Uingereza yatoa bilioni 6/- tetemeko


Leonce Zimbandu

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amepokea msaada wa Sh. bilioni 6.3 kutoka Shirika la Misaada la Uingereza (DFID) kwa ajili ya ujenzi wa Sekondari ya Ihungo, Bukoba mkoani Kagera.

Ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kuanza mara moja chini ya Wakala wa Majengo ya Serikali (TBA) ili kutekeleza masharti ya msaada wa kujenga shule ya kisasa itakayohimili tetemeko la ardhi.

Profesa Ndalichako (pichani) alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana baada ya kukabidhiwa msaada huo.

Alisema DFID pia imeonesha nia ya kujenga nyumba 10 za walimu wa sekondari ya Rugambwa, hali hiyo ikionesha Uingereza kuguswa na tukiohilo.

“Nimeona niwaite leo ili kuzungumzia msaada ambao Serikali imepokea kutoka DFID kwa ajili ya kujenga shule ya Ihungo ambayo inatarajiwa kukamilika Januari,” alisema.

Alisema shirika hilo lilifikia hatua hiyo baada ya ujumbe wake kutembelea waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Kagera Septemba 10.

Profesa Ndalichako alifafanua kuwa michoro ya ramani ya shule hiyo imekamilika ambayo inahusisha ujenzi wa maabara na vyumba vya kisasa vya madarasa.

Mkuu wa DFID Tanzania, Vel Gnanendran alisema baada ya kutembelea Kagera walijionea namna watu walivyoathirika na tetemeko hilo. “Uingereza kupitia DFID imeamua kutoa msaada wa kuijenga shule hiyo na nyumba 10 za walimu,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo