Katibu Mkuu UN apokea tamko la akina Seif


KATIBU Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, amepokea Tamko la maandishi kutoka kwa muungano wa vyama vya Umoja wa Kiliberari (Liberal International - LI) kuhusu mkwamo wa kisiasa visiwani Zanzibar uliotokea baada ya uchaguzi wa Oktoba 25 mwaka jana na wa Machi 20.

Tamko hilo limebeba ujumbe wa mwito wa kuheshimiwa kwa haki za binadamu, kurejeshwa kwa demokrasia na utawala wa kisheria Zanzibar na Tanzania kwa jumla, huku Chama cha Wananchi (CUF), kikieleza kulipokea kwa mikono miwili kwa imani kuwahaki itatendeka.

Hatua hiyo ya LI kuandikia UNHRC imekuja wiki kadhaa baada ya Maalim Seif kukutana na taasisi za kimataifa zinazoshughulikia maendeleo ya demokrasia na utawala bora na wakuu wa serikali za Marekani, Ulaya na Canada.

Maalim Seif alifuatana na baadhi ya wasaidizi wake na alifika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kimaita (ICC) iliyoko The Hague, Uholanzi, ambako aliwasilisha malalamiko ya uvunjaji wa haki za binadamu unaofanywa Zanzibar kwa alichosema ni idhini ya viongozi wa CCM.

Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa LI, Robert Woodthorpe, Ban alipokea tamko hilo na kuliwasilisha katika kikao cha 33 cha Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC) kinachoendelea New York, Marekani.

Woodthorpe alinukuliwa na Sauti ya Ujerumani (Deustchewelle) jana akisema suala hilo liliwasilishwa katika ajenda namba tatu ya UNHRC, iliyokuwa ikijadili mambo mbalimbali lengo likiwa ni kuitaka Tanzania na Zanzibar kushimu haki za binadamu na demokrasia.

“Tumeandika taarifa na tumeiwasilisha kwenye mkutano wa 33 wa UNHRC ambapo LI inataarifu taasisi za kimataifa, kuongeza msukumo kwa Serikali ya Tanzania kuacha uvunjifu wa haki za binadamu, kuzuia shughuli za kisiasa na haki zingine kwa wananchi wa Zanzibar,” alisema.

Alisema tamko lao limebainisha uwepo wa uvunjifu wa haki za binadamu hasa kwa upande wa upinzani, ukiwamo ukiukwaji wa demokrasia baada ya uchaguzi wa Oktoba 25.

Woodthorpe alisema mgombea urais wa Zanzibar kupitia CUF, Maalim Seif alipeleka taarifa ya kilichotokea katika uchaguzi huo makao makuu ya IL na baada ya kupitia walijiridhisha hivyo kupeleka UN.

Alisema katika tamko hilo wametoa mapendekezo ambayo yanaweza kusaidia Wazanzibari kujiona sehemu ya watu wenye kuishi katika misingi ya uhuru. Alisema waliiomba UNHRC kuweka vikwazo vya kisiasa, mali na zuio la kusafiri kwa baadhi ya viongozi kutokana na ukiukwaji huo wa haki za binadamu na uvunjifu wa demokrasia.

Taasisi hiyo ambayo CUF ni mwanachama wake, ilitoa mwito kwa wabunge wanaofuata mtazamo wa kiliberali upande wa serikali na upinzanikatika mataifa yote duniani, kuchukua msimamo imara kupitia mabunge ya nchi zao na kutoa matamko ya kupinga walichokiita uonevu wanaofanyiwa viongozi wa upinzani Zanzibar na wafuasi wao.

Ofisa Habari wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Alli Kondo alisema kimsingi hawajapata taarifa rasmi kuhusu suala hilo na kueleza kuwa wanawasiliana na ubalozi wa Tanzania nchini Marekani ili kupata taarifa. “Nimewasiliana na idara husika wanasema bado hawajapata taarifa kuhusu suala hilo, ila wanawasiliana na ubalozi wa Marekani ili kujua nini kinaendelea na wataeleza,” alisema.

Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka alisema chama kilichotajwa kusababisha hali hiyo kutokea, hakina taarifa yoyote na watatoa taarifa iwapo watahitajika.  Sendeka alisema CCM inaamini Uchaguzi Mkuu Zanzibar ulishamalizika na kwamba yanayosemwa sasa hawawezi kuyazungumzia.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo