Tanzania yataka wawekezaji wabanwe kodi


Mwandishi Maalumu, New York

Dk Augustine Mahiga
TANZANIA imezitaka nchi zilizoendelea kuwajibisha wawekezaji na kampuni zao ili walipe kodi.

Hayo yalielezwa juzi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk Augustine Mahiga wakati akihutubia Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa (UN) na kutumia fursa hiyo kuelezea vipaumbele vya Serikali ya Tanzania.

Waziri Mahiga alifafanua kuwa, lengo namba 16 la maendeleo endelevu linatambua kuwa rushwa inakandamiza juhudi za kupambana na umasikini na kuleta usawa wa jinsia, kwani inazuia fursa.

Katika muktadha huo, alisema serikali ya Tanzania imeanzisha vita dhidi ya rushwa kwa kuhuisha uwazi, uwajibikaji na usahihi katika utoaji huduma kwenye taasisi zake.

Alisisitiza kwamba Serikali imeweka misingi mizuri ya uwajibikaji inayomtaka mtumishi wa umma kutambua kwamba wajibu wa kwanza ni kutoa huduma bora na kwa wakati kwa umma.

“Juhudi hizi za Serikali za kupambana na rushwa hazitazaa matunda bila kuungwa mkono na jumuiya ya kimataifa. Nchi zilizoendelea zinatakiwa kuwajibisha wawekezaji wao pamoja na kampuni zao ili kulipa kodi stahiki,” alieleza zaidi Waziri Mahiga.

Aliongeza: “Ni lazima wawe tayari kurudisha mali na fedha zilizoibwa kutoka nchi zinazoendelea na kuzificha katika nchi zao ili mali na fedha hizo zisaidie maendeleo yetu.”

Kuhusu fursa za jinsia na uwezeshwaji wanawake, Waziri Mahiga alielezea juhudi ambazo zimefanywa na Serikali katika kuwezesha wanawake ikiwamo kushika ngazi za juu za uamuzi kuanzia Serikali Kuu hadi Bunge na uwezeshwaji kiuchumi.

Katika kuthibitisha kuwa Tanzania inazingatia usawa wa jinsia katika uteuzi wa ngazi za uamuzi, Waziri Mahiga alieleza kwamba, kwa mara ya kwanza wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Rais John Magufuli aliteua mwanamke kuwa Makamu wa Rais.

“Uteuzi huu unathibitisha nia ya nchi yangu ya kuona wanawake wengi zaidi wanakuwa kwenye nafasi za juu za uamuzi. Na ajenda hii ya uwezeshaji wanawake sasa inamilikiwa na wanawake wenyewe,” alisisitiza Waziri. Kwa vijana, kiongozi huyo wa ujumbe wa Tanzania aliyemwakilisha Rais wa Tanzania, alisema.

Vijana ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa lolote, si tu kwamba ni viongozi wa kesho lakini pia wa sasa.

Alihadharisha kwamba kutowapa kiupaumbele vijana ni kujitafutia matatizo makubwa kutokana na alichosema ni rahisi kurubuniwa na makundi hatari kwa ustawi wa jamii na Taifa.

“Kutoka na kwamba idadi ya vijana ni kubwa, Serikali inachukua hatua mbalimbali za kuwezesha kundi hili la jamii ambalo ni muhimu katika utekelezaji wa ajenda 2030. “Na ili vijana watekeleze jukumu hilo, Serikali imeanzisha mfuko wa maendeleo wa vijana ambao hadi Machi jumla ya Sh bilioni 1.6 zilipelekwa kwa vikundi 284 vya vijana,” alisema.

Kuhusu elimu, eneo ambalo ni kipaumbele kingine cha Tanzania, Waziri alieleza kuwa upatikanaji elimu jumuishi na ya viwango, ndicho kipaumbele cha Serikali kwa kuwa inaamini kuwa, elimu ni ni nyenzo muhimu kwa maendeleo endelevu.

Alifafanua, kuwa Serikali inahakikisha kwamba watoto wote wanapata elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari. Pamoja na kutoa elimu bure, imeboresha mitaala yake kwa kuzingatia mahitaji ya karne ya 21.

“Alipoingia madarakani, Rais Magufuli alitangaza kuanzia elimu ya msingi hadi sekondari kuwa bure. Serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 263 ili kuhakikisha elimu inakuwa bure kwa wote.

Vipaumbele vingine vya Tanzania ambavyo Waziri aliviainisha ni pamoja na mikakati ya Serikali imejiwekea katika utekelezaji wa mkataba wa mabadiliano ya tabia nchi utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na kukabiliana na ugaidi ambao alisema ni tatizo ambalo linaendelea kukua na kuwa tishio hata kwa Afrika Mashariki.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo