Vigogo 4 Misitu ‘watumbuliwa’


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa misitu wanne na kusimamisha shughuli za uvunaji mazao ya misitu wilayani Rufiji kwa muda usiojulikana, baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.

Maofisa waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, Dk Paul Ligonja, Ofisa Misitu wa Wilaya, Gaudens Tarimo, Ofisa Misitu Yonas Nyambuya na Ofisa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa Wilaya, Seleman Bulenga.

Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo jana wakati akizungumza na watumishi wa wilaya kwenye ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya jumba la maendeleo.

Aidha, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya, Juma Njwayo kukusanya magogo yote msituni na kuyapiga mnada na kuitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kwenda Rufiji kuchunguza leseni za uvunaji walizotoa kwa wilaya hiyo.

Waziri Mkuu alibainisha kwamba wilaya hiyo ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa uvunaji mazao ya misitu bila ya kufuata taratibu licha ya kuwa na maofisa misitu.

“Hakuna mafanikio katika sekta ya misitu kwenye wilaya hii. Nasimamisha shughuli zote za uvunaji mazao ya misitu na watendaji wake kwa sababu hatuwezi kuacha watu wanakata magogo bila kufuata taratibu.

“Haiwezekani Rufiji iwe ‘shamba la bibi’, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye leseni, hadi tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa wanashiriki vitendo vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga mihuri ya Kilwa, kisha fedha wanatia mifukoni,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Rashid Salum kufuatilia maagizo aliyotoa kuhusu kizuizi cha Ikwiriri kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alipokutana na watumishi wa wizara hiyo.

Julai 18 Waziri Mkuu alikutana na watumishi wa wizara hiyo Dar es Salaam na kusisitiza, kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasio na uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.

Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo kupunguza vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu barabarani, baada ya kukosa tija, alitolea mfano wa barabara ya mikoa ya Kusini kuanzia Dar es Salaam yenye vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi kikitumika kukagua mazao ya misitu na maliasili.

Awali, Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengelwa alilalamikia vitendo vya dharau vinavyofanywa na watumishi katika wilaya hiyo, jambo linalosababisha wananchi kukosa imani na Serikali yao.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo