Jaji Francis Mutungi: Mlezi wa vyama ‘aliyeitibua’ CUF


Mary Mtuka

TAMKO la Septemba 23, mwaka huu lililotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, limekitibua Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kuhalalisha uenyekiti wa Profesa Ibrahim Lipumba aliyesimamishwa uanachama.

Jaji Mutungi ametoa msimamo na mwongozo wake kuwa wanachama wengine waliosimamishwa pia ni halali na viongozi walioathirika kutokana na uamuzi wa kikao cha Baraza la Uongozi la CUF, Agosti 28, mwaka huu, ni viongozi halali.

Ingawa tamko hilo halali kwa mujibu wa sheria, limetokana na utekelezaji wa majukumu ya Ofisi ya Msajili, lakini mapokeo yaliyoakisi fununu za kuwapo upendeleo kwa Profesa Lipumba, ‘yamekoleza moto’ wa mzozo wa kisiasa kwa chama hicho.

Jaji Mutungi akatumia vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa, vikiwamo 10(f) sura ya 258, 8A(1) na kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Usajili wa vyama hivyo, toleo namba 111 la 1992, kufanya upembuzi wa hoja zilizofikishwa ofisini kwake.

Hoja hizo zilikuwa za upande wa Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake wanaopinga kufukuzwa na kusimamishwa uanachama, na majibu ya uongozi wa CUF kuhusu uamuzi unaolalamikiwa. Hatimaye, Jaji Mutungi akaandika, “hivyo baada ya upembuzi kama nilivyobainisha hapo juu, msimamo na mwongozo wangu ni kwamba, Profesa Ibrahim Lipumba bado ni Mwenyekiti halali wa Taifa wa CUF…”

Kwa tamko hilo, Profesa Lipumba akarejea Makao Makuu ya CUF Jumamosi iliyopita, akisindikizwa na wafuasi wake na askari polisi waliokuwa kwenye magari matatu.

CUF imeitisha kikao cha Kamati ya Utendaji itakayojadili msimamo na mwongozo wa Jaji Mutungi kuhusu Profesa Lipumba kurejea katika nafasi yake ya awali, huku kukiwa hakuna dalili za kukubalina na mlezi huyo wa vyama vya siasa.

Wakati Kamati ya Utendaji ikikutana leo, moja ya shughuli zake zikielezwa ni kumhoji Profesa Lipumba kwa ‘uhalifu’ alioufanya ofisi za chama hicho, Buguruni jijini Dar es Salaam, Jumamosi, hali iliyopo sasa ni kama kusema ‘CUF imetibuka’.

Shughuli zinazofanyika sasa, kauli za viongozi na malumbano ya baada ya tamko la Jaji Mutungi, havikielekezi chama hicho kwenye mwelekeo bora wa siasa.

Ndio maana Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, anasema kinachoendelea ndani ya CUF ni sawa na ‘biashara haramu’ inayoweza kukiua chama hicho.

Anaasa kuwa ni wakati muafaka kwa wanaoifanya biashara hiyo wakajulikana na kwamba ni aibu kuvumilia kasoro hizo ziendelee ndani ya chama hicho.

Lakini aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, anaielezea hali ya kisiasa iliyopo hivi sasa ndani ya CUF, inahitaji ushiriki wa mahakama ili kupata suluhu na si Msajili anayedai kutokuwa na mamlaka ya kuchukua hatua alizozitangaza. Kwa mujibu wa Kafulila, Msajili anapaswa kushauri kwa mujibu wa sheria na si kuchukua hatua kama alivyofanya Ijumaa iliyopita.

Mtazamo huo unafanana na ule wa Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani na Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Onesmo Kyauke wanaomkosoa Jaji Mutungi kwa uamuzi wake. Katani anasema tukio la Profesa Lipumba kurejea CUF akisindikizwa na polisi, muda mfupi baada ya kutambuliwa na Jaji Mutungi, ni sawa na ‘kutumika’ kukiharibu chama hicho.

Anaeleza kushangazwa kwake na hatua ya polisi kulinda kile alichokiita kuwa maandamano ya Profesa Lipumba kurejea CUF, licha ya kuwapo katazo la kufanyika kwake (maandamano). Kwa upande wake, Dk Kyauke anamkosoa Jaji Mutungi kwa uamuzi wa kumtambua Profesa Lipumba, kisha anakishauri chama hicho ‘kukimbilia’ mahakamani.

Agosti 5, mwaka jana Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa CUF kwa madai ya kukerwa na hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumkaribisha Waziri Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.

CUF pamoja na vyama vingine vya Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD viliunda Ukawa ukiasisiwa kutoka kwenye Bunge Maalum la Katiba. “Nafsi yangu inanisuta hivi sasa kuendelea na uongozi huku waliokuwa wanaipinga rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Warioba (Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) wakikaribishwa kuwania uongozi wa nchi kupitia Ukawa,” akasema.

Hata hivyo, Profesa Lipumba alitengua kujiuzulu huko, lakini CUF iliendelea na mchakato wa uchaguzi wa kuziba nafasi yake, hali iliyozua vurugu ambazo hazijatulia hadi sasa.

Pamoja na Profesa Lipumba, wanachama wengine waliosimamishwa ni wabunge Magdalena Sakaya (Kaliua) na Maftaha Nachuna (Mtwara Mjini). Pia wamo Naibu Mkurugenzi wa Habari Taifa, Abdul Kambaya, na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) la CUF, Masudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha Kapasha na wanachama Musa Kombe, Habibu Mnyaa na Haroub Shamis.

Suala la msingi ni uamuzi utakaofikiwa na Kamati ya Utendaji ya CUF ili kuwasilishwa kwenye vikao vya juu ikiwa ni sehemu ya kufikia uamuzi unaoweza kukoleza mgogoro uliopo sasa, ama kuufikisha tamati na chama hicho kuendelea na shughuli za kawaida.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo