Watanzania wengi sasa kuonja ndege



* Serikali yapania kutangaza nauli nafuu
* Ndege mpya kutua karibu viwanja vyote

Sharifa Marira

WATANZANIA wengi wanatarajiwa kuanza kunufaika na usafiri wa anga, kutokana na unafuu wa huduma hiyo utakaowezeshwa na ndege mpya za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Akizindua jana Dar es Salaam, ndege hizo aina ya Bombardier Q 400, Rais John Magufuli mbali na kutaja madhambi ya Shirika hilo, alielezea unafuu wa ndege hizo mpya, unaotarajiwa kuonekana mpaka kwa wateja.

Akitolea mfano wa safari ya kutoka Dar es Slaam kwenda Mwanza, Rais Magufuli alisema gharama ya mafuta ya kurusha Bombardier Q ni Sh milioni moja wakati ndege zingine ikiwemo Boeing, gharama ni Sh milioni 28.9.

Kutokana na gharama kubwa ya kurusha ndege zinazotumika katika usafiri wa anga kwa sasa kabla ya ujio wa Bombardier Q, Rais Magufuli alisema nauli ya usafiri kati ya Dar es Salaam na Mwanza, ilifikia Sh 800,000.

Alifafanua kuwa kutokana na ujio wa Bombardier Q mbili, moja ya mashirika yaliyokuwa yakitoa huduma hiyo nchini, limeamua kupunguza wafanyakazi, baada ya kupata habari ya ujio wa ndege nafuu. Kuhusu kasi ya Bombardier Q, ikilinganishwa na ndege zingine ambazo zimekuwa zikitoa huduma hiyo nchini, Rais Magufuli huku akitumia mfano wa Dar es Salaam- Mwanza, alisema tofauti ni dakika 20 tu.

“Dakika 20 ni nini katika unafuu wa usafiri?” Alihoji Rais Magufuli, huku akisisitiza kuwa ndege hizo hazijaandikwa CCM, hivyo ni za Watanzania wote na kila mmoja, akiwemo Mbowe (Freeman- Mwenyekiti wa Chadema) na Lipumba (Profesa Ibrahim-aliyekuwa Mwenyekiti wa CUF), watapanda.

Ndege hizo ambazo zina uwezo wa kutua katika viwanja ambavyo havina lami zitaanza na safari za Kilimanjaro, Arusha, Zanzibar, Mwanza, Dodoma, Tabora, Bukoba, Comoro, Dar es Salaam na Kigoma.

Madudu ATCL

Mbali na umuhimu wa unafuu wa ndege hizo, Rais Magufuli alitaja madudu ya ATCL na mengine yanayofanywa nje ya Shirika hilo, huku akitamani urais uwe wa miaka miwili ili ampe mtu mwingine, kwa kuwa kazi hiyo ni ngumu na inamkosesha usingizi.

Rais Magufuli alitaja mambo yaliyomkera ATCL kuwa ni pamoja na kutengenezwa kwa hasara kubwa ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa mafuta hewa, kupoteza zaidi ya Sh milioni 700 bila wahusika kuchukuliwa hatua.

Alisema kampuni hiyo ilipata kukagua ndege iliyokuwa inakwenda Tabora lakini ikagundua kuwa tairi ni bovu, lakini kutokana na ‘upigaji’ walilazimisha safari na ilipofika Tabora tairi lilipasuka wakaamua kukodi ndege nyingine kwa dola 6,000 (Sh milioni 12) za Marekani.

Alisema viongozi na wakurugenzi walikuwa wanajilipa Sh 50,000 kwa ajili ya kutembelea uwanja wa ndege, hivyo walikuwa wanatumia nafasi hiyo kurudia kutembelea zaidi ya mara tatu na kujilipa posho za muda wa ziada.

Alisema ATCL ilikosa wafanyakazi wenye uamuzi na kujituma, huku akivitaja vituo vilivyokithiri uozo huo kuwa ni Comoro, Mwanza, Mtwara na Dar es Slaam.

Alisema kulikuwa na wafanyakazi pandikizi wa mashirika shindani, tiketi za watoto zilitumika kwa watu wazima na kukatisha tiketi kupitia mawakala, ili baadaye wawalipe asilimia ambazo waligawana.

“ATCL ilikithiri kwa kutofuata ratiba unaweza ukaambiwa ndege inaondoka leo lakini ikaondoka jioni au kesho au hata wiki, hivyo abiria walikata tamaa na kuona ubabaishaji ambao hauwasaidii.

“Kulikuwa na mafuta hewa, ndege ilikuwa inaonekana kuwa iko Mwanza kumbe iko hapa hapa na imejazwa mafuta, wakubwa waliamua ‘kupiga dili’ walikuwa wanasema ndege imejaa ili tiketi ziuzwe kwenye mashirika mengine … ambao hawafai toeni nje,” aliagiza.

Alisema Sh milioni 700 zilipotea kituo cha Comoro, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa na mhusika aliyepoteza fedha ambaye alitakiwa kustaafu Februari mwaka huu, aliongezwa muda ili aendelee kupoteza.

“Haiwezekani tununue ndege kwa gharama kubwa halafu watu watumie kwa manufaa yao, ndege inakwenda na abiria watatu, wanne kumbe inakwenda kufanya ununuzi wa mtu, nayajua yote,” alisema.

Utumbuaji

Alimtaka Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa na Bodi ‘kutumbua’ bila kuwaonea huruma wafanyakazi wabovu.

Alisema aliondoa wafanyakazi wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) zaidi ya 500 hivyo hawezi kushindwa kuondoa wafanyakazi 200 huku kukiwa na vijana wengi wanaotafuta ajira.

Wake wa viongozi

Rais Magufuli alisema wapo viongozi wakiwamo mawaziri ambao wake zao wanafanya kazi katika Shirika hilo ambalo lilikuwa linaizalishia Serikali hasara.

“Wapo wake za viongozi, sisi wenyewe tumekuwa na tabia ya kuwekana, wewe kama ni Waziri kwa nini mkeo aendelee kukaa katika Shirika ambalo halizalishi?” Alihoji.

Ndege zingine

Alisema Serikali inajipanga kununua ndege zingine mbili ambazo moja itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 160 na nyingine abiria 240 na tayari fedha za kununulia zipo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo