‘Sinema’ ya siasa za CUF yaendelea


Fidelis Butahe na Suleiman Msuya

HALI si shwari CUF. Huo ndio ukweli kutokana na Baraza la Uongozi kueleza vifungu vya Katiba ya Chama hicho ilivyotumika kumfukuza uanachama Profesa Ibrahim Lipumba ambaye naye ametaja vifungu vyake, kupinga uamuzi huo.

Msuguano huo umewaacha wafuasi wa chama hicho njia panda, huku wanaounga mkono pande hizo mbili zinazovutana wakibaki njiapanda bila kujua hatima ya chama hicho.

Wakati hayo yakiibuka ndani ya chama hicho, wanasheria waliozungumza na JAMBO LEO walimtaka mtaalamu huyo wa uchumi kwenda mahakamani kama anaona hakutendewa haki na chama chake.

Walisema kuendelea kwake kusimamia ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi aliyemtambua kuwa Mwenyekiti halali wa CUF, hakuwezi kumpa uhakika wa kurejea kwenye wadhifa wake.

Mkanganyiko

Baraza Kuu la chama hicho lililokutana juzi Zanzibar, lilisema limemfukuza Profesa huyo uanachama na si uongozi, kwa sababu aliandika barua ya kujiuzulu na tayari wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama hicho walisharidhia uamuzi wake.

Profesa Lipumba ambaye aliandika barua ya kujiuzulu uenyekiti Agosti 5 mwaka jana, kabla ya Juni kuandika nyingine ya kutengua na kusisitiza kuwa yeye ni Mwenyekiti halali, alitumia kifungu cha 83 (1) ya Katiba ya chama hicho, kuwa Baraza la Uongozi lina uwezo wa kuwasimamisha uanachama Katibu Mkuu, Mwenyekiti wa Taifa na Makamu wake na si kuwafukuza uanachama.

Hata hivyo, katika maelezo yake, Baraza Kuu lilisema limemfukuza kama mwanachama wa kawaida kwa mujibu wa kifungu cha 10 (c) kinachosema: “Atafukuzwa au kuachishwa uanachama na Mkutano Mkuu wa Taifa au Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa masharti ya Katiba hii”.

Katika hoja ya Profesa huyo kuwa barua yake ya kujiuzulu haikujibiwa, Baraza Kuu lilisema angeweza kuhoji kutojibiwa barua hiyo au kuandika barua ya malalamiko, huku ikitumia kifungu cha 108 (5).

Kifungu hicho kinasema: “Mwanachama au kiongozi yeyote aliyeamua kukata rufaa kwa jambo lolote lile, atafanya hivyo kwa ngazi iliyo juu ya kikao kilichotoa uamuzi ambao hakuridhika nao katika kipindi kisichozidi siku 14 tangu siku uliotolewa uamuzi huo”.

Wakati Profesa Lipumba akishikilia msimamo wake wa kuwa Mwenyekiti halali, CUF imebainisha kuwa alitamka kuwa kuanzia wakati akitoa barua ya kujiuzulu, alitamka kuwa hatakuwa kiongozi tena na atabaki kuwa mwanachama wa kawaida, tayari vikao vya Baraza Kuu vilishakaa mara tatu na hakuhudhuria vikao hivyo, jambo ambalo lilimpotezea sifa.

Chama hicho kilinukuu Ibara ya 117 (2): “Kiongozi atajiuzulu kwa kuandika barua na kuweka saini yake kwa Katibu wa Mamlaka iliyomchagua au kumteua, na kiongozi huyo atahesabiwa kuwa amejiuzulu ikifika tarehe aliyoainisha katika barua yake kuwa atajiuzulu pindi akikubaliwa na Mamlaka iliyomchagua au iliyomteua.

“Au kama hakuanisha tarehe ya kujiuzulu kwake, basi atahesabiwa amejiuzulu baada ya Katibu wa Mamlaka iliyomteua au kumchagua, kupokea barua hiyo na Mamlaka iliyomchagua au kumteua kukubali”.

Wanasheria

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Kitivo cha Sheria, Dk Onesmo Kyauke alisema kilichobaki sasa ni msomi huyo kwenda mahakamani ili kudai haki yake.

Dk Kyauke alisema iwapo aliitwa kwenda kujitetea mbele ya Baraza hilo na hakwenda basi hawezi kuwa na sifa za kuendelea kuwa katika nafasi hiyo na sehemu sahihi kwa sasa ni mahakamani.

“Sina mambo mengi ya kuzungumzia kilichotokea, lakini iwapo Katiba imefuatwa, hana sifa tena ya kuwa Mwenyekiti, hivyo kwa ushauri wangu aende mahakamani,” alisema.

Mwanasheria wa Mahakama ya Rufaa, Profesa Abdallah Safari alisema kwa mtazamo wake, sehemu sahihi kwa Lipumba ni mahakamani, kwani ndani ya chama inaonekana haaminiki tena.

“Naamini salama yake ni mahakamani, kwani kikatiba natambua Baraza lina nguvu ya hicho kilichotokea, hasa kama limemjadili kama mwanachama na si kiongozi,” alisema.

Waunga mkono

Katika hatua nyingine, Jumuiya za Vijana, Wanawake, Baraza la Wazee na Bodi ya Wadhamini ya Chama cha Wananchi (CUF), wameunga mkono uamuzi wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kumfukuza Profesa Lipumba.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, viongozi wa taasisi hizo za CUF walisema uamuzi uliofanywa na chama ni sahihi.

Wazee

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa CUF, Hamid Juma Haji alisema wako pamoja na Baraza Kuu na wanamtaka Lipumba aheshimu uamuzi huo.

“Sisi wazee tumekuwa katika wakati mgumu kupitia hali hii lakini uamuzi ambao umefanywa na viongozi wa Baraza ni sahihi na tunaunga mkono,” alisema.

Vijana

Mwenyekiti wa Juvicuf Taifa, Hamidu Bobali alisema wao vijana wanaungana na Baraza Kuu ili kunusuru chama. Bobali alisema vijana wamegundua mazingira ya hujuma ndani ya chama chao hivyo hawako tayari kuona ikitokea.

Wanawake

Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake, Severine Mwijage alisema wanaunga mkono kwa asilimia 100 uamuzi huo na kuahidi kutoa ushirikiano katika masuala yote ya kupigania chama.

Wadhamini

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chama hicho, Abdallah Katau alisema Bodi inakubaliana na uamuzi huo huku akimtaka Lipumba aondoke ndani ya chama hicho kwani hana sifa za kuwa hapo.

Lipumba

Akizungumza jana Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alisema uamuzi wa Katibu Mkuu Maalim Seif kumvua uanachama ni batili kwani amevunja Katiba ya chama hicho. Aidha, amesema hafukuziki CUF na hana mpango wa kuhama hivyo wenye lengo hilo wajipange na ataitisha kikao cha Baraza Kuu Taifa muda wowote kuanzia sasa.

“Nipo CUF, na nipo ngangari kinoma, hivyo kiti kimejaa wasiwe na wasiwasi, na kikao cha Baraza Kuu kitaitishwa hivi karibuni, mimi sifukuziki CUF sina mpango wa kuhama wala kukiacha na kadi yangu bado inadai,” alisema.

“Kwangu Katibu Mkuu ni Katibu Mkuu, nafasi na ofisi yake ipo, aje, akija apite hapa kwa Mwenyekiti anisalimie ili nimwelekeze cha kufanya, pia apate miongozo ya kukijenga chama maana nipo hapa na nitazidi kuwapo,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo