Wake wa waliouawa kesi ya Zombe kudai fidia


BAADA ya Mahakama ya Rufaa kutoa adhabu ya kunyongwa hadi kufa kwa aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wa madini kutoka Mahenge mkoani Morogoro, wake wa marehemu hao wamesema wanajipanga kulishtaki Jeshi la Polisi ili liwalipe fidia.

Mahakama ya Rufani ilitoa hukumu ya kunyongwa hadi kufa kwa Christopher Bageni Septemba 16, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara hao watatu wa madini; Mathias Lunkombe, Sabinus Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na dereva teksi Juma Ndugu. Mauaji hayo yalifanyika katika Msitu wa Pande uliopo Mbezi Luis, jijini Dar es Salaam.

Katika hukumu hiyo iliyotolewa na jopo la majaji watatu; Benard Luanda, Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage, aliyekuwa mkuu wa upelelezi wa mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Abdallah Zombe na wenzake wawili walinusurika baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yao.

Pamoja na Zombe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ambao waliachiwa huru ni ASP Ahmed Makelle na Koplo Rajabu. Ilidaiwa kuwa washtakiwa hao walitenda kosa hilo, Januari 14, 2006.

Msimamo wa wajane Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wake wa marehemu walisema hawajaridhishwa na hukumu hiyo kwa kuwa imemtia hatiani mtuhumiwa mmoja tu.

Hata hivyo, walisema ilimradi imethibitika kwamba Polisi waliua, wanajipanga kufungua kesi ya madai ili walipwe fidia, wakieleza kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuona Serikali imezitelekeza familia za marehemu hao kwa zaidi ya miaka kumi sasa.

Mke wa marehemu Mathias Lunkombe aliyeachwa na watoto wawili, Mapha Kazingoma alisema hali ya maisha baada ya kifo cha mumewe ilikuwa mbaya kutokana na kulazimika kulipia kodi ya nyumba na gharama za shule kwa watoto.

Mjane huyo alisema kwa kuwa tayari Serikali kupitia mahakama imejiridhisha kuwa wanaume zao waliuawa kimakosa, kuna haja ya kudai fidia ili kupunguza uchungu waliopata na makali ya maisha.

“Tuko katika mchakato wa kukutana wote (wake wa marehemu) ili tuone tunafanyaje kufungua kesi hiyo, lakini lazima tulipwe fidia kwa kuwa sasa imethibitika kuwa waume zetu waliuawa kwa makusudi,” alisema.

Mjane huyo alimwomba Rais John Magufuli kuzisaidia familia za marehemu hao ili zipate haki waliyokuwa wakiisotea siku nyingi. Aliyekuwa mke wa marehemu Sabinus Chigumbi maarufu kwa jina la Jongo, Theresia Maswanyiaalisema kuwa kitendo cha kutelekezwa na Serikali kimeendelea kusababisha majonzi kwao, kwani licha ya kuwa na majukumu ya malezi ya watoto watano alioachiwa na marehemu mumewe, hakuna msaada wowote anaopata kutoka serikalini.

Theresia ambaye kwa sasa anaendesha maisha kwa kutegemea kodi ya nyumba aliyoachiwa na marehemu mumewe, alisema mara baada ya hukumu hiyo kutolewa wote wamekutana na kuweka mikakati ya kufungua kesi ya madai ili Serikali iwalipe fidia. “Kwa kweli suala hilo kwetu halijaisha, tunakusanya nguvu ili tufungue madai watulipe fidia,” alisema mjane huyo.

Polisi wasimulia marehemu walivyouawa Katika hatua nyingine, baadhi ya askari polisi wamesimulia tukio la mauaji ya wafanyabiashara hao wa madini wakieleza kuwa lilikuwa ni ukatili wa kutisha.  Polisi hao waliokuwepo mahakamani siku ya hukumu walisema kulichofanyika ni unyama wa kutisha, hivyo hukumu iliyotolewa ni sahihi.

Huku wakiomba wasitajwe gazetini, polisi hao walisema kabla ya kuuawa, wafanyabiashara hao waliomba askari hao wasimuue mmoja kati yao kwa sababu alikuwa bado mwanafunzi na kwamba hata kiumri alikuwa mdogo.

“Waliomba aachwe ili aje alee famili zao, kwa sababu wao walikuwa tayari kufa kwa sababu tayari walishaelezwa kuwa watauawa,” alisimulia askari huyo. “Licha ya maombi hayo, yule waliyeomba aachwe ndiye aliyekuwa wa kwanza kuuawa kwa kupigwa risasi na baada ya tukio hilo, ndugu wa mwanafunzi huyo ambaye alikuwa miongoni mwa walioomba alilamba damu ya ndugu yake.”

Alifafanua: “Baada ya kulamba damu hiyo huku akiwa amepiga magoti kama walivyokuwa wameelekezwa, alilala chini tayari kwa kumiminiwa risasi ndipo naye aliuawa kwa kumiminiwa risasi kwa nyuma.”

Askari mwingine alisema damu ya wafanyabiashara hao na dereva teksi itaendelea kuwatafuna hata wale ambao hawakupatikana na hatia kwa mauaji ya vijana hao.

“Mimi ni askari lakini naamini vijana hao hawakuwa na hatia, damu yao itaendelea kuwatafuna wote, hata walioachiwa huru kwenye kesi hiyo kwani hakuwa Bageni peke yake na kilichofanyika ni ukatili wa wazi,” alisema..
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo