Nyama choma ya baa hatari


NYAMA ni mojawapo ya mlo unaopendwa na watu wengi. Ukienda kwenye baa, migahawa na hotelini utakuta milo mingi inayoliwa ikiandamana na nyama.

Hii inatokana na ukweli kwamba wataalamu wa afya wanapendekeza kula mlo kamili, wakiwa na maana chakula chenye virutubisho vyote, protini, wanga, madini na vitamini. Vyote hivi wanapendekeza vitumike kwa uwiano sahihi ili kuwa na afya bora.

Protini ni aina ya viinilishe vinavyopatikana kwa wingi katika nyama. Kazi ya protini ni kujenga mwili. Nyama ni sehemu ya vyakula ambayo inaonekana kuvuta hamu ya kula kwa watu wengi. Wanywaji baa hupendelea kula nyama zaidi kama moja ya kihamasishio cha starehe ya kupata kilevi.

Nyama inayotumiwa zaidi ni ile inayotokana na ng’ombe, nguruwe, mbuzi, kuku na kondoo,hata hivyo inaweza kuchafuliwa na vimelea mbalimbali vya maradhi endapo kanuni bora za usafi hazitazingatiwa wakati wa uandaaji na utunzaji wa nyama hiyo.

Taarifa ya utafiti iliyofanywa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) katika maeneo mbalimbali ya uandaaji wa nyama katika kiwango cha kuwa tayari kuliwa, umebaini kuwa kuna ukiukwaji mkubwa wa kanuni za afya.

Katika uchunguzi wao, kanuni hizi zimekuwa zikivunjwa zaidi kwa wale wanaoandaliwa nyama choma na hizi mara nyingi hufanyika kwenye baa.

Kwa hali halisi ya mazingira ya Tanzania, watu wengi hupenda kufanya starehe baa ambako hunywa na kula. Mazingira ya baa nyingi ambazo katika maneo ya mji, unaweza kuziona karibu kila kona, nyama choma ni moja ya kiburudisho muhimu kinachopatikana kwa wingi.

Kasoro za utayarishaji

TFDA inaeleza kuwa kabla ya kuliwa, nyama huweza kuandaliwa kwa njia ya kuchomwa kwenye jiko la mkaa, kuni, jiko la umeme au gesi hadi hapo inapobadilika rangi kuashiria kuwa imeiva.

Utayarishaji wa aina hii hupendwa na walaji wengi kwa kuwa unaamika. Hii ni bala ya kupika kwa kutumia maji au mafuta yake, hivyo kuwa na ladha nzuri.

Utayarishaji wa nyama kwa njia ya kuchoma hufanyika kwa wingi kwenye maeneo ya baa, hoteli, migahawa na hata majumbani.

Hata hivyo, baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa mara nyingi nyama inayochomwa haiivi vizuri na hivyo kubaki na vimelea vya maradhi ambavyo ni hatari kwa afya ya mlaji.

Hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi hasa nyama inayochomwa inapokuwa haikukaguliwa na kupitishwa na mamlaka husika kuwa inafaa kwa matumizi ya binadamu.

Aina ya vimelea vya maradhi vinavyoweza kupatikana kwenye nyama mbichi ni pamoja na Salmonella, Compilobacter, Brucella Abortus, L. Monocytogens, C. Bovis, na E. Coli ambavyo hupatikana kwenye matumbo au minofu ya wanyama husika. Iwapo kanuni za usafi hazitazingatiwa wakati wa uchinjaji wa mnyama, vimelea hivyo huweza kuingia kwenye nyama mbichi hasa wakati mnyama anapochunwa ngozi na kutolewa utumbo.

Namna ya kuchoma nyama

Ili nyama iweze kuiva vizuri na hivyo kuepuka uchafuzi au uwepo wa vimelea vya maradhi ni muhimu kuzingatia vigezo kadhaa.

Kigezo cha kwanza ni ukubwa wa kipande cha nyama ambacho kimewekwa kwenye jiko kwa ajili ya kuchomwa. Mchomaji anapoweka vipande vikubwa vya nyama inaweza kuiva na kubadilika rangi sehemu ya nje tu na kuacha ya ndani.

Ili vimelea vya maradhi viweze kufa, linahitajika joto lisilopungua kiasi cha nyuzi joto 75 hasa kwa sehemu ya katikati ya kipande cha nyama inayochomwa. Kigezo cha pili ni kiasi cha moto au joto linalotumika kuchomea nyama.

Wachomaji wengi wa nyama hupenda kuchoma kwenye moto mdogo kwa muda mrefu kwa lengo la kuepuka nyama isiungue.

Kitaalamu joto hili linaweza lisiue vimelea vya maradhi bali likawezesha vimelea hivyo kuendelea kuishi na kuzalisha sumu.

Kigezo cha tatu ni aina ya vimelea vya maradhi vilivyopo kwenye nyama. Kuna vimelea ambavyo vina uwezo mkubwa wa kustahimili joto kali. Nyama iliyochafuliwa na aina hii ya vimelea inahitaji kupikwa kwenye moto mkali usiopungua nyuzi joto 100 ili kuweza kuua viini vya maradhi.

Ili kupunguza uchafuzi wa vimelea vya maradhi kwenye nyama iliyochomwa, mchomaji anapaswa kuhakikisha kuwa ananunua ile ambayo na kuruhusiwa kutumiwa na binadamu. Kanuni hii inalenga kuwatahadharisha wachomaji wa nyama kutonunua nyama sehemu zisizotambulika ili kuepuka kununua iliyotokana na mnyama mwenye magonjwa hatari kwa afya ya binadamu.

Eneo la kuchomea na kuuzia nyama linapaswa kuwa safi na liwe limekaguliwa na kuruhusiwa kufanyia biashara hiyo na Afisa Afya wa eneo husika.

Maeneo mengi hususan kwenye minada, nyama inachomwa kwenye mazingira yenye vumbi na yasiyozingatia kanuni za usafi, hali inayoweza kuhatarisha afya ya walaji. Vyombo vinavyotumika kukatia na kuuzia pia vinapaswa kuwa katika hali ya usafi wakati wote.

Wachomaji wa nyama wanapaswa kuzingatia kanuni bora za usafi na kuepuka mienendo inayoweza kusababisha uchafuzi wa nyama.

Kwa mfano, baadhi ya wachomaji nyama hususani maeneo ya baa, hupokea fedha kutoka kwa wateja na kutoa chenji wakati akiwa anaendelea kutayarisha nyama iliyokwisha chomwa tayari kwa kuliwa.

Hali hii inaweza kusababisha nyama ilichomwa kuchafuliwa na vimelea mbalimbali vya maradhi. Ni vyema mwandaaji wa nyama asijihusishe kabisa na upokeaji wa fedha wakati anapotoa huduma ya nyama inayochomwa.

Vifaa vya kuchomea

Vifaa vya kuchomea nyama vinapaswa kusafishwa kwa maji safi ya moto na sabuni ili kupunguza idadi ya vimelea ambavyo vinaweza kuwa vimeingia kwenye nyama.

Nyama inapaswa kukatwa vipande vyembamba kwa ajili ya kuchoma ili sehemu ya katikati iweze kufikiwa na joto kali lenye uwezo wa kuua vimelea. Ikumbukwe kuwa ili kuwa na ufanisi katika kuua vimelea vya maradhi ni vizuri mchomaji akaanza kwanza kwa moto mkali na baadaye mdogo.

Mtayarishaji wa nyama choma anatakiwa kutenganisha sehemu na vifaa vya kukatia na kuandalia nyama mbichi na nyama iliyoiva. Uchunguzi unaonesha kuwa waandaaji wengi wa nyama choma wamekuwa wakitumia meza moja, kibao kimoja na kisu kimoja kwa ajili ya kukatia nyama mbichi na nyama iliyochomwa.

Hii ni hatari sana kwa afya ya walaji kwa kuwa upo uwezekano mkubwa wa uchafuzi kutokea baada ya nyama kuiva.

Nyama iliyochomwa, kuiva vizuri na kuandaliwa katika mazingira yanayofaa inatakiwa kuliwa ikiwa bado ya moto. Endapo nyama iliyochomwa itakuwa imepoa, inashauriwa kurudishwa tena kwenye moto mkali kabla ya kuliwa.

Wachomaji wengi wa nyama huchukua pande kubwa la nyama na kulichoma na wanapoona limeiva hulitoa na kulikatakata tena kwa kulipoooza kidogo ili asiungue wakati wa ukataji.

Hii ndiyo kusema, anaipoozesha ili asiathirike kwa joto kali wakati anaikata na akimaliza huiweka kwenye chombo tayari kumpelekea mlaji. Matokeo ya mpango wa namna hii, mlaji hupelekewa nyama ambayo tayari imepoa jambo ambalo ni hatari kwa afya yake.

Mbaya zaidi mkataji anaweza akawa anapokea fedha na hata kurejesha chenji, mazingira ambayo yanamfanya kueneza vimelea vya maradhi kwa nyama anayopelekewa mteja.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo