Serikali itapongezwa ikiokoa watoto mazingira hatarishi


Magendela Hamisi
KWA muda mrefu kumekuwa na changamoto ya ongezeko kubwa la watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi huku baadhi yao wakilelewa katika vituo maalumu.

Baada ya kubainika idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika mazingira hayo, katika mikoa mbalimbali hapa nchini hususan maeneo ya mijini kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kulitafutia ufumbuzi suala hilo.

Dar es Salaam ni moja ya majiji hapa nchini ambalo limekuwa likiweka mikakati mara kadhaa ya kuwaondoa watoto hao. Hata hivyo hakuna matunda ya mikakati hiyo baada ya watoto hao kuendelea kuongozeka badala ya kupungua.

Hakuna sababu za moja kwa moja zinazobainishwa kuwa zinachangia ugumu wa kudhibiti watoto hao kwenda mijini na kubaki huko, licha ya kuwa wengi wanasema hakuna mipango madhubuti ya kukomesha tatizo hilo.

Zipo baadhi ya sababu zinazojulikana kuwa ndizo chanzo cha baadhi ya watoto kukimbia katika familia zao na kwenda kuishi katika mazingira hatarishi ambazo ni pamoja na ugomvi baina ya baba na mama ambapo mwisho wa siku wanalazimika kutengana na hivyo watoto hao kukosa uangalizi.

Hata hivyo, baadhi yao watoto wamekuwa wakijiingiza katika vitendo vya uhalifu inayosababisha Serikali kutumia nguvu kubwa kudhibiti uhalifu unaojitokeza kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa mingine.

Mfano siku chache zilizopita mmoja wa viongozi wa Jeshi la Polisi nchini alinukuliwa na vyombo vya habari akibainisha kuwa moja ya sababu za kuwepo vitendo vya uhalifu hususan ‘panya road’ ni baadhi ya watoto wa mitaani ambao wamekuwa wakijiingiza katika makundi hayo.

Hivyo, kutokana na jitihada nyingi kukwama za kuwaondoa au kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, jana Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kwa sasa serikali inajipanga kuhakikisha wanafanya mchakato wa kuanza kuwachukua ili kuwapeleka katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Binafsi napongeza mchakato huo kwa maana utasaidia kupunguza watoto wanaoishi mazingira hayo magumu kuzagaa mitaani ambao wengine wanaishia kutumbukia katika kujiunga na makundi ya uhalifu jambo ambalo linakuwa na hasara kwa familia na Serikali kwa ujumla. Pia utasaidia kuhakikisha vijana hao wanaweza kujiajiri kutokana na mafunzo watakayopata hususan ya ujasiriamali watakayopata wakiwa katika mafunzo ya JKT ikiwemo kilimo, ufugaji kuku na ufundi wa aina mbalimbali utakaosaidia kuwaweka kando na vitendo viovu.

Wakati mwingine hata kama watashindwa kujiajiri wenyewe wanaweza kuajiriwa katika kampuni mbalimbali za ulinzi jambo ambalo litasaidia wao kuishi vizuri pamoja na kutunza ndugu zao.

Kutokana na kuwepo kwa mkakati huo wa kuwaingiza JKT, watoto wanaoishi katika mazingira magumu kuanzia wenye umri wa miaka 18 ni vema ukafanywa kwa umakini ili kuhakikisha kuwa wanaopata nafasi hiyo ni wale wenye sifa kwa maana upo uwezekano wa baadhi ya wahusika wa kusaili watoto hao kutumia nafasi hiyo kuwaingiza wasio wahusika.

Natoa tahadhari hiyo kwa kuwa vijana wengi wanahitaji nafasi za kujiunga na JKT kwa kuwa wanaamini ni moja ya sehemu ya njia sahihi ya kujiunga na majeshi mengine ya ulinzi na usalama jambo litakalosaidia kuwahakikishia ajira Serikalini.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo