JPM: Waathirika Kagera wajijengee


RAIS John Magufuli amesema Serikali itarekebisha miundombinu iliyoharibika mkoani Kagera kutokana na tetemeko la ardhi la wiki iliyopita, lakini akawataka waliobomokewa nyumba, wajipange kuzirekebisha.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Gerson Msigwa, imeeleza kuwa Rais Magufuli alisema hayo jana Ikulu Dar es Salaam, wakati akipokea taarifa ya maafa yaliyosababishwa na tetemeko hilo, kutoka kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa iliyoeleza kuwa tayari Sh bilioni 3.6 zilikuwa zimekusanywa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Ikulu, Rais Magufuli alisema Serikali pekee yake haitaweza kujenga nyumba zote zilizobomoka, ambazo taarifa ya Waziri Mkuu ilisema zilizobomoka ni 2,063; zilizo kwenye hali hatarishi 14,081 na zilizopata uharibifu mdogo ni nyumba 9,471.

Madhara mengine yaliyotokea ni pamoja na vifo vya watu 17 na majeruhi 440 huku watu 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.Kuhusu miundombinu iliyoharibika, Rais Magufuli alisema Serikali itarekebisha shule, vituo vya matibabu, barabara na huduma nyingine za kijamii.

Pamoja na kupokea taarifa hiyo, Rais Magufuli amepokea mchango wa fedha taslimu Dola za Kimarekani 200,000, sawa na takribani Shilingi za Kitanzania milioni 437, kutoka kwa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni.

Mbali na msaada huo, pia amepokea taarifa ya mchango wa mabati, blanketi na magodoro vyenye thamani ya Sh milioni 115 kutoka kwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa tetemeko hilo.

Rais Magufuli aliwashukuru wote waliojitoa kusaidia waathirika akiwemo Rais Museveni wa Uganda; Rais Kenyatta wa Kenya na Rais Paul Kagame wa Rwanda, ambao wamempigia simu za kumpa pole na tayari wametoa misaada yao.

Pia alishukuru nchi mbalimbali, mashirika, wafanyabiashara, watumishi wa umma na watu binafsi na kuongeza kuwa michango hiyo ina umuhimu mkubwa, katika kukabiliana na athari za maafa hayo. 

Aidha, Rais Magufuli amewasihi Watanzania kupuuza watu wanaotaka kutumia maafa haya kueneza chuki dhidi ya Serikali na ameweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna teknolojia ya kutabiri tetemeko la ardhi na hilo halikuletwa na Serikali.

Dk Magufuli amesema hata mataifa makubwa yenye maendeleo makubwa ya uchumi na teknolojia, yamekuwa yakikumbwa na tetemeko la ardhi na kusababisha vifo vingi na uharibifu mkubwa wa mali.

“Nilikuwa najaribu kuangalia kwa mfano nchi kama China mwaka 2014; watu 617 walipoteza maisha, mwaka 2013 walipoteza maisha watu 193, mwaka 2010 walipoteza maisha watu 2,998 na mwaka 2008 China ilipoteza watu 98,712.

“Ukijaribu kuangalia Japan, nchi iliyoendelea na ina utaalamu wa hali ya juu sana, kwenye mwaka 2016 April 14, ilipoteza watu sita, baada ya siku mbili, Aprili 16, 2016 tetemeko likatokea tena na likaua watu 35.

“Mwaka 2012 likaua watu 3, mwaka 2011 likaua watu 15,904 mwaka 2008 likaua watu 12, mwaka 2007 likaua watu 11, mwaka 2004 liliua watu 40 na mwaka 1923 liliua watu 142,800 na hiyo ni Japan,” alisema.

Katika taarifa yake, Waziri Mkuu alisema Serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kupeleka chakula, huduma za matibabu na hifadhi za dharura kwa waathirika na imeratibu ukusanyaji wa michango kutoka sehemu mbalimbali.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo