Bodi ya Uhuru yajitumbua


Siku moja baada ya vigogo wa CCM kuhojiwa na wasaidizi wa Rais Johh Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama hicho kuhusu sakata la kuuzwa kwa mtambo wa kuchapisha magazeti wa Modern, malimbikizo ya mishahara na kulegalega uongozi, Bodi ya Kampuni ya Uhuru Publications Limited (UPL) imeandika barua ya kujiuzulu.

Msemaji wa Chama hicho, Christopher ole Sendeka aliiambia JAMBO LEO jana, kuwa hatua iliyochukuliwa na Bodi hiyo ni ya hiari, ikiwa ni muda mfupi kabla ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari, kuhusu uamuzi huo chini ya Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Adam Kimbisa.

“Bodi imeandika barua ya kujiuzulu, sasa ukiniuliza kuwa wamechukua uamuzi huo kutokana na kuibuliwa kwa uuzwaji wa mtambo na mambo mengine, hapo hutakuwa sahihi, wewe kama unahitaji kujua hilo fanya uchunguzi wako,” alisema Sendeka.

Uamuzi wa Bodi hiyo umekuja zikiwa ni siku mbili tangu Rais Magufuli atembelee ofisi za UPL na kuelezwa kuhusu uuzwaji wa mtambo huo na kufuatiwa na mshikemshike wa vigogo wa chama hicho kuitwa kutoa maelezo ya kina kuhusu mambo yaliyoibuliwa na wafanyakazi wa kampuni hiyo.

Habari kutoka ndani ya Chama hicho zilizoifikia JAMBO LEO zilieleza kuwa kazi hiyo ya kuwahoji watu mbalimbali ilifanywa na wasaidizi wa Rais, huku watoa taarifa kuhusu ‘madudu’ hayo, wakiwamo wanahabari na watumishi wa chama hicho, wakiahidiwa kulindwa ili wasifukuzwe kazi au kuwajibishwa na uongozi wa kampuni.

Baadhi ya vigogo hao walilazimika kupanda ndege kuwahi mahojiano hayo yaliyofanyika juzi na jana, huku taarifa zaidi zikieleza kuwa hali imekuwa tete kwa baadhi ya ‘wapigaji’ kutokana na Rais kuonesha wazi kutaka kukirejesha chama hicho katika ramani iliyoanza kupotea.

Juzi Rais Magufuli akifuatana na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana na Sendeka, alifanya ziara ya ghafla katika ofisi ndogo ya makao makuu ya CCM na UPL na kuzungumza na wafanyakazi walioibua sakata hilo.

Miongoni mwa yaliyoibuliwa ni kuuzwa kwa mtambo huo, malimbikizo ya madeni na uongozi kulegalega katika utendaji.

Mtambo huo ulisitisha huduma ya kuchapisha magazeti tangu mwaka 2012 ambapo kwa sasa kampuni hiyo inachapisha katika mtambo wa Jamana kwa Sh milioni 52 kwa mwezi.

Wanaotajwa kuhojiwa ni pamoja na mwenyekiti wa CCM katika moja ya mikoa Kanda ya Kati na kada wa chama hicho ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais kuwa Mkuu wa Wilaya.

“Yupo mmoja alikuwa mkoani alipigiwa simu na kutakiwa kufika leo (juzi) kwa ajili ya kuhojiwa juu ya masuala mbalimbali, likiwamo hilo la mtambo,” alisema mtoa habari huyo.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa baada ya ziara hiyo, baadhi ya vigogo walikuwa wakijadiliana kuhusu suala hilo katika mitandao ya kijamii, huku wakiponda watoa taarifa kwa Rais, “hao nao watashughulikiwa maana walichokuwa wakijadiliana, nacho kimechukuliwa na wahusika. “Rais alitaka kupata maelezo ya kina kuhusu jambo hili, ndiyo maana alituma wasaidizi wake kuhoji watu mbalimbali, wakiwamo waliompa hizo taarifa.”

Gazeti hili lilimtafuta Katibu wa Uchumi na Fedha wa CCM, Zakia Meghji na kumwuliza kuhusu suala hilo, lakini badala ya kujibu alikata simu, hata alipopigiwa kwa zaidi ya mara tatu hakupokea.

Baadaye CCM ilitoa taarifa ya kujiuzulu kwa Bodi hiyo ya UPL, ikieleza kwamba Mwenyekiti wa CCM, Rais Magufuli amepokea barua ya kujiuzulu kwao ambayo nakala yake pia imetumwa kwa Kinana.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo