Maalim Seif, Lipumba ana kwa ana Buguruni



Suleiman Msuya na Celina Mathew

Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba aliyetangazwa kuvuliwa uanachama, wanatarajiwa kukutana uso kwa uso leo hali inayotarajiwa kutoa sura mpya ya mgogoro wa chama hicho.

Wawili hao wanatarajiwa kukutana kwenye ofisi za makao makuu ya chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam wakati Maalim Seif atakapofika hapo, siku nne tangu Baraza Kuu la Taifa la CUF lilipotangaza kumvua uanachama Profesa Lipumba.

Kukutana kwa viongozi hao kutatokea huku Maalim Seif akitafuta kuonana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Manguili kuwasilisha malalamiko yake dhidi ya Jeshi hilo, ambapo jana alisotea kuonana na kiongozi huyo bila mafanikio.

Taarifa zilieleza kuwa kabla ya kuingia ofisini, Maalim Seif atataka kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali wanayoamini Jeshi hilo lina uwezo nayo, ikiwamo barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ya kumtambua Lipumba ambayo nakala yake imepelekwa kwa IGP.

“Tangu asubuhi tunawasiliana na Jeshi la Polisi kupitia Msaidizi wa IGP, hadi ninavyoongea nawe saa tisa hii (alasiri), hakuna msaada tuliopata,” alisema Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani.

Alisema maombi ya upande wa Maalim Seif kukutana na IGP yamejikita katika kupata ufafanuzi wa barua ya Msajili na mambo mengine ambayo wanaamini kuwa Jeshi hilo linahusika, hivyo kupaswa kutolea ufafanuzi. Alisema waliandika barua kwa IGP kuomba kuonana naye lakini walijibiwa na Msaidizi kuwa IGP ana majukumu mengine hivyo hawataonana naye.

Alisema kuna hali inayowatia shaka katika mchakato wa kurejeshwa Profesa Lipumba madarakani na kwamba pamoja na wao kumfukuza, bado kuna mambo wanahitaji ufafanuzi.

Hata hivyo, JAMBO LEO lilipomtafuta IGP Mangu kuzungumzia suala hilo alisema: “Sina taarifa za watu hao, hata hivyo niko kwenye kikao nadhani ungewasiliana nao ili wakueleze vizuri wamefikia wapi.”

Hata hivyo, Msaidizi wa IGP aliyetajwa kwa jina moja la Makuri aliyeelezwa alikuwa akiwasiliana na CUF, alisema: “Ni kweli tumewasiliana nao, ila mimi si Msemaji wa Jeshi la Polisi, mpigieni Advera (Bulimba) atakuelezeni kila kitu kwani anajua, nielewe hivyo.”

Lipumba
Akizungumzia ujio wa Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema anamkaribisha na kwamba yuko tayari kufanya naye kazi kwa sababu ofisi yake ipo.

“Kama Katibu Mkuu (Maalim Seif) anakuja aje, ofisi yake ipo jambo la msingi akifika aripoti kwangu ili niweze kumpa mwongozo wa kazi za kufanya tujenge CUF,” alisema Lipumba.

Huku akieleza kwamba hana taarifa ya ujio wa wabunge na mameya wa CUF kutoka Zanzibar katika makao makuu ya chama hicho, Profesa Lipumba alisema:

“Sijaitisha kikao cha wabunge, kama wamejipanga kuja kufanya vurugu nawasihi watumie busara zao, ili kumaliza mgogoro ndani ya chama, unaoendelezwa na wenzetu wa Zanzibar.”

Alisema kwa sasa wapo kwenye utaratibu wa kuhakikisha wakurugenzi wa idara za CUF wanabadilishwa na kuongeza Makamu Mwenyekiti ambaye alihama chama na nafasi yake kuwa wazi akisema viongozi hao watathibitishwa kwenye kikao cha Baraza Kuu.

“Nina mamlaka ya kuteua na kutengua wakurugenzi, na ili waweze kuwa kamili lazima wathibitishwe, lakini katika kipindi cha mpito wanaweza kuendelea kufanya kazi kama kawaida,” alisema.

Aliongeza kuwa sakata hilo linazidi kuibua mwamko mpya kwa wanachama na anapokea simu nyingi huku akisema atazunguka mikoa mbalimbali nchini, ili kujenga chama, na hawako tayari kuona CUF inakufa Bara.

Alisema wakati mapambano hayo yakiendelea wapo wanachama wenye ari ya kuhakikisha CUF inajengwa na kwa sasa wana kazi kubwa ya kukuza chama na mgogoro unamalizika.

Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema hana mpango wa kwenda mahakamani kupinga kutimuliwa kwake kwa sababu anaamini uamuzi wa Msajili ni wa msingi na Maalim Seif na wenzake sasa wanaubeza, ingawa awali waliusifu.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo