Kampuni ajira za utapeli zakithiri



WAKATI vijana wengi nchini wakilalamikia Serikali kwa kukosa ajira, baadhi ya watu wameibuka na kampuni hewa zinazotangaza nafasi za kazi na kutapeli fedha na mali kwa wanaoomba kazi.

Mbali na kutapeliwa fedha, baadhi ya wanawake hujikuta wakilazimishwa kutoa rushwa ya ngono kwa ahadi ya kupewa kazi na mishahara minono bila mafanikio. Watu walioingia kwenye mtego huo wamejikuta wakitapeliwa kati ya Sh 10,000 na Sh 30,000.

Uchunguzi wa JAMBO LEO umebaini kuibuka na kuzagaa kwa kampuni hizo mijini ambazo hubandika au kugawa matangazo barabarani na kwenye vituo vya mabasi, mitaa inayopitwa na watu wengi, pia kusambaza vipeperushi kwa wapita na sehemu zenye mikusanyiko mikubwa ya watu.

Uchunguzi umebaini kuwa baadhi yao hudiriki kutumia vyombo vya habari na kulipia matangazo na nyingine mitandao ya kijamii. Kampuni hizo huwataka wahusika kuwasiliana nao kwa kupiga namba za simu za mikononi na husisitiza wanao ‘beep’ au kutuma ujumbe mfupi wa maneno hawajibiwi.

Kampuni ambazo zimetiliwa shaka na watu walioomba kazi na kulazimika kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ni Rifa Consultants Co. Ltd, Human Capital, GHM Company Ltd.

Mmoja wa waomba kazi katika kampuni ya Rifa Consultants Co. Ltd, Halima Mchau alisema baada ya kuomba kazi kama ilivyo kawaida, alisubiri majibu na baada ya kujibiwa pamoja na mashariti mengine, alikutana na ya kulipa Sh 16,500.

Mwomba kazi huyo alisema kutokana na masharti hayo, aliingiwa wasiwasi kwani hajapata kukutana na mazingira hayo ya kuomba kazi na kutakiwa kutoa fedha za usaili. Abraham Ntambara alisema aliomba kazi katika kampuni ya Human Capital na kukutana na masharti ya kulipa Sh 12,000.

Katika barua za majibu kwenda kwa waomba kazi, kampuni hizo zilijulisha waombaji kwamba wamechaguliwa kusailiwa na kuelekeza kuwa wanapaswa kulipa fedha hizo siku mbili kabla ya usaili.

Baadhi ya kampuni hizo, zinaelezewa kutoa masharti nafuu kama vile mwajiriwa kujua kusoma na kuandika Kiswahili, huku zikitolewa ahadi za mshahara wa kati ya Sh 200,000 hadi Sh 600,000 kwa mwezi.

Mmoja wa watu waliowahi kushiriki mfumo huo wa utapeli, alidai kuwa walikuwa wanakusanya hadi Sh milioni tatu kwa siku kutoka kwa watafuta ajira.

Alibainisha kwamba walikuwa wakitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya bandia, ambazo huharibiwa baada ya kufanikisha utapeli, ili kuepuka kukamatwa.

Alisema kinachofanyika ni kusambaza matangazo ya ajira na kuweka namba hizo ili wahitaji waombe na kuingizwa kwenye utapeli bila kujua.

Miongoni mwa kazi zinazotangazwa wa wingi ni usimamizi wa ofisi, usambazaji bidhaa, usafi, utunzaji stoo, usambazaji barua na uwekaji kumbukumbu za majalada.

Wengine walioingizwa kwenye utapeli huo walidai kuwa baadhi ya kampuni hujinadi kuwa za kimataifa, hivyo kuhitaji wanaojua Kiingereza.

“Ninayo furaha kukutaarifu kuwa timu ya usaili imepokea, kupitia na kujadili ombi lako na kufanya uamuzi wa kukuita kwenye usahili wa ana kwa ana,” inasema sehemu ya barua
ya majibu.

Barua hiyo ilibainisha kuwa taasisi hiyo ni ya kimataifa hivyo lugha ya mawasiliano ni Kiingereza na pia ndiyo lugha itakayotumika kwenye mazingira ya kazi.

Pia barua iliendelea kusema, kuwa watu wote ambao wamechaguliwa wanashauriwa kuandaa kila kitu kwa Kiingereza na si lugha nyingine yoyote.

“Hatutakubaliana na jambo lolote ambalo litakuwa kwa Kiswahili kabla ya usaili, uzingatie agizo la mteja wako,” alisema.

Aidha, katika kuhakikisha kuwa kampuni hizo zinaonesha uhalali wao, zimekuwa zikitaja kuwa na matawi katika miji mbalimbali. Kampuni ya Rifa ilieleza kuwa ofisi zake ziko Dar es Salaam, mtaa wa Ohio, karibu na benki ya Barclays.

Pia ilisema ipo katika eneo la Afrika Mashariki ambako wanafanya shughuli mbalimbali. Taarifa hizo zilionesha fedha hizo ambazo wanatakiwa kutoa kuwa zitasaidia waomba kazi kupewa chai, ada ya mahojiano na malipo ya wahoji wanaotoka nje ya mkoa husika.

Hali kadhalika wasailiwa walipaswa kulipa fedha hizo kupitia mtandao wa simu namba +255 783749091 kabla ya jana saa moja usiku kwa kampuni ya Rifa.

Maeneo ambayo yametajwa kwa ajili ya usaili ni Karena Hotel ya Shinyanga ambako unafanyika leo na wahusika walitakiwa kuwasiliana kwa namba +255 686479958 kwa maelezo zaidi.

Dar es Salaam usahili utakuwa kesho na mawasiliano yafanywe kwa namba +255 686479958 kwa maelezo zaidi, Morogoro namba +255 686479958, Meatu Hotel Singida namba +255 686479958, Tanga namba +255 686479958 na Arusha namba +255 686479958.

Maeneo mengine ni Mbeya namba +255 686479958, Mwanza Ngasamo Hotel namba +255 686479958, Pwani namba +255 686479958 na Mtwara namba +255 686479958. Barua hiyo imeandikwa na Abubakari Gondwe ambaye anajitambulisha kama Mkuu wa Idara ya Ajira wa kampuni hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo