Hujuma misaada ya waathirika tetemeko haikubaliki


TAHARIRI

KAMA kuna jambo linaweza kuwashitua na kuwasikitisha Watanzania katika kipindi hiki kigumu cha wenzao kuendelea kuugulia maumivu ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera, huku Serikali ikifanya kila njia kuwasaidia, wanatokea watu kuwaibia misaada.

Jana vyombo karibu vyote vya habari nchini, viliripoti taarifa za vigogo watatu mkoani humo, kufungua akaunti inayofanana na iliyofunguliwa na Serikali kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia waathirika wa tetemeko hilo na wao kukusanya fedha na kuzitumia binafsi.

Taarifa hiyo ambayo iliikariri Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, iliwataja Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba, Steven Makonda na Mhasibu Mkuu wa Mkoa, Simbaufoo Swai.

Watatu hao wanadaiwa kufungua akaunti zingine mbali na ile rasmi ya Serikali na kutumia jina hilo hilo la ‘Kamati Maafa Kagera’ kwa lengo la kujipatia fedha. Kwa kuwa kwa mujibu wa Rais John Magufuli jana walifikishwa mahakamani hatutaingia kwa undani kuhusu suala hilo.

Kama kweli hilo limetokea, ndilo ambalo Rais Magufuli mara nyingi amekuwa akilikemea na kuliita ni upigaji dili, lakini hili linauma zaidi, kwa sababu dili hizo zinapigwa kwenye migongo ya waathirika ambao hivi sasa hawana nyuma wala mbele.

Matukio kama haya ya kutumia fursa potofu kama hizi, yamekuwa yakiripotiwa sehemu nyingi na hayana tofauti na wale ambao hukimbilia sehemu za ajali na badala ya kuokoa watu, huwapora mizigo na fedha mifukoni bila soni wala huruma.

Mengine ni kama yanayojitokeza misibani kwa baadhi ya watu kujifanya wana majonzi, lakini wakitumia fursa za misiba kujinufaisha kwa kukodi magari kwa gharama hewa na wengine kulipia majeneza kwa gharama hewa pia.

Wote hawa kama alivyopata kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere (marehemu) ni ‘mazi ga nyanza’, kwamba ni wale wale walio na fikra zinzofanana za kutumia maafa kujinufaisha kimaisha. Watanzania tunapaswa kuwa na huruma, tunapaswa kusaidiana, lakini pia kushukuru wanaotusaidia kupunguza machungu yanayotupata.

Inakuwa si sawa watu kujinyima wakiamini wanachangia walengwa, lakini kumbe michango yao inaingia mifuko haramu. Kama kweli kitendo kama hiki kitakuwa kimefanyika, basi kitakuwa kimetokana na nguvu za shetani, ambacho hata Mungu atakiadhibu na tunaomba ikithibitika kuwa dili hilo lilifanyika basi sheria ifuate mkondo wake, ili liwe onyo na funzo kwa wengine wenye nia ovu kama hiyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo