Polisi sasa yaruhusu mikutano ya ndani



VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vimesema kauli ya Jeshi la Polisi kuondoa marufuku ya mikutano ya ndani kwa vyama vya siasa si ya kupongeza kwa kuwa hatua hiyo ilikuwa kinyume na Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa.

Ukawa imesema kauli hiyo imetolewa na polisi kwa aibu waliyoipata kutokana na CCM kuendelea kufanya mikutano ya ndani na nje bila kuzuiwa, huku wapinzani wakiminywa na viongozi wake kukamatwa na kuhojiwa bila sababu za msingi.

Kauli hiyo ya Ukawa inafuatia ile ya Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani kutangaza kuruhusu mikitano ya ndani ya vyama, huku akisisitiza maandamano na mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa bado imezuiwa isipokuwa kwa wabunge katika majimbo yao.

Kamishna huyo amevitaka vyama vya siasa na wananchi kuheshimu sheria za nchi na kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kuimarisha usalama wa raia na mali zao.

Takribani mwezi mmoja uliyopita Marijani alizuia mikutano hiyo na kubainisha kuwa inatumika vibaya kuchochea vurugu na vitendo vya uvunjifu wa Amani. Katika kauli yake mbele ya vyombo vya habari, Marijaji alisema:

“Tumeona hakuna hoja ya kiusalama ya kuendelea kuzuia mikutano ya ndani kwa vyama na kuanzia leo (jana) tunaondoa katazo la mikutano ya ndani ya vyama vya siasa,” alisema na kuongeza:

“Baada ya katazo hali ya kisiasa na kiusalama imeimarika, tumetoka kule ambako tulikuwa tunatishana, watu walihamasisha watu kutotii sheria za nchi na kukiuka mamlaka ya Serikali na huko tumeshatoka, sasa hakuna tena haja ya katazo kwa kuwa vikao vingi ni vya kiutawala na kiutendaji,” alisema.

Alisema katazo la maandamano na mikutano ya hadhara isipokuwa ya wabunge kwenye majimbo yao bado lipo, hadi tathmini pana zaidi ya hali ya usalama itakapofanyika. “Mikutano ya wabunge imekuwa ikiendelea siku zote, lakini ile ya kualikana kwa ajili ya kupandikiza chuki dhidi ya Serikali au kuhamasisha wananchi kutotiisheria za nchi hii, hiyo hapana,” alisema.

Alisema kama hali ya kisiasa itaendelea hivi, basi Jeshi hilo litaruhusu mikutano ya hadhara na maandamano, ila kwa sasa hawezi kujua ni lini watafikia hatua hiyo.

“Lakini pale ambapo usalama wa nchi hii unahatarishwa, hatutasita, hatutaona aibu, hatutakuwa na kigugumizi, pa kupiga marufuku tutapiga marufuku, pa kukamata tutakamata” alisema. Alisema licha ya kuondoa katazo hilo, bado Jeshi la Polisi litazidi kufuatilia mikutano hiyo ya ndani ili kubaini kama inakiuka taratibu.

“Ufuatiliaji ni kazi yetu ya kila siku, tumesomea, tuna vifaa na tuna watu wa kufanya hiyo kazi, kwa hiyo tutafuatilia na tutajua kama tulivyokua huko nyuma,” alisema na kuongeza:

“Penye heri tutajua na penye shari tutajua pana shari, penye heri hatuna matatizo, penye uvunjivu wa sheria na uchochezi tutaingia,” alisema.

Aliongeza kuwa anaamini hadi hapa ilipofika hali ya utulivu ni kutokana na ukomavu wa kisiasa na juhudi zilizofanywa na watu mbalimbali na hakuna tena kitu cha kurudisha hali hiyo nyuma.

“Wote tuna nia moja ya kujenga nchi hii katika misingi ya amani, na wala siamini kama kuna chama cha siasa chenye nia ya kuleta vurugu endelevu, hapa tulipofika ni mahali pema,” alisema.

Katazo la mikutano ya hadhara na maandamano, lilisababisha Chadema kuanzisha operesheni inayojulikana kama Ukuta (Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania).

Operesheni hiyo ilikuwa ianze Septemba mosi lakini ikaahirishwa baada ya watu mbalimbali wakiwamo viongozi wa vyama vya siasa kukisihi chama hicho.

Hata hivyo kilisisitiza kuwa endapo hakutakuwa na kikao cha pamoja kati ya Rais John Magufuli na viongozi wa dini ili kupata suluhu kutokana na katazo hilo, basi operesheni hiyo itafanyika Oktoba mosi.

Akizungumzia kauli hiyo jana, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alisema: “Huu ni ubatili wa sheria, maana polisi hawana mamlaka ya kuzuia mikutano ya siasa iwe ya ndani au ya nje. Jeuri waliyoipata inatokana na CCM ambayo inaendelea na mikutano bila kuzuiwa.”

Kiongozi huyo wa Kambi ya Upinzani Bungeni na mbunge wa Hai alisema hakuna sheria inayozuia vyama vya siasa kufanya mikutano huku akisisitiza: “Hili ni tamko la hatari sana. Iweje vyombo vya dola viwe juu namna hii.”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CUF, Julius Mtatiro alisema: “Kisheria na kikatiba hawana haki hata kidogo na hili tamko lao la leo (jana) sijui niliitaje…, polisi wanazuiaje mikutano wakati vyama vipo kisheria na vinatekeleza wajibu wake wa kufuata sheria.”

“Polisi walipaswa kuomba radhi baada ya kutoa kauli yao. Hawapaswi kusifiwa zaidi ya kuonywa.”
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo