JPM avunja rekodi Afrika


RAIS John Magufuli, amevunja rekodi Afrika, kwa kuibuka kidedea mbele ya marais 128 wa Bara hilo, waliopata kufanyiwa utafiti kuhusu kukubalika na wananchi wao, baada ya utafiti wa sasa kuonesha kukubalika na Watanzania kwa asilimia 96.

Kabla ya matokeo ya utafiti huo yaliyotolewa jana, rekodi ya marais waliopata kukubalika na wananchi wao kwa wingi katika utafiti, ilikuwa ni kwa asilimia 93 tu.

Rekodi hiyo ilikuwa ikishikiliwa na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni mwaka 2000 (93%); Rais mstaafu wa Tanzania, Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa mwaka 2005 (93%) na Rais mstaafu wa Kenya, Mwai Kibaki mwaka 2003 (93%).

Wengine waliopata kukubalika kwa viwango vya juu ni Sam Nujoma wa Namibia (90%), Ifikepunye Pohamba wa Namibia pia (90%) na Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria (90%).

Taarifa ya utafiti huo wa Sauti ya Watu ilifanya marejeo ya utafiti uliopata kufanywa huko nyuma na taasisi ya Afrobarometer, ambayo imekuwa ikikusanya taarifa kutoka nchi 34 za Afrika, kuhusu kiwango cha kukubalika kwa marais katika vipindi tofauti.

Ingawa maswali na mbinu ya utafiti wa Afrobarometer ni tofauti na wa Sauti ya Wananchi, lakini Twaweza walitumia matokeo ya Afrobarometer kufanya ulinganishi na matokeo ya utafiti huo uliotangazwa jana, kutokana na uwezo na muda wa utafiti wa taasisi hiyo katika nchi za Afrika.

Akizungumza wakati wa kutoa matokeo ya utafiti huo, Mshauri Mwandamizi wa Mawasiliano wa Twaweza, Risha Chande alisema asilimia 88 ya wananchi wana imani kuwa Rais Magufuli ataendelea na kasi aliyoanza nayo mpaka mwisho wa awamu yake ya kwanza ya uongozi.

“Utafiti huu unaonesha kuwa asilimia 69 ya wananchi walifurahishwa na juhudi za Rais za kuondoa wafanyakazi hewa, wakati asilimia 61 walipongeza sera ya elimu bure, huku asilimia 61 wakifurahishwa na ‘utumbuaji’ watumishi wa Serikali,” alisema Chande.

Chande alisema utafiti huo unaonesha kuwa wananchi wengi wanaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Tano ya kufanya maboresho katika huduma za umma, ikiwamo Mamlaka ya Mapato (85%), shuleni (75%), vituo vya Polisi (74%), Mahakama (73%) na vituo vya afya (72%).

Kwa huduma zinazotolewa katika utumishi wa umma, utafiti ulionesha kuwa asilimia 95 ya wananchi wanaridhishwa na huduma za madaktari, walimu na maofisa tawala kwenye ofisi za umma.

“Pamoja na kiwango kikubwa cha kukubalika kwa Serikali ya Awamu ya Tano, wananchi walisema suala la umakini na kanuni za demokrasia na haki, ni vema zifuatwe, ambapo wanane kati ya kumi, walisema watendaji waondolewe panapokuwa na uthibitisho wa vitendo viovu,” alisema Chande.

Akifafanua, Chande alisema utafiti huo pia umeonesha kubadilika kwa matarajio ya wananchi ambapo katika kipindi cha nyuma, kulikuwa na hali ya kutojali miongoni mwa wananchi kulikotokana na utendaji duni wa watendaji.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo