Vigogo Kagera watumbuliwa kwa ‘kulamba’ fedha za maafa


Fidelis Butahe

KUFA kufaana. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda kutumia maafa ya tetemeko la ardhi mkoani humo kujinufaisha binafsi.

Badala ya misaada kufikia wananchi wanaosota, huku baadhi wakikosa mahala pa kuishi imefikia mikononi mwa viongozi hao wawili.

Wateule hao wa Rais John Magufuli ambao hivi karibuni walikula kiapo cha uadilifu wa utumishi wa umma katika hafla iliyofanyika Ikulu, wamebainika kufungua akaunti zingine za benki kwa kutumia jina linalofanana na akaunti rasmi ya kuchangia maafa iitwayo ‘Kamati Maafa Kagera’, kwa lengo la kujipatia fedha.

Hata hivyo, ulaji huo waliojitengenezea umewatokea puani, baada ya Rais kutengua uteuzi wao na kuviagiza vyombo vya Dola kuwachukulia hatua za wote waliohusika katika njama za kufungua akaunti hiyo.

Kama hiyo haitoshi, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhasibu Mkuu wa Mkoa huo, Simbaufoo Swai kutokana na kuhusika na njama hizo.

Akaunti hiyo ya maafa ilifunguliwa kuwezesha watu wa kada mbalimbali kuchangia maelfu ya wananchi waliokosa makazi baada ya nyumba 840 kuanguka na nyingine 1,264 kupata nyufa yakiwamo majengo 44 ya taasisi za umma. Tetemeko hilo lilitokea Septemba 10 na kusababisha vifo vya watu 17.

Uamuzi wa Rais ulitolewa jana na Majaliwa muda mfupi baada ya kupokea hundi ya msaada wa Sh milioni 545 kutoka kwa Waziri Mkuu wa India, Narendra Modi ambayo iliwasilishwa kwa niaba yake na balozi wa nchi hiyo nchini, Sandeep Arya kwa ajili ya waliokumbwa na maafa hayo.

“Natoa mwito kwa wananchi na taasisi kuendelea kuchangia misaada kwa walioathirika kwa kutumia akaunti rasmi ya ‘Kamati Maafa Kagera’, ambayo imetangazwa na Serikali,” alisema Majaliwa.

Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, haikuweka wazi kiasi ambacho wateule hao wa Rais walichota kupitia akaunti hiyo bandia, wala muda walioifungua, baada ya Serikali kutangaza akaunti yake rasmi.

Sakata hilo liliibuka huku baadhi ya wananchi wa Bukoba wakisota na kulalamika kukosa baadhi ya mahitaji muhimu huku Serikali ikihaha kusaka misaada kila kona kwa kupokea michango kutoka kwa mashirika, taasisi, viongozi na watu mbalimbali.

Awali, katika makabidhiano ya hundi hiyo, Arya alisema Waziri Mkuu wa India alisema Serikali na wananchi wa nchi hiyo walipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kutokea kwa maafa hayo yaliyosababisha vifo vya watu na uharibifu wa mali.

Rais Magufuli alimshukuru Waziri Mkuu huyo na Serikali yake kwa kutoa mchango huo na kwamba aliguswa na moyo wa upendo walioonesha.

“Balozi Sandeep Arya naomba unifikishie shukrani zangu za dhati kwa Waziri Mkuu, mwambie kwa niaba ya Serikali yangu tunamshukuru sana kwa kutoa msaada huu muhimu kwa ajili ya Watanzania wenzetu waliopatwa na maafa Kagera,” alisema Rais.

“Tumefarijika kwamba marafiki zetu mmeguswa kwa namna ya kipekee na tatizo lililoipata nchi yetu.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo