Walimu 62 watumbuliwa


HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imewasimamisha kazi walimu wakuu 62 wa shule za msingi na sekondari wilayani Nyamagana wakituhumiwa kuiba Sh milioni 132.5 za ruzuku ya elimu bure na kusajili wanafunzi hewa 5,559.

Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba (pichani), alibainisha hayo jana wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu hatua hiyo.

Alisema katika uhakiki wa wanafunzi hewa Jiji hilo liliunda timu ya wataalamu wa ndani kufanya kazi hiyo katika shule 38 za sekondari na 78 za msingi ambapo awamu ya kwanza katika sekondari hizo walipokea idadi ya wanafunzi 24,209, lakini ikabainika kuwapo tofauti ya wanafunzi 3,809 hewa.

“Takwimu tulizofanyia uhakiki kwa shule 38 za sekondari zilituonesha kuwapo kwa wanafunzi hewa 3,809 kati ya 24,209 na kuisababishia Serikali hasara ya Sh 125,265,590 za ruzuku iliyotolewa kwa shule hizo.

“Pia tulibaini wanafunzi wengine walikuwa wamehitimu kidato cha nne mwaka jana, lakini bado waliwekwa kwenye orodha kuwa wako shuleni wanaendelea na masomo,” alisema Kibamba.

Alisema kwa shule za msingi 78 za Jiji hilo, walipokea idadi ya wanafunzi 75,208 lakini uhakiki ulipofanyika ili kujiridhisha na kuhesabu mmoja mmoja walipatikana wanafunzi 73,498 na hivyo kubaini wanafunzi hewa 1,750 na walimu wakuu walipohojiwa, hawakuwa na majibu ya kuridhisha.

Kibamba alisema wanafunzi hewa 1,750 waliisababishia hasara Serikali kwa kupeleka ruzuku ya Sh 7,320,565, huku tume hiyo ikibaini kuwapo wanafunzi waliohitimu darasa la saba
mwaka jana, hali iliyolazimu kuundwa tume nyingine ya wajumbe 10 wakiwamo wa vyombo vya Dola ili kufanya uhakiki upya.

Mkurugenzi huyo aliongeza kuwa baada ya tume ya pili kurejea upya kufanya uhakiki Machi, ilibaini kuwa takwimu ambazo tayari zilikuwa zimetumwa Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Elimu, ambazo katika uhakiki, awali zilionesha wanafunzi wa sekondari 38 walikuwa 21,845 na baada uhakiki walithibitika wanafunzi halali kuwa ni 20,301.

“Uhakiki huu wa pili ulionesha wanafunzi wa sekondari hewa wangekuwa 1,650 na fedha za ruzuku zingeletwa na Serikali katika sekondari zao bila kuwapo shuleni.

“Pia uhakiki huo kwa shule 78 za msingi kwa takwimu za Machi zilizotumwa TAMISEMI, zilionesha wanafunzi 95,613 lakini halali ni 87,596 tulibaini wanafunzi hewa 8,017 nao fedha zao zingekuja,” alisema.

Aidha, Kibamba alisema Jiji limechukua hatua za awali kwa kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi zaidi na baada ya kukamilika watawasilisha taarifa kwa Tume ya Utumishi ya Walimu, ili kuchukua hatua za kimaadili kwa watumishi hao, wakati uongozi ukijiandaa kuchukua hatua zaidi za kisheria kwa wakuu wa sekondari 25 na 78 wa msingi waliohusika kusajili wanafunzi hewa, ili wanufaike na fedha za ruzuku.

“Tulipoamua kutekeleza agizo la Rais John Magufuli, walimu walidhani tunatania na hivyo rai yangu kwa watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wasifanye kazi kwa mazoea.

“Watekeleze majukumu yao na waepuke kutoa taarifa za udanganyifu ambazo zitawasababisha wafukuzwe kazi na kufikishwa kwenye vyombo vya maadili na sheria,” alionya.

Katika taarifa ya Mkurugenzi huyo, shule za msingi zilizoongoza kuwa na wanafunzi hewa ni Mbugani (509), Nyakabungo C (528), Nyakato (397), Nyakabungo B (330), Nyakabungo (492), Igogo B ( 305) Pamba C (362), Moringe (218) Miembeni (256) na kufanya idadi ya 1,750.

Kwa upande wa sekondari alisema jumla yake ni 3,809 na kuongeza kuwa uhakiki wa vyeti vya shule na vya taaluma kwa watumishi linaendelea na limeingia awamu ya pili.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo