Tetemeko latikisa tena Kagera

WAKAZI wa Mkoa wa Kagera bado wanaishi kwa hofu kubwa kutokana na tetemeko la ardhi kutikisa tena jana usiku, mkoa huo na kusababisha wakimbie nyumba zao.

Hali hiyo, ilitokea siku moja baada ya tetemeko lenye ukubwa wa 5.7 kutikisa ardhi na kusababisha vifo vya watu 17 na kujeruhi wengine 253.

Wakizungumza na gazeti hili jana kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti, baadhi ya wananchi hao walisema wakati tetemeko likitokea jana usiku, walihofia maisha yao wakikumbuka madhara yaliyotokea Jumamosi kutokana na tetemeko la ardhi lililodumu dakika 15.

Walidai kuwa baada ya kusikia ardhi ikitikisika na kutetemeka jana usiku wa saa 4:19 wakiwa tayari wengine wamelala wali-kumbwa na kihoro cha kupoteza maisha kwa kuwa ilikuwa mara yao ya kwanza kushuhudia hali hiyo.

Walisema tofauti na Jumamosi ambapo tetemeko hilo lilikumba watu wengi wakiwa kwenye kumbi za starehe saa 9:27 alasiri hali ilikuwa ni tofauti.

“Haijapata kutokea mkoani kwenu na katika maisha yangu. Usiku nikiwa nimelala nilisikia kelele za watu wakilia ‘tunakufa, tunakufa’, nikatoka nje huku ardhi ikitikisika na kusababisha nyumba na baadhi ya vyombo kuparaganyika. Nilishikwa na hofu sikulala tena,” alisema mkazi wa Kibeta.

Aidha, Maige Ngadala alisema Jumamosi walinusurika kufa kutokana na tetemeko, lakini usiku wa kuamkia jana lilipita saa 4 usiku na baadaye saa 11 alfajiri.

“Kwa kweli nilijisikia vibaya na kujiuliza tumemkosea nini Mungu. Tetemeko kupita mara tatu eneo hilo hilo moja na ni maajabu na sijapata kuona. La kwanza limetuachia vilio na majonzi kwa kupoteza ndugu zetu, mali na nyumba hata pa kulala hatuna,” alisema Ngadala.

Mjane ambaye alifiwa na mumewe mwezi jana, Renatia Christopher alisema alipata pigo kubwa kutokana na nyumba aliyokuwa akiishi kuanguka kutokana na tetemeko la Jumamosi.

Alisema nyumba hiyo ndiyo imekuwa ikimsaidia kupata kipato cha kuendesha familia ya watoto watano lakini sasa hajui pa kuanzia.

“Sijui nilichomkosea Mungu mimi, mwezi jana tu nilipoteza mume wangu, leo nyumba mbili zote zimeondoka na sina msaada mwingine wala njia ya kuendesha maisha yangu unavyoniona,” alisema kwa majonzi mjane huyo.

“Ilikuwa kama muujiza siku ya tetemeko, ni jambo ambalo sikutahajia linitokee maishani mwangu, kwani nimekuwa nikisikia kwenye vyombo vya habari tu tetemeko limetokea nchi fulani hasa Japan na limeua watu kadhaa. Nilihisi ndio mwisho wa maisha yangu wakati linatokea,” alisema Rweyemamu mkazi wa Mukishenyi.

Askari Magereza ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema tetemeko kwake ni kitu cha kawaida, lakini siku linatokea juzi alishindwa namna ya kufanya na kujikuta akibaki amesimama kwenye ukumbi wa Bwalo la Polisi.

“Matetemeko nilishayazoea Mbeya ambako nilipata kuishi kwa kuwa yanapita kila mara, lakini hili la juzi hapa Bukoba ni ki-boko. Siku hiyo nilikuwa naangalia mpira kantini Polisi nilishituka kuona watu wanakimbia ovyo na kujikuta wanakwama mlangoni. Nilibaki nimesimama ukumbini nikisubiri lolote litokee,” alisema skari huyo.

Malalamiko

Kutokana na madhara yaliyotokea ambapo maeneo ya Hamugembe, Nshambya na Kibeta yanayodaiwa kuathirika zaidi wa-nanchi waliilalamikia Serikali kwa kushindwa kuwasaidia hata mahema ili waishi kwa muda wakati wakijipanga upya.

Walidai kuwa tangu nyumba zao zianguke hawana mahali pa kuishi bali nje ya nyumba zilizobomoka na zingine kuanguka na hivyo kutishia uhai wa maisha yao.

Walisema licha ya ujio wa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bado hakuna msaada ambao Serikali iliwapa kunusuru afya za watoto kwa sababu wanalazimika kulala nje wakati huu ambao mvua zimeanza kunyesha.

Mkuu wa Mkoa, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu akizungumza na gazeti hili kwa simu kuhusu hatua zilizochukuliwa, alisema Kamati ya maafa ya mkoa ikishirikiana na ofisi ya Waziri Mkuu inapita kwenye maeneo yaliyoathirika kupata idadi kamili ya waathirika na nyumba zilizoanguka ama kupata nyufa ndipo watoe mahitaji yao.

“Kamati mbili za ofisi ya Waziri Mkuu na ya mkoa zinapita kufanya tathmini kwenye maaneo yenye athari, ili tujue idadi ya waathirika na idadi ya nyumba ndipo tuombe mahitaji ya vifaa kama mabati, saruji na mahema kutoka kwa wadau,” alisema Kijuu.

Pia alikiri kuwa saa 4:19 usiku kulitokea tena tetemeko lakini halikuwa na madhara kwa binadamu ambapo alisema dawa kwa ajili ya majeruhi zipo za kutosha na hakuna upungufu.

Meja Jenerali Kijuu alisema mbali na vifo 17 vilivyotokana na tetemeko, Mutukula wilayani Mishenye vilitokea vifo viwili baada ya kupigwa na radi saa 5 asubuhi ambapo majeruhi waliobaki hospitalini ni 61 na wengine 109 waliruhusiwa baada ya hali zao kuimarika.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo