Mwendokasi waua 12 barabarani Njombe


MWENDOKASI wa basi la kampuni ya New Force ndicho chanzo cha upotevu wa maisha ya watu 12 na majeruhi 28 barabarani usiku wa kuamkia jana.

Basi hilo lilipinduka saa 2 usiku mkoani Njombe katika kijiji cha Lilombwi kata ya Kifanya tarafa ya Igominyi lilipofika kwenye kona ya barabara likitoka Dar es Salaam kwenda Songea mkoani Ruvuma.

Akizungumza na JAMBO LEO kutoka mkoani humo jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Pudensiana Protas alisema kwa sasa majeruhi wanaendelea na matibabu na ndugu wanachukua miili kwenda kuzika huku wengi wa marehemu wakiwa ni wa Ruvuma.

“Hadi sasa hakuna kifo kilichoongezeka, kinachofanyika ni ndugu kuchukua miili kwenda kuzika. Hivyo kama kutakuwa na taarifa nyingine tutawaeleza, lakini chanzo cha ajali ni mwendokasi wa basi hilo,” alisema Kamanda.

Wakati huo huo, Rais John Magufuli ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizopatwa na msiba kutokana na ajali hiyo.

Katika taarifa ya jana ya Ikulu, salamu hizo kwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Rehema Nchimbi, Rais Magufuli alieleza kupokea taarifa za ajali hiyo kwa masikitiko makubwa na kuungana na familia, ndugu, jamaa na marafiki waliopatwa na msiba katika kipindi kigumu cha majonzi.

“Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Dk Nchimbi naomba unifikishie pole nyingi kwa waliopatwa na msiba, wamepoteza wapendwa wao, wamepoteza watu waliowategemea na hakika familia zimetikisika.

“Sote tuwaombee waliofikwa na msiba wawe na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu na pia marehemu wapumzishwe mahali pema peponi,” alisema.

Aidha, Rais Magufuli aliwapa pole majeruhi na kuwaombea wapone haraka ili waweze
kuungana na familia zao na kuendelea na shughuli zao za kila siku.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo