…Ukuta wahamishiwa ng’ambo


Emeresiana Athanas

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeahirisha maandamano na mikutano ya hadhara isiyokoma ya Operesheni Ukuta iliyokuwa ianze leo na kutaja mbinu mpya ya kuendeleza operesheni hiyo ikiwamo kuishtaki Serikali nchi za nje.

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati akitoa taarifa ya Kamati Maalumu ya Kamati Kuu ya Chama hicho ya kusitisha oparesheni hiyo, Mwenyekiti Freeman Mbowe alisema uamuzi huo umefikiwa kutokana na tathmini ya mambo kadhaa yaliyofanywa na Kamati.

Kutokana na tathmini hiyo, alisema Kamati imeona hakuna umuhimu wa kuendelea na maandamano na mikutano nchi nzima iliyotarajiwa kuanza leo, ili kupisha mbinu nyingine za kuendeleza fikra za kuendeleza Ukuta.

“Ukuta si tukio la siku moja la kuandamana au kufanya mikutano kwa siku moja, bali ni kujenga fikra za Watanzania katika kupinga wanachoamini ni utawala wa kiimla na kidikteta unaojengeka nchini,” alisema.

Ziara
Alitaja mbinu mpya za kuendeleza harakati za Ukuta za kudai haki na demokrasia, kuwa ni kufanyika ziara ya wiki moja ya ujumbe wa chama hicho, ukiongozwa na Katibu Mkuu, Dk Vincent Mashinji, Ujerumani na Denmark.

Kwa mujibu wa Mbowe, ziara hiyo imelenga kueleza serikali za nchi hizo hali halisi ya kisiasa nchini, ili kujenga shinikizo la kidemokrasia dhidi ya utawala wa kidikteta wa Serikali, kwani chama hicho kinatambua umuhimu wa diplomasia na uhusiano wa kimataifa kama sehemu muhimu ya kudai haki na demokrasia duniani.

Mwenyekiti alisema mbali na ziara hiyo yenye mafanikio katika chama hicho, ziara zingine zitafanyika katika mataifa rafiki wa Tanzania ya Umoja wa Ulaya (EU), nchi za Scandinavia, Uingereza, Marekani na Kanada.

“Viongozi hao watapata fursa ya kuielezea dunia kuhusu ukiukwaji mkubwa wa demokrasia na haki za Watanzania, Taifa letu limekuwa na tabia ya kujipambanua kama Taifa la amani, lakini limekuwa likitesa watu huku dunia ikiwa haijui,” alisema.

Mbinu zingine
Alisema chama hicho kitafanya mbinu na juhudi za kidemokrasia kwenye mataifa mengine, ili Serikali itambue kuwa chama hicho hakiishii Tunduma, kwani kina uwezo mkubwa wa kwenda nchi mbalimbali kuzungumza na kueleweka.

Alitaja nyingine kuwa ni maandalizi ya kufungua mashauri mahakamani kupinga hatua za kukandamiza demokrasia, haki za binadamu na ukiukwaji wa Katiba na sheria za nchi, ambazo zinafanywa na Serikali.

Alitaja mbinu nyingine kuwa ni ziara katika kanda na mikoa ya kichama, ili kuendeleza harakati za Ukuta kwa kujenga na kuimarisha uhai wa chama na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

“Hivyo mikutano na maandamano ya hadhara iliyotakiwa kufanyika kesho (leo) haitafanyika hadi tarehe na siku itakayopangwa,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo