Mbatia ataka Rais afunge mjadala IPTL, Escrow


Fidelis Butahe

MWENYEKITI wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia (pichani) amemtaka Rais John Magufuli kuwachukulia hatua waliotajwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta Escrow na IPTL akieleza kwamba wakati sakata hilo lilipoibuka bungeni, kiongozi mkuu huyo wa nchi alikuwa waziri hivyo anawajua wote waliohusika.

Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo amehoji; iweje Rais Magufuli alitengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kwa sababu ya kujibu swali bungeni akiwa amelewa na sasa anashindwa nini kuwatumbua waliotajwa kupata mgawo wa fedha hizo?

“Bunge lilitoa maazimio manane kuhusu Escrow, mpaka sasa utekelezaji wake unasuasua. Tunashuhudia utumbuaji majipu tu kwa watendaji mbalimbali, lakini hatuoni chochote kuhusu wahusika Escrow na IPTL, kwa hili vipi Rais Magufuli?” alisema.

Mbatia alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu hukumu ya Baraza la Usuluhishi la Benki ya Dunia kulitaka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) kuilipa Benki ya Standard Chartered Hong Kong (SCB-HK) zaidi ya Sh bilioni 320.

Uamuzi wa baraza hilo umekuja takribani miaka miwili tangu Serikali iliporuhusu kiutatanishi kufanyika kwa malipo ya zaidi ya sh bilioni 350 kutoka katika akaunti hiyo iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda Kampuni ya Harbinder Singh Seth ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited (PAP).

Akaunti hiyo ilifunguliwa BoT kuhifadhi fedha za malipo ya umeme kusubiri kumalizika kwa mzozo wa kimkataba baina ya Kampuni ya IPTL na Tanesco.

Malipo hayo tata yalisababisha Bunge kutoa maazimio manane, ikiwa baada ya ripoti yake na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuwasilisha bungeni na wahusika kuonekana kuhusika moja kwa moja au kwa kushindwa kutekeleza majukumu yao.

“Hatuna viongozi wa kweli na mfumo ni uleule uliotekwa na dhana ya kujadili watu. Katika Escrow Rais Magufuli alikuwa sehemu ya maazimio ya Bunge akiwa waziri wa ujenzi,” alisema Mbatia na kuongeza:

“… Alikuwa katika Baraza la Mawaziri na anajua uamuzi wa Kikwete (Jakaya-Rais mstaafu) kuwaondoa akina Tibaijuka (Profesa Anna) na Muhongo (Profesa Sospeter) na anajua kuwa maazimio ya Bunge lazima yaheshimiwe.”

Alisema Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani ametumbua majipu mengi lakini ameshindwa kuwatumbua waliohusika katika sakata la Escrow na IPTL.

“Nawatahadharisha watawala, wajue leo wapo, lakini kesho hawapo. Tungezingatia maazimio ya Bunge, haya yasingetokea. Hii ni kwa sababu ya kubebana na kulindana,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo