issa
Suleiman Msuya
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es
Salaam limewakamata na kuwaweka mahabusu na kuwahoji viongozi waandamizi wa Chadema
kwa madai ya kufanya mkutano wa ndani bila
kibali.
Taarifa zilizolifikia JAMBO LEO jana zilieleza
kuwa viongozi waliokamatwa baada ya mkutano wa Kamati Kuu ya Chama hicho na
kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kwa mahojiano
ni Mwenyekiti wa Chama hicho, Freeman Mbowe, Mjumbe wa Kamati Kuu, Edward
Lowassa, Katibu Mkuu, Vincent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu Bara, John Mnyika na
Makamu Mwenyekiti, Said Issa Mohammed.
Habari zaidi zilieleza kuwa viongozi hao
walifanya vikao vya kawaida vya Kamati ya Kuu ili kujadili masuala ya chama ikiwamo
mipango ya Operesheni ya Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
“Baada
ya mkutano wa Kamati Kuu, ulianza mkutano wa wajumbe takriban 178 na ulipoanza
kujadili Ukuta, polisi walivamia na kukamata viongozi wetu,” alisema mmoja wa
wabunge aliyekuwa kwenye mkutano huo.
Taarifa
zaidi zilionesha kuwa viongozi hao walikamatwa saa 8 mchana na kufikishwa Polisi
saa 10:30 jioni.
Akizungumza
na wanahabari baada ya kufikishwa Polisi, huku Mbowe, Lowassa, Mashinji na
Mnyika wakiwa ndani kwa mahojiano, Mwanasheria wa Chama hicho, Tundu Lissu
alisema:
“Kamati
Kuu ilianza mkutano saa 6 mchana na ikamaliza, wakati mkutano unaoshirikisha
wote ulipoanza, ndipo walikuja askari wanane
waliovalia kiraia na kuwakamata.”
Hata
hivyo, Lissu alisisitiza kwamba mbali na hatua hiyo ya Polisi, Chadema
haitarudi nyuma huku akieleza kuwa Operesheni Ukuta iko pale pale.
“Hatutafanya
kazi kwa maagizo ya mtu bali kwa kufuata sheria na Katiba ya nchi,” alisema
Lissu.
Gazeti
hili lilishuhudia viongozi mbalimbali na mashabiki wa Chadema wakijikusanya kwa
vikundi katika viunga vya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam na ofisi za
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jirani na kituo hicho, wakifuatilia kukamatwa
kwa viongozi wao.
0 comments:
Post a Comment