Abraham Ntambara na Hussein Ndubikile
CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi ya Abiria (Taboa), kimeibua
hoja mpya ya kupinga Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu
nchini (Sumatra), kufungia kampuni za mabasi, pale moja ya mabasi yanapopata
ajali, wakati wakijiandaa na mgomo wa mabasi nchi nzima.
Kabla ya hoja hiyo mpya, Taboa walikuwa wakipinga
kutangazwa kwa siku moja ya ukaguzi wa magari nchi nzima, wakidai watalazimika
kusitisha huduma mpaka ukaguzi wa mabasi yote utakapokamilika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa Taboa,
Enea Mrutu aliyesisitiza nia ya kugoma kesho kutwa bado ipo, alipinga Sumatra kufungia
kampuni za mabasi kufanya safari zake, mara baada ya kutokea ajali ya basi moja.
“Kama gari moja linapata ajali halafu wanafungia kampuni
nzima, wao ndiyo walianza kuvunja sheria kwa sababu sheria inasema unatakiwa
kufungia gari moja tu lililopata ajali,” alidai Mrutu.
Mrutu alisisitiza kuwa kugoma au kutokugoma siku hiyo ya
Jumatatu, itategemeana na maridhiano yatakayofikiwa katika kikao cha leo,
kitakachofanyika Wizara ya Ujenzi, Mawasialiano na Uchukuzi kikiwakutanisha
wao, Sumatra na Kikosi cha Usalama Barabarani.
Aliitahadharisha Serikali kuwa wasiwasikilize baadhi ya
madereva ambao wamekuwa wakiwapigia simu na kusema kuwa Taboa hawawezi kufanya
mgomo.
“Hao madereva wasiwasikilize, wao tumewaajiri tu na sisi
ndio wenye umiliki wa magari na tunaweza kufanya hivyo ila tunaiheshimu tu Serikali,”alisema.
Aliongeza kuwa umefika wakati Serikali isimamie na kufuata
sheria zilizotungwa na Bunge badala ya kusimamia sheria zinazotoka vichwani
mwao.
Wakati Mrutu akisema hayo, Mkurugenzi wa Sumatra,
Gilliard Ngewe alisisitiza kuwa sheria za leseni za usafirishaji, zinaipa nguvu
mamlaka hiyo kuifungia kampuni bila kujali kuwa ajali imesababishwa na dereva
au ubovu wa magari.
“Sheria za leseni za usafirishaji zilizopo zinatupa
mamalaka hasa tatizo linapogundulika madereva wasio na sifa wamechangia ajali
za mabasi ya waajiri wao,“ alisema.
Alisema endapo itabainika kampuni imeaajiri madereva
wasiotakiwa, Sumatra hutoa muda kwa kampuni kuwafanyia mafunzo na usaili tena
ndipo yafunguliwe.
Alisisitiza pia Sumatra pia hufungia kampuni za mabasi
itakapogundulika kuwa kampuni yenye mabasi zaidi ya sita, imeajiri meneja asiye
na vigezo vya kufanya kazi hiyo.
Aliwaagiza wamiliki wote wa mabasi ya masafa marefu,
kuzingatia masharti ya leseni ya usafirishaji kwa kuendelea kutoa huduma hiyo
hadi utaratibu mwingine wa ukaguzi wa magari hayo utakapotolewa.
Ngewe alisema Sumatra iko katika mchakato na Jeshi la
Polisi wa kuweka utaratibu mzuri wa kutekeleza ukaguzi wa mabasi, ambao awali
ulipangwa kufanyika Jumatatu kabla ya kuibuka kwa tishio hilo la mgomo.
Aliwataka wananchi kuondoa hofu ya habari zinazosambazwa
na vyombo vya habari ya kuwepo kwa mgomo wa mabasi Agosti 22 mwaka huu, na
kufafanua kuwa mamlaka hiyo inafuatilia jambo hilo kuhakikisha huduma ya
usafiri inakuwepo wakati wote.
Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama
Barabarani, Mohamed Mpinga, ameionya Taboa kuwa wakigoma watakuwa wemeenda
kinyume na sheria ya leseni waliyopewa na Sumatra.
“Wakigoma watakuwa wanaenda kinyume na watapatwa na
madhara makubwa… sitarajii kama watafanya hivyo,”alisema Mpinga alipozungumza
katika mahojiano na kituo kimoja cha redio jana Dar es Salaam.
0 comments:
Post a Comment